Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili nami niweze kuchangia Wizara hii ya Maliasili na Utalii. Pia napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani katika Wizara hii Mheshimiwa Ester Matiko kwa hotuba nzuri. Baada ya kusema hayo naombe niende moja kwa moja kwenye kuchangia Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Maliasili na Utalii ina mchango mkubwa sana katika maendeleo ya Taifa hili, ina mchango mkubwa katika pato la Taifa na imeweza kuchangia asilimia 17.5 kwa maana ya GDP. Pia sekta hii inachangia ajira milioni moja na laki tano(1,500,000) katika nchi hii, kwa maana ajira laki tano za moja kwa moja lakini pia ajira milioni moja ambazo si za moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Sekta ya Utalii ni sekta ambayo inaliingizia Taifa letu fedha za kigeni. Asilimia 25 ya pesa za kigeni katika Taifa hili zinatokana na Wizara ya Maliasili na Utalii. Sekta hii ya Utalii ni sekta namba mbili katika kuvutia wawekezaji. Mwaka jana 2016 Sekta hii ya Utalii imeweza kuliingizia Taifa letu dola za Kimarekani bilioni 2.1. Kwa kutambua umuhimu, fursa na mchango wa Sekta ya Utalii katika kuwezesha na kuendeleza uchumi wa nchi yetu, ni dhahiri kabisa tunahitaji Sera Wezeshi na mikakati thabiti kuweza kuendeleza na kuboresha sekta hii ya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wawekezaji na wafanyabiashara wa Sekta ya Utalii wamekuwa wakikumbwa na changamoto nyingi, naomba niongelee utitiri wa kodi, ada, leseni na tozo mbalimbali katika sekta hii. Jambo la kusikitisha tozo, ada na leseni hizi hazilipiwi kwenye mamlaka moja, zimekuwa zikilipiwa kwenye mamlaka tofauti na hivyo kuwa kikwazo na changamoto kwa wawekezaji na makampuni yanayowekeza katika sekta ya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako naomba niseme baadhi ya tozo na leseni mbalimbali na mamlaka mbalimbali zinazolipiwa gharama kwenye sekta hii. Utaambiwa uende TRA ukalipe kodi; nenda Wizara ya Maliasili na Utalii ukalipe leseni na ada; nenda Marine Park Authority ukalipe concession fee, nenda Tanzania Civil Aviation Authority ukalipe leseni ya huduma za anga na ukaguzi; nenda SUMATRA ukalipe SUMATRA vehicle sticker; nenda TANAPA ukalipe motor vehicle guide fee; nenda Ngorongoro Conservation Area ukalipe NCAA vehicle fee. Niiombe Serikali iangalie ada, tozo na leseni ambazo zina tija katika sekta ya utalii ili kupunguza changamoto na usumbufu kwa wawekezaji katika sekta hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee katazo la matumizi ya mkaa na kilio cha wananchi. Naomba nieleweke, sipingi harakati za Serikali katika kulinda misitu yetu kwa utalii endelevu. Lakini, karibu kila mtu anatumia mkaa ikiwa ni pamoja na sisi baadhi ya Wabunge. Serikali haijaja na nishati mbadala ambayo inapatikana kwa urahisi na ambayo ni affordable kwa mwananchi wa kawaida especially vijijini, ambayo inaweza kumsaidia katika matumizi ya nyumbani. Kwa hiyo, niishauri Serikali iweze kuangalia ni jinsi gani inaweza kuja na nishati mbadala ili tuweze kumwezesha mwananchi wa kawaida aweze kumudu gharama za matumizi ya kupikia na taa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna option ya gesi lakini option hii ni ghali sana. Mtungi wa kilo 15 ni shilingi 52,000, siamini mwananchi wa kawaida wa kijijini kule Serengeti ninakotoka mimi anaweza kumudu hii gharama. Pia kuna option ya makaa ya mawe, sijaona kwenye hotuba hii kwamba kuna utafiti wowote umefanyika ambao unaonesha nishati ya makaa ya mawe hayana madhara kwa matumizi ya nyumbani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali kwa maeneo ambayo ni ya wafugaji, kuna miradi imefanyika ya biogas kwa maana ya kutengeneza biogas kwa kutumia kinyesi cha ng’ombe, tuweze ku-invest katika hii area na ile miradi ambayo imefanywa na wafadhili. Kwa mfano, Serengeti kuna Kata ya Morotonga, Ring’wani kuna miradi imefanywa na wafadhili. Niiombe Wizara ya TAMISEMI kwa kushirikiana na Halmashauri zetu kuona ni jinsi gani inaweza ikachukua hii miradi na kuiendeleza na kui-scale kwenye Wilaya zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee Mkoa wa Mara ninakotoka. Mkoa wa Mara ni Mkoa ambao una makabila mengi na wenye tamaduni tofauti. Wizara ya Maliasili na Utalii haijaweza kuwekeza kwenye fursa ya utalii wa tamaduni mbalimbali zinazopatikana katika Mkoa wa Mara. Niombe Waziri uweze kuangalia pia ni jinsi gani tunaweza kuwekeza kwenye tamaduni zinazotokana na makabila mbalimbali badala ya kuangalia utalii wa wanyamapori peke yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 70 ya mbuga ya Serengeti iko Mkoa wa Mara, lakini wananchi wa Mkoa wa Mara wamekuwa wakiishi maisha ya kimaskini kama vile hii mbuga ya Serengeti haiko Mkoa wa Mara. Ni asilimia 10 tu ya watu walioajiriwa Serengeti National Park wanatoka Mkoa wa Mara. Namwomba Mheshimiwa Waziri wakati anakuja kuhitimisha hotuba yako atuambie watu wa Serengeti na watu wa Mkoa wa Mara ni sababu gani ni asilimia kumi tu ndiyo wameajiriwa katika Serengeti National Park, je, ni kwa sababu hatuna watu wenye uwezo ambao wanaweza kufanya kazi kwenye mbuga hiyo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na changamoto ya wanyama wanaotoka mbuga ya Serengeti kuvamia vijiji vilivyo pembezoni ya mbuga ya Serengeti na kufanya uharibifu wa mali za wananchi ikiwemo mashamba, pia kuwadhuru wananchi na kusababisha vifo kwa baadhi ya wananchi ikiwa ni tembo, nyumbu na wanyama wengine wanaokula mazao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kwamba kuna kifuta jasho na kifuta machozi, lakini kuna wananchi wa vijiji vinavyozunguka Wilaya ya Serengeti ikiwemo Pakinyigoti, Makundusi, Robanda ambao hawajalipwa toka mwaka 2005. Namwomba Mheshimiwa Waziri wakati anakuja kuhitimisha hoja yake atuambie compensation plan ya hawa watu ikoje na watalipwa lini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto hiyo kuna migogoro kati ya Askari wa Wanyamapori na wananchi wanaoishi pembezoni mwa mbuga ya Serengeti. Askari hao wamekuwa wakiwabambikia kesi wananchi wanaoingia kwenye hifadhi ama kwa kujua au kwa kutokujua kwa sababu hakuna mipaka inayoeleweka. Kinachonisikitisha ni kwamba wananchi hawa wamekuwa wakipelekwa Mahakama ya Bunda na siyo Serengeti wakati Mahakama ya Bunda ina uwezo sawa na Mahakama ya Serengeti. Namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja yako atuambie watu wa Serengeti ni kwa nini wanapelekwa Mahakama ya Bunda na siyo Mahakama ya Serengeti.