Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana ni vigumu sana mimi kuchangia vizuri sana kwenye hii Wizara kwa sababu kuna wakati Waziri Maghembe akiwa Waziri wa Maji nilikuwa mshauri wake, lakini kwa sababu mimi sasa hivi ni Mbunge wa Jimbo, inabidi nichangie vizuri kwa kutumia nukuu nyingi hasa za Katiba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 8(1) ya Katiba inasema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya Kidemokrasia na haki ya kijamii na kwa hiyo (a) wananchi ndiyo msingi wa mamlaka yote na Serikali itapata madaraka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba; (b) Lengo kuu la Serikali litakuwa ustawi wa wananchi; (c) Serikali itawajibika kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 9 kuhusu mamlaka ya nchi na vyombo vyake vyote vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote katika lengo la kuhakikisha kuwa; (i) kwamba matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi na hasa zaidi yanaelekezwa kwenye jitihada za kuondosha umaskini, ujinga na maradhi.
Sasa kwenye wajibu wa kulinda maliasili, Ibara ya 27(1) kila mtu anawajibu wa kulinda Maliasilia ya Jamhuri ya Muungano, mali ya Mamlaka ya Nchi, na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi na pia kuheshimu mali ya mtu mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ndogo ya (2) watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali za mamlaka ya nchi ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu na kuendesha uchumi wa Taifa kwa umakini, kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya Taifa lao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika haki ya kufanya kazi, Ibara ya 24(1) bila kuathiri masharti ya sheria za nchi, zinazohusika kila mtu anayo haki ya kumiliki mali na haki ya hifadhi kwa mali yake aliyonayo kwa mujibu wa sheria. Sasa hapa kidogo nita-pause.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale watu ambao wananyang’nywa mali zao, mifugo, hasa ng’ombe bila fidia, hiyo inavunja Katiba, na wakati mwingine wanapigwa faini za mamilioni kwa risiti fake, hiyo ni kuvunja sheria za nchi na kuvunja Katiba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na wakati mwingine katika risiti zile ambazo zingine mimi ninazo Mheshimiwa Profesa akizitaka mimi nitampatia, risiti imeandikwa hii umepigwa faini kwa ajili ya posho za viongozi, sasa kama posho ile huwa inakuja mpaka kwa Waziri mimi sijui, lakini risiti ninayo na imeandikwa faini hii umepigwa kwa ajili ya posho za viongozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye Ibara 24(2) bila kuathiri masharti ya Ibara ndogo ya (1) ni marufuku kwa mtu yeyote kunyang’anywa mali yake, kwa madhumuni ya kutaifisha au madhumuni mengineyo bila idhini ya sheria ambayo imeweka masharti ya fidia inayostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba, hii ambayo mimi ninainukuu hapa ambayo ndiyo Katiba yetu inakataza kutumia sheria ambazo zinanyang’anya mali ya wananchi bila fidia. Kwa hiyo mimi naomba sana tujitathimini kama Taifa, kama hatua zile kama zinaelekezwa na sheria hizo, basi sheria hiyo ni mbovu, na inatakiwa iletwe hapa tuirekebishe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie masuala yanayohusu Jimbo langu la Sikonge. Jimbo la Sikonge au Wilaya ya Sikonge kwa asili yake hiyo Wilaya siyo ya wafugaji, lakini leo wafugaji wamekuja wengi sana kwa sababu ya makosa ya Serikali. Kosa la kwanza la Serikali, mwaka 1959 baada ya kuonekana kwamba kuna uharibifu wa mazingira katika maeneo ya wafugaji yaliyo mengi, Gavana alitoa order kwamba mifugo ipunguzwe hadi chini ya 100 kwa kila mfugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini order ile