Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Lucy Fidelis Owenya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyozungumza utalii unachangia sana katika pato la Taifa, lakini wafanyabiashara katika sekta hii, niungane na wenzangu kusema kwamba tozo na kodi ni nyingi sana, ziko kodi 36 na nimeziambatanisha hapa naomba uzione ili wakati Kamati ya Bajeti inakaa wakati wa Finance Bill waangalie ni jinsi gani wanaweza wakazipunguza kodi hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anasema kwamba VAT haikuathiri watalii kuja nchini. Kwa mfano kabla ya VAT Ngorongoro Crater mwaka 2014 walikuja watalii 332,163, mwaka 2016 wamekuja watalii kuingia Crater 228,689, kuna pungufu ya 103,000, sasa kama wanabisha siyo VAT, basi wafanye uchunguzi ni kitu gani kinafanya watalii hawaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuko katika sekta, watalii wengi walikataa kulipa zile VAT. Sasa wao wanasema watalii wameongezeka sijui hizi takwimu wanatoa wapi, sijui mnajumlishia na hao Wachina wanaokuja kujenga barabara huku, sielewi kwa kweli, naomba Waziri atueleze hizi takwimu anazitoa wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kodi nyingi sekta hii inakuwa vigumu sana kufanya matangazo, unakuta wafanyabiashara wana kodi nyingi lakini ni wao wao watengeneze vipeperushi, wajilipie exhibition lakini TTB haiwezeshwi. TTB mwaka 2016 waliomba shilingi bilioni 2.7 mpaka sasa hivi wamepata milioni 422, watafanyaje advertisements?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kuna masoko mapya kama Nchi za Czech, Ukraine, Yugoslavia na sehemu nyinginezo, wanataka kuja Tanzania lakini TTB ndiyo inayotakiwa iende ikatangaze vivutio vya Tanzania lakini wanashindwa, kuna vivutio vingi. Mathalani, Mkoa wa Kilimanjaro Kijiji cha Mrusunga, Kata ya Mbokomu, Moshi Vijijini, kuna mti mrefu mita 80 mti ule unakadiriwa umekaa zaidi ya miaka 500, lakini Wizara ya Utalii haijafanya utafiti wowote, wanatakiwa waende wakaweke uzio pale ili muuweke kati ya vivutio wageni wanavyokuja kutembelea Mlima Kilimanjaro, wakati wanangojea kupanda, wakati wa climatization, tuiweke kwenye itinerary Wazungu waweze kwenda pale waende wakapige picha na tunaweza kupata mapato. Wizara imekaa kimya sijui wanasubiri mzungu aje apige picha aseme ame-discover mti mrefu Afrika, wakati watafiti wako hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri hivi vitu tuvifanye wenyewe na tuwe proud na nchi yetu wenyewe, tusingojee Wazungu waje hapa watuambie wame- discover Mlima Kilimanjaro wakati sisi tuko hapa na babu zetu walikuwa wanaokota kuni kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la wakulima na hifadhi TANAPA. Mfano, kuna wakulima wanaolima mpunga kule Mbarali wakulima hao wana vijiji 32, TANAPA inataka iende ikachukue vijiji vile ifanye hifadhi, lakini wameshaendelea wamejenga viwanda zaidi ya 46 wana ma-godown karibu 56, wana wafanyakazi zaidi ya 10,000, viwanda vile walivijenga kwa zaidi ya billioni 72, tayari wameshawekeza kwenye viwanda na Serikali wanasema Tanzania ya viwanda, sasa hivi wanataka kwenda kuwanyang’anya vile viwanda, sasa wataenda wapi, watafanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Waziri nimeshazungumza naye na pia nilimwona Waziri Mkuu kuhusiana na suala hili. Naomba vile vijiji waviache waendelee na ile kazi tayari ni ajira iko pale, tayari viwanda viko pale, wawaache wafanye kazi, waende wakaendeleze hifadhi nyingine. Kuna hifadhi kama ya Selous inatakiwa kuendelezwa, Saadani inatakiwa kuendelezwa, sasa wanaenda kufukuza watu ambao tayari wana makazi, wana wafanyakazi, wana kila kitu, kwa nini wasiende huko ambako kunatakiwa kuendelezwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa nimekosea sana kama sitauongelea Mlima Kilimanjaro. Kila siku nimekuwa katika Bunge hili tangu tumeanza naongelea suala la rescue.

