Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru kwa kunipatia nafasi hii. Pia nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia kuwa na afya njema na kuniwezesha kuchangia katika hoja iliyopo Mezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara ya kwanza nataka niishukuru na kuipongeza timu ambayo ilisimamia kuhakikisha Tanzania concession fee inapita na kuifanya Serikali iweze kupata mapato. Nitataja kwa majina ni akina nani walisimamia hiyo timu, ilikuwa chini ya Mwenyekiti wa Bodi iliyopita Ndugu Modestus Lilungulu, Mama Chijoriga, Ndugu Fumbuka, Mama Wilmo, Mheshimiwa Jenista Mhagama na mimi mwenyewe Riziki Lulida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtajiuliza kwa nini tumefikia hapo? Tanzania tulifikia mahali ambapo uchumi wetu ulikuwa nyuma, watu walikuwa hawataki kulipa tozo ambayo ni halali katika nchi hii. Tozo ya dola nane katika hoteli ni hasara kubwa katika nchi hii na uchumi mkubwa unakwenda kwa wawekezaji sisi wenyewe Watanzania tunakosa mapato. Nilimwomba Waziri Mkuu ashirikiane na Wizara watufanyie semina, namshukuru juzi tumepata semina ya kwanza, bado haijatosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haijatosha kwa vile watu wengi au baadhi ya Wabunge bado hawana uelewa. Ili kujenga uelewa kwa Wabunge wapya, kwanza watembezwe katika maeneo husika wajionee kiasilia. Leo unaona mwenye hoteli anatoza dola 500 anataka atoe dola nane lakini jiulize TANAPA ndiyo wanajenga barabara, wanapeleka maji, TANAPA na Ngorongoro ndiyo wao wanapeleka maaskari kutunza maeneo yale ili watalii wawe katika usalama. Je, mnaposimamia tozo hizi ziendelee kuwa kwao sisi wenyewe tuendelee kupata tabu, ni nini hicho? Maana yake hatujafunguka. Ili tufunguke, naomba tena tuje tufanyiwe semina mbalimbali ili watu wapate uelewa (awareness creation) kwa ajili ya Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha mwekezaji anaingia ndani ya mbuga, ana hoteli lakini anaingiwa na kigugumizi cha kutotaka kulipa kodi na anatumia mbinu zote mpaka kwenda mahakamani toka mwaka 2007 na ndiyo sasa hivi concession fee imeruhusiwa na tutalipa katika fixed rate ambapo uchumi wa nchi utaruka. Baadhi ya Wabunge mnasema tusilete hizi tozo, kwa faida ya nani? Tuna ajira ndani ya TANAPA, watoto wetu, ndugu zetu wanafanya kazi watapata wapi mishahara? Kuna tour operators ambao wanakuja kufanya kazi Tanzania na wana wafanyakazi, kama tozo hizi mnataka zirudi kwa upande wa pili hela hii itapatikana wapi? Ndiyo maana nasema tupewe semina tena ili kujenga uelewa wa Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nizungumzie Mbuga kubwa ya Selous. Selous ni mbuga ya kwanza kwa ukubwa Afrika, lakini ni mbuga kubwa duniani lakini hakuna chochote kinachofanyika ndani ya Selous hata mapato hayaonekani. Kuna corridor ambayo inatoka Mozambique inakuja Tanzania, kila mwaka tembo, simba, chui na nyati wanakuja Tanzania, haijatangazwa hata siku moja, kila mwaka inatangazwa Mbuga ya Serengeti. Kwa nini mnaiacha Selous isitangazwe halafu mnaridhia kuwapa percent ndogo ya 17.2. Jamani tufike mahali tufunguke tuinue uchumi huu kwa kuiongezea pesa za promotion ili Selous ifanye kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Selous na ukubwa wake lakini two third ya Selous ipo Mkoa wa Lindi na Mwenyezi Mungu ameujalia Mkoa wa Lindi kuna fukwe kubwa za bahari kuanzia Lindi mpaka Mtwara. Kwa nini Selous isingefunguka ili ikasaidia uchumi wa kusini, Selous imefungwa. Ni uwindaji na ujangili kwa kwenda mbele matokeo yake tunapigania uchumi ambao umefungwa na baadhi, sielewi kama ni makusudi au ni dhamira. Nataka kesho Waziri atakapokuja kufunga hoja yake aniambie kwa nini Selous haiwi utilized. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwenda Liwale kwenye Selous yenyewe hakuna barabara, kutoka Nangurukuru kwenda Liwale mpaka Nachingwea ambayo Selous inachukua asilimia 2.3, hakuna barabara. Nataka Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano akishirikiana na Waziri wa Maliasili na Utalii watujibu kwa nini wameifunga Mbuga ya Selous isifanye kazi? Imefikia mahali tunajiuliza, tunataka uchumi endelevu na uchumi upo na wanakuja wageni wakileta fedha za kigeni lakini unaona ajabu Selous haitumiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia uchumi wa utalii ambao uko ndani ya Tanzania na ukitaja Tanzania ni lazima na Zanzibar uitaje. Utalii huu Bara unaonekana lakini Zanzibar haionekani. Ili kuondoa umaskini ni lazima kuhakikisha maeneo yote haya mawili yanaendelezwa kiutalii. Maana yake mtalii anatoka Ulaya akiwa na package kuwa anaingia Serengeti, Ngorongoro anamalizia Zanzibar, kwa nini Zanzibar pesa hakuna, kwa nini Zanzibar wasifunguke na utalii huu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo madogo kama Seychelles, ni nchi ndogo lakini utalii na uchumi wao ni mkubwa lakini Zanzibar imedorora. Lazima tujiulize kuna nini Zanzibar mpaka utalii wake uko mikononi mwa wajanja na Wazanzibari wenyewe inabidi wafunguke. Humu ndani kuna Wazanzibari, tumieni fursa yenu kuiona Zanzibar inakwamuka na utalii wa Zanzibar unafanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mwenyekiti wa Kupambana na Ujangili ndani ya Bunge, nataka kuzizungumzia corridors. Corridors kubwa za tembo Tanzania moja ipo Rukwa (Rukwati) na nyingine ipo Niassa (Mozambique). Corridor ya Rukwa (Rukwati) ambayo inatokea Zambia inakuja mpaka Katavi haitangazwi, vilevile ya kutoka Mozambique kuja mpaka Tanzania haitangazwi matokeo yake wameingia wafugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikupe taarifa, nikiwa na mwenzangu Mheshimiwa Jenista Mhagama, tulikutana na kundi la ng’ombe, wale wafugaji wakiwa na silaha wanaingia ndani ya mbuga. Tukajiuliza wanakwenda kufanya nini ndani ya mbuga, kuna tembo, simba, faru na nyati, kuna harufu kubwa ya baadhi ya wafugaji kushirikiana na majangili. Hivyo, Wabunge mtapendelea ufugaji lakini mnashindwa kuelewa kuwa hao wafugaji sio wote ni wafugaji wengine wanatumika. Hivyo, elimu ya wafugaji itolewe na wenyewe wafunguliwe kuwa wengine wanatumika ndiyo maana unaona ujangili unaingia ndani ya mbuga kwa kupitia hao wafugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, sina mengi sana, nawashukuru sana.