Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busega
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami napenda nikushukuru sana kunipa nafasi hii ili kuweza kuchangia katika hotuba hii ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niungane na msemaji wa kwanza, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri pamoja na wataalam wao kwa kuweza kuandaa bajeti hii ambayo wote tumeisikiliza hapa kwa makini sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Maliasili na Utalii ni nyeti sana. Nadhani kama Waheshimiwa Wabunge tunatakiwa tuiangalie kama moja ya Wizara ambazo zinaingiza mapato makubwa sana katika uchumi wa nchi yetu. Wizara hii jinsi ilivyo na inavyofanya kazi ina changamoto nyingi sana na hasa ukizingatia suala la utalii kwa mfano ndiyo sura ya nchi ndani na nje ya nchi yetu lakini kuna vitu ambavyo havijakaa sawa. Kwa maana gani? Kwa maana kwamba kunapaswa kuwa na uwiainishaji kati ya wageni wanaoingia nchini na watu walioko hapa nchini, watu wanaokuja kufanya shughuli hapa nchini na sisi Watanzania tulioko hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yakiunganishwa vizuri na yakifanyika vizuri yatachochea nchi yetu kupata watalii wa kutoka na kuongeza kipato kwa ajili ya matumizi ya Watanzania. Bajeti yetu hii kwa mfano Mheshimiwa Waziri kasema hapa kwamba kwa mwaka 2015/2016, Wizara hii iliweza kuchangia zaidi ya bilioni 1.9 dola za Kimarekani na mwaka huu unaokwisha wa 2016/2017 imechangia zaidi ya dola bilioni mbili, ni hela nyingi sana hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kuna ukiritimba mkubwa sana mtu anapokuja hapa Tanzania anakutana nao. Mtalii anapoingia hata pale airport, watu wa Idara ya Uhamiaji wanavyowapokea wale wageni, lugha wanayoitumia si lugha ambayo inapaswa kutumika kwa kukaribisha wageni. Kuna haja sana Mheshimiwa Waziri wa Utalii, ajaribu kuongea na hizi Idara ikiwezekana washirikiane kwa karibu zaidi na wawape fursa ya kutembelea vivutio mbalimbali ili wajue thamani ya kumpokea mgeni pale airport na kumpa treatment inayostahili kwa sababu ni mgeni anayekuja kwa ajili ya kujenga nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hii ina changamoto nyingi, ina tozo kibao, tozo zaidi ya 36. Hizi kodi na tozo hazina afya au tija kwa ajili ya kujenga sekta hii. Kuna haja ya kuangalia namna ya kupunguza hizi tozo na kodi ili kusudi tuweze kupata mapato mengi zaidi kutokana na watu wanaokuja hapa nchini kwa ajili ya shughuli za kitalii au shughuli nyingine mbalimbali. Haya tunayoyasema hatujaanza leo hata mwaka jana tulishauri. Ningeomba sana Wizara ya Fedha na Wizara ya Maliasili na Utalii wajaribu kukaa na kuona kodi na tozo zipi ziweze kuangaliwa upya. Hii itaongeza ufanisi wa kupata mapato makubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ina changamoto moja nyingine kubwa sana. Wizara hii imepelekea wafugaji katika nchi yao sasa kuonekana ni yatima kitu ambacho ni tatizo kubwa sana. Ukiangalia hivi mfugaji anapokwenda akaingiza mifugo ndani ya hifadhi au kwenye msitu na mtu anayekata misitu kwa ajili ya kuchoma mkaa na kadhalika ni nani mharibifu zaidi ya hapa? Kila siku tunaona magunia ya mkaa zaidi ya milioni 50 yanaingia Dar es Salaam ambayo yanatokana na kukata miti ambao ni uharibifu wa mazingira lakini mfugaji anaonekana ndiyo haramu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wakati Mheshimiwa Waziri anakuja ku-windup hotuba yake tunataka tuone ni namna mfugaji katika nchi hii naye anapewa nafasi na kuthaminiwa. Kwa mfano kule Muleba, Mkuu wa Wilaya anasema kwamba amewapa notice wafugaji wahame, waende wapi hawa ni Watanzania. Pili, ukisema wahame ina maana kwamba waanze kutafutana wewe umetokea wapi, kila mmoja amfukuze mwenzake. Tutajenga situation ambayo siyo nzuri kwa ajili ya nchi yetu na tutaanza kuleta ubaguzi ambao hauna tija yoyote kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana hili suala la mifugo na hifadhi, ndiyo tunahitaji tuwe na hifadhi lakini naomba tuziangalie sheria. Kuna baadhi ya mashamba mengine yalikuwa ya mifugo sasa hayafanyi kazi, kwa nini tusiyakate yale mashamba yakatumika kwa ajili ya wafugaji kufugia mifugo yao na kutoka kwenye hifadhi? Hata hivyo, tujue kwamba idadi ya wananchi inaongezeka kila kukicha lakini ardhi haiongezeki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hali hiyo ni lazima kuwe na mustakabali sasa wa kitaifa wa kuangalia kwamba tunahitaji kuhifadhi misitu na hifadhi zetu wakati huohuo wananchi nao wanahitaji kutumia mazao ya mifugo, kufuga mifugo na kufanya kilimo chao, vinginevyo tutachochea vurugu ambayo haina tija kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kuwepo na doria dhidi ya ujangili na biashara haramu ya nyara za Serikali. Hii maana yake ni kuwe na vikosi maalum visaidie kulinda hifadhi zetu hizi au maliasili yetu hii. Wenzetu siku hizi wana teknolojia mpaka kutumia zile ndege ambazo haziendeshwi na rubani (drones) na wana mpaka wale mbwa maalum wa kunusa, naomba tuongeze hiyo jitihada ili kusudi tuhifadhi na kulinda maliasili yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tuitangaze Tanzania. Mimi nimefurahi juzi nilipanda ndege ya Bombadier wameweka kwenye ndege air flying magazine wameonesha baadhi ya picha na mahali vilipo na kuutangaza utalii wa nchi yetu, ni kitu kizuri sana. Tunapaswa tutoke pale tulipo, sasa tumepata ndege zetu lakini vilevile suala la kutangaza utalii nje ya nchi ubadilike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Bodi ya Utalii (TTB) ipewe mamlaka na ipewe fedha kwa ajili ya kuendesha utalii nje ya nchi. Haiwezekani Ngorongoro wanaenda kutangaza kivyao, TANAPA kivyao, sijui nani kivyao, haiwezekani wote wanatoka Tanzania hawa. Hii Bodi ingewezeshwa, tena bahati nzuri imepata Mwenyekiti mzuri sana, Advocate Mihayo, ni wakili mzuri anajua vizuri sana haya mambo. Nina imani kabisa kwamba akiwezeshwa na Bodi ikiwezeshwa tutafanya kazi nzuri sana ya kuitangaza nchi yetu nje ya mipaka yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala lingine ambalo lipo na naomba kwenye kitabu chako ukurasa wa 19 umekosea sana, unasema wananchi walindwe na mali zao dhidi ya wanyama waharibifu, tuna tatizo la tembo wanaharibu mazao na mali za binadamu, lakini bado watu hawapati fidia inavyotakiwa. Tunaomba Wizara yako iunde kikosi maalum ambacho kitasaidia kwa ajili ya kuhifadhi na kuwalinda wananchi pamoja na mali zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitabu chako una-refer kwamba Magu wanapata hicho kifuta jasho na kifuta machozi. Magu hawapakani na Hifadhi ya Serengeti isipokuwa ni Wilaya ya Busega, zamani ilikuwa ni sehemu ya Magu. Naomba rekodi za Mheshimiwa Waziri azibadilishe isomeke Busega badala ya Magu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna kuboresha miundombinu inayopakana na hifadhi, nimeshamwomba Mheshimiwa Waziri barabara ya Kijereshi naomba anisaidie waitengeneze kwani inasaidia sana kuongeza idadi ya watalii wanaoingia Serengeti na iko Busega. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri hili uweze kulifanyia kazi ili kusudi sasa tuweze kuimba wimbo mzuri wa kuongeza watalii na kuongeza mapato katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri kuzingatia sana suala la Ushirikishaji wa Jamii katika Uhifadhi (WMAs)…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hotuba hii.