Rescue katika Mlima Kilimanjaro bado hairidhishi, unakuta mgonjwa anaugua kule juu, sijui ni kwa nini pamoja na mapato yote haya wanayopata kutoka Mlima Kilimanjaro wasinunue helicopter ya ku-rescue wagonjwa wanaopata matatizo kule mlimani ikiwa ni pamoja na ma-porter.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni shida mtu akipata ugonjwa kutoka Uhuru Peak mpaka ashushwe chini, akutane na gari ya National Park ile inayo-rescue unakuta ameshakufa, ni zaidi ya masaa kumi, lakini wakinunua helicopter yenye uwezo wa kuweza kushuka kule Shira wataokoa maisha ya watu na wale Wazungu wanaokuja wataona kwamba tunawajali pamoja na Porters, lakini sisi tumekuwa tukiwaleta kwa mikono, wanakufa, wanaenda kufanya uchunguzi kwa nini wamekufa lakini tatizo ni rescue system tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo nimeulizia mara nyingi kuhusu vyoo, vyoo ni tatizo katika mlima wetu mmesema watu wanaenda ku-camp crater naomba kumuuliza Mheshimwa Waziri wana-camp crater watajisaidia wapi? Mazingira tutayatunzaje? pale crater hamna choo, vile vyoo vilivyoko kwenye camping roots ni vya shimo, vimejaa, kila Tour Operator anajaribu kupeleka chemical portable toilets, lakini ile waste wanaipeleka wapi? Wanaenda kuimwaga kule kwenye yale mashimo ya National Park ya choo, lakini bado yamejaa, kwa hiyo bado yale mazingira Mlima unarudi pale pale kunazidi kuwa kuchafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo naomba sana, hili suala la choo, kuna vile vyoo vya Wajerumani mlivyovileta vya kujaribu vimeishia wapi? Maana yake mnakuja hapa mnaongea maneno mazuri lakini hamtekelezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine tunacholalamika kule Kilimanjaro ni fees za forest. Mtu analipa National park fee mfano kule Umbwe, Longai na Lemosho, unalipa forest fee unalipa na National Park fee, unaenda mpaka Umbwe unafika Umbwe hakuna maji, inabidi warudi tena chini wanunue tena maji, zote hizi ni tozo tu zinazidi sasa unakuta tunashindwa kufanya biashara kwa sababu ya hivi vitozo vidogovidogo. Kwa hiyo, naomba sana waliangalie hilo.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine pamoja na mambo mengine ni lile suala la Faru Fausta, Faru Fausta anatumia fedha nyingi sana shilingi millioni 60 kwa mwezi ni fedha nyingi. Mnyama yule alizoea kutembea huru, hivi kwa nini msimuache afe naturaly kama anavyokufa tembo, anavyokufa simba lakini anakuwa ni chakula kwa ajili ya wale wanyama wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini wanamtesa yule mnyama wanamfungia kwenye cage, ana vidonda, anateseka mnyama wa watu, kwa nini wasimuachie aende kwenye mbuga ili akafe natural death kama wanyama wengine, lakini mnamuweka pale mnampa madawa mnamtunza kuliko binadamu, at the end of the day lazima atakuja kufa tu. Kwa hiyo, wamwache afe kwa kifo chake cha kawaida, lakini siyo mumtunze pale na wakati tunahitaji fedha nyingi kwa ajili ya kutunza hifadhi zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, watu wamekuwa wakija sana Northern Circuit, nami niungane na wengine niombe sasa tuweke mkazo Southern Circuit. Southern Circuit kumekuwa ni monopoly, unakuta ni mtu mmoja amejenga hoteli kule, barabara sio nzuri sana kwa hiyo unakuta Wawekezaji wa ndani inawawia vigumu sana kwenda kuwekeza kule kama nilivyozungumza mwanzoni. Licence ni nyingi, fees ni nyingi, unakuta Local Tour Operators ni vigumu sana kwenda kuwekeza kule chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara iweke mazingira wezeshi ili Watanzania nao waweze kwenda kuwekeza kule Southern Circuit, wajenge hoteli tuweze kuuza Southern Circuit, maana yake sasa hivi ukisema unaiuza Southern Circuit huwezi, unakuta ni zaidi ya dola 6,000. Mtu anataka apande mlima, atembee aende Southern Circuit, aende aka-relax Zanzibar, inafika karibu dola 12,000 au 15,000 watu hawawezi ku-afford hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujio wa watalii sasa hivi kuna competition, wenzetu Kenya wanapeleka very cheap kwa sababu ndege zao zinawaleta wageni direct mpaka Nairobi, kwa hiyo inakuwa ni rahisi kwa wao kuweza kuuza utalii Nairobi kwa bei rahisi kuliko ilivyo Tanzania... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.