Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kwanza ya kuchangia katika Wizara hii. Nianze tu kwa kuipongeza Wizara, Waziri, Mheshimiwa Profesa Maghembe; Naibu Waziri, Mheshimiwa Injinia Ramo na watendaji wote wakiongozwa na Katibu, Mkuu Meja Jenerali Milanzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Rais wa nchi yetu kwa kuwateua hawa lakini kwa kulinda maliasili ya nchi yetu na kuonesha kwamba ana nia nzuri ya kuendeleza utalii kwa kununua ndege ambazo zitakuwa zinatoa watalii maeneo mbalimbali na kuwaleta hapa kwa ajili ya kuongeza mapato ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze leo kwa kutumia hotuba zote hizi mbili ya Waziri na Kamati, yote ambayo tulitegemea kusema humu ndani hasa mimi naona wamezungumzia maeneo mengi. Nianze kwa kuangalia kitabu cha hotuba ya Waziri, ukurasa wa 17, ibara 36 wanasema:-
“Dhana ya ushirikishwaji jamii katika uhifadhi wa wanyamapori ilianzishwa kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanashiriki katika uhifadhi na kunufaika kwa mujibu wa Sera ya Wanyamapori ya mwaka 2007”.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye maeneo yangu ya Bunda na kwa bahati mbaya lugha inakuwa tofauti nikisema tembo inakuwa kosa basi niseme ndovu. Nimshukuru Waziri katika msimu wa kilimo wa mwaka jana na mwaka huu wametusaidia kuleta magari na askari ili kuzuia ndovu wasije kwenye maeneo ya makazi ya watu na kula mazao yao. Nina ombi maalum kwa Waziri kwamba kwa sasa wakulima wale wamelima sana na mazao yao yako kwenye hatua nzuri, kwa mwezi wa Tano, Sita na Saba watusaidie kupeleka magari na askari wa wanyamapori ili wananchi waweze kuvuna kwa msimu huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kitabu hiki cha hotuba ukurasa wa 19, ibara ya 39 inasema, jumla ya shilingi milioni 567.5 zimelipwa kwa wananchi ambapo shilingi milioni 504 ni kifuta jasho. Miongoni mwa Wilaya zilizolipwa hizo hela ni Bunda, nikushukuru Waziri kwa sababu amewakumbuka watu wa Bunda kwa Vijiji vya Unyari na Kiumbu. Mheshimiwa Naibu Waziri alifika Kijiji cha Maliwanda ambacho kimeathiriwa sana na wanyamapori lakini kwa bahati mbaya katika malipo haya hawakupata na Kijiji cha Sarakwa. Nilishaenda Ofisi kwao wakaniahidi kwamba watafanya marekebisho na hawa watu watapata malipo yao ya kifuta jasho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapohapo nizungumzie hili la kifuta jasho. Mwaka jana katika hotuba hii ya bajeti tumezungumzia marekebisho ya kanuni za wanyamapori kuhusu kifuta jasho. Wanasema kutoka kwenye mpaka, mpaka kwenye eneo ambalo ni kilomita tano kutoka kwenye mpaka ambao wananchi na wanyamapori wanaishi, mwananchi atakayeliwa mazao yake zaidi ya kilomita tano analipwa shilingi laki moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuseme ndovu amekula mazao kilomita arobaini kutoka eneo la mpaka analipwa shilingi laki moja kwa heka moja. Iko sheria pale kwamba kama umelima heka arobani halafu ndovu wamekuja kwenye shamba lako wamekula heka arobaini unalipwa heka tano tu kwa shilingi laki moja. Kwa lugha nyingine unalipwa shilingi laki tano, kwa heka 40 unalipwa heka tano tu heka 35 inakuwa sadaka. Sasa ni vizuri tukaangalia namna gani ya kurekebisha sheria hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia kwenye kitabu hiki namna gani watu wanaozunguka wanyamapori wananufaikana nao. Katika eneo langu la Unyari miaka mitatu iliyopita ndovu walivunja jengo la watoto na akina mama wajawazito. Tukajitahidi kujenga jengo hilo na Serikali ikaahidi kwamba itaezeka na kufanya finishing. Niishukuru Wizara imetoa shilingi milioni 50 jengo lile linaendelea vizuri lakini alipokuja Waziri wa Afya amesema jengo lile kwa sababu tumelijenga vizuri liwe kituo cha afya. Kwa sababu ya sera yetu, nafikiri Mheshimiwa Waziri ni vizuri sasa akatusaidia hela nyingine kwa sababu inahitajika pale shilingi milioni 50 nyingine ili kubadilisha maeneo yale yote yawe kituo cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni matumaini yangu kwamba tutasaidiana katika jengo hili ili kiwe kituo cha afya na ikiwezekana hata kama litaitwa Profesa Maghembe siyo mbaya ili mradi tu umetutengenezea eneo limekuwa zuri zaidi kwenye maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna matatizo ya mipaka kati ya vijiji kumi na tano na Pori la Akiba la Grumeti. Mgogoro huu ni wa muda mrefu, tumesema sana na tunafikiri ile Kamati iliyoundwa ya Wizara tatu itafika kwenye eneo letu na kuweza kuangalia mipaka hii. Ipo hoja kwamba mwaka 1994 wakati eneo hilo linachukuliwa kutoka open area kuwa game reserve (pori la akiba), wananchi hawakushirikishwa. Kwa hiyo, tunafikiri kuwa sasa ni muda muafaka kuangalia mipaka hiyo na Kamati imesema ili tuweze kujua ukweli uko wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi ni kwamba wakati hilo pori la akiba linachukuliwa ambalo maarufu kule kwenye maeneo yangu kama Kawanga kulikuwepo na malambo mawili yaliyochimbwa na wananchi kwa ajili ya kunywesha mifugo. Yale malambo mawili sasa wanyamapori ndiyo wanakunywa maji lakini sisi huku chini hatuna maji ya kunywa. Mheshimiwa Waziri anajua mpaka wetu ni Mto Rubana, sasa watu wakienda katika maji yale wanafukuzwa kwa sababu wakivuka Mto Rubana tu wameenda porini. Kwa hiyo, tulifikiri ni muhimu sana Serikali kuja kuangalia namna ya kuchimba malambo upande wa pili ili ng’ombe wawe wanapata maji yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumzia kero ya mipaka ambayo ni ya muda mrefu lakini kuna vijiji vya Mgeta, Tingirima, Kandege na vyenyewe havikupata huu mgao wa kifuta jasho. Ni vizuri sasa tukaona ni namna gani wanaweza kuzingatiwa, lakini Maliwanda ni kijiji cha kwanza kuzingatiwa katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo nilitaka nichangie hayo, ahsante sana.