Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Angelina Adam Malembeka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Nami naungana na wenzangu kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri wote na Manaibu Waziri kwa kazi nzuri wanayoifanya. Kwanza niseme kwa moyo wangu wa dhati naipongeza Hotuba ya Waziri Mkuu kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika cchango wangu nitaanza na suala la ukusanyaji wa mapato. Kwa kuwa ukusanyaji wa mapato ni suala la Muungano, napenda pia tuiangalie bandari yetu ndogo ya Mkokotoni. Bandari ile huwa inachukua mizigo ya kwenda Tanga, Mombasa, Dar es Salaam na maeneo mengine kimya kimya. Sasa naona ni vizuri tuiangalie bandari yetu ya Mkokotoni tuweze kuiboresha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, katika bandari yetu ya Mkokotoni ni vizuri pia tukaandaa kivuko ili tuweze kuwasaidia wananchi wa Jimbo la Tumbatu. Wananchi wa Jimbo la Tumbatu kwanza hakuna gari hata moja, siyo kwamba Serikali imeshindwa kutokana na miundombinu iliyokuwa kule, hakuna.
Sasa ni vizuri basi tuwasaidie kuwe na kivuko cha uhakika kupitia ukusanyaji wa mapato utakaotokana katika bandari ile. Kabla sijaendelea kuchangia, napenda nikumbushe; wakati nachangia hotuba ya Mheshimiwa Rais, nilishasema kwamba inawezekana na itawezekana ifike wakati Waheshimiwa Wabunge tuanze kupimwa akili kabla ya kuingia Bungeni. (Makofi, Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kanuni zipo, watu wana akili zao timamu, lakini wao wamegoma wenyewe kuongea kwa idadi yao, halafu mwenzao akiongea, wanamtilia fujo.
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina akili zangu timamu nimetumwa na wanawake wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kuja kuwasemea.
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Siwezi kuja hapa nikasaini posho ya mwezi ya kikao…
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: …halafu nikakaa kimya.
MBUNGE FULANI: Taarifa!
MWENYEKITI: Mheshimiwa Malembeka, naomba ukae, kuna taarifa!
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: …halafu nikakaa kimya.
MBUNGE FULANI: Taarifa!
MWENYEKITI: Mheshimiwa Malembeka, naomba ukae, kuna taarifa!
MWENYEKITI: Mheshimiwa Malembeka, endelea.
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa mwenyekiti, ahsante. Kwanza taarifa yake naikataa kwa sababu hajitambui.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukusanyaji wa mapato ni wa Muungano, ndiyo maana na Mawaziri wa Fedha kule Zanzibar na hapa wapo. Sasa kwa kuwa yeye hajui ukusanyaji wa mapato ni suala la Muungano, naomba akajifunze na aende kule Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba unilindie muda wangu na ninaendelea. La pili nataka nikuhakikishie, kwa umri niliokua nao, sijawahi kumwambia housegirl wangu aache kazi kwa ajili ya kuangalia TV kwa sababu najua madhara yake. Mboga zitaungua, kazi zitakuwa hazifanyiki na ana muda maalum kwa kufanya ile kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani mtu umetumwa na Jimbo lako, unkuja hapa unashindwa kuchania eti kwa sababu ya TV. Mbona housegirls wenu mnawakataza kuangalia TV? Mna matatizo gani? Huko kwenye TV kwenyewe kuna mambo yanafanyika ambayo hayaruhusiwi kuonekana hadharani. Watu wanabadilkishana Tai, watu wanapaka poda, watu wanabadilishana vipindi, hatuonyeshwi moja kwa moja. Vinazuiwa! Kwa nini Bunge mnaling’ang’ania hivyo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika ukurasa wa 12, suala la viwanda. Naipongeza Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri inayoifanya. Ni mikakati iliyojipanga kwa ajili ya kuboresha na kuanzisha viwanda kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba katika mkakati ule, tuangalie upya wawekezaji wetu kutokana na kwamba kuna baadhi ya wawekezaji ambao wanapenda sana kuwanyanyasa wananchi wetu wakiwepo vijana wanaofanya kazi katika maeneo yale. Ninafurahia viwanda viwepo na vigawanye katika Kanda mbalimbali ili kila Mkoa uweze kufaidika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi pia ni mdau wa Jimbo la Ukonga, nina nyumba yangu kule na nimekuwa Diwani kwa miaka kumi. Kwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Ukonga Chama chake kimemkataza kusema, naomba niseme haya kwa niaba ya Mbunge wa Ukonga ambaye kanyamaza. (Makofi/Vigelegele/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Ukonga nataka nizungumzie Barabara. Kuna barabara iliyoanzishwa miaka ya nyuma, naomba Serikali imalizie. Ni barabara ya Chanika - Kitanga mpaka Masaki, kuna barabara ya Chanika - Homboza mpaka Masaki, kuna barabara ya Mvuti kuelekea Dondwe, barabara ya Pugu – Majoe - Mbondole, barabara ya Mbondole -Msongola mpaka Mbande, barabara ambayo inatoka Banana – Kitunda - Kivule hadi Msongola.
Barabara hizo ziliweza kufanyakazi na wananchi wana shida na barabara zile na Mbunge wao amekatazwa kusema; ninaomba kama Mbunge wa Viti Maalum mwenye hisia na Jimbo la Ukonga, nalisemea Jimbo hilo. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado nikiwa na uwakilishi wa wananchi napenda niingie katika ukurasa wa 54 Sekta ya Afya. Katika Jimbo la Ukonga, bado tuna Hospitali ya Kivule. Naishukuru Serikali hii imetenga fedha ya kuongeza kwa ajili ya kukamilisha hospitali ya Kivule.
Naomba Serikali isaidie pia kwa ajili ya Zahanati.
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: …ilianzishwa kwa nguvu kubwa ya Mheshimiwa Jerry Silaa akiwa Mstahiki Meya kwa ridhaa yake. Naomba Serikali i-support tukamilishe.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Malembeka, naomba ukae kuna taarifa!
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Zahanati ya Mbondolwe, Luhanga, Lubakaya na Yongwe, ziweze kufanya kazi katika Jimbo la Ukonga. Nataka nizungumzie kuhusu; eeh!
MWENYEKITI: Mheshimiwa Malembeka, naomba ukae, kuna taarifa. Haya Mtoa taarifa
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaomba muda wangu uendelee kulindwa.
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza taarifa naikataa. Nimekuwa Diwani miaka kumi nikikaa ndani ya Jimbo la Ukonga, sikumjua. Haya ninayozungumza nina uhakikanayo, niliyapanga nikiwa Mwenyekiti wa Huduma za Jamii Manispaa ya Ilala.
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kuhusiana na vita dhidi ya rushwa na ufisadi. Napongeza kwa dhati juhudi zinazofanywa na Mheshimiwa Rais za kupasua majipu na ninaomba majipu haya yasiishie ndani ya wananchi wa huku, twende kwenye Vyama.
Hata kama mtu akibadilisha shati; akivua shati la kijani akivaa leupe, tumfuate huko huko, tukamtumbue. Kwa sababu wengine wamehama; wametoka huku wameenda upande wa pili. Tuwafuate tukawatumbue majipu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie kuhusiana na suala la vijana kwa upande wa bodaboda. Nafurahi kwamba Serikali hii imewatambua bodaboda, naomba waendelee kupewa mafunzo, waelekezwe waweze kukata Bima ya Afya, lakini pia naomba Serikali hii iandae utaratibu kuona jinsi gani ya kuagiza vifaa vya bandia kwa sababu sasa hivi tumepata walemavu wengi sana kutokana na suala la bodaboda. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niingie ukurasa wa 21 kwa ajili ya suala zima la walemavu. Naishukuru Serikali yangu Tukufu ambayo ni sikivu, imeweza kutenga mambo maalumu kwa ajili ya walemavu. Ninaomba tuendelee kuwasaidia kupata miradi na kuwapa elimu, tuwasaidie kuwapangia maeneo ya kufanya biashara zao. Lakini pia tuangalie utaratibu wa kuwapunguzia masharti ili waweze kupata mikopo nafuu na kuendesha biashara zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe masikitiko yangu; nasikitika sana kuona baadhi ya walemavu viungo vyao wanafanya kama vile mradi au kichekesho. Kile kitendo, binafsi mimi kinaniuma, kinaniudhi. Ninafahamu kabisa ulemavu siyo kushindwa, lakini bado wapo baadhi ya walemavu wanakubali kutumika kama kichekesho kwa ajili ya shughuli nyingine. Mimi hiyo tabia kwa kweli siipendi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niongelee zaidi pia kuhusiana na suala la maslahi ya Watumishi. Siku zote niseme kwamba kazi nzuri inavyoenda na kazi yoyote utamu wake fedha. Hatuwezi tukakaa kila siku tunataja section mbili tu; Walimu, Madaktari! Naomba nisemee sekta nyingine zote zilizobaki kwamba maslahi yao yaboreshwe ili waweze kufanya kazi vizuri na kwenda sambamba na kasi ya Hapa Kazi Tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka pia nizungumzie katika suala zima la…
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Malembeka, inatosha naomba ukae muda umemalizika.
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Eeeh! Muda umeisha!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda umeisha namalizia kwa kusema kwamba nyoka wa kijani haumi, siku akiuma hana dawa. Naunga mkono hoja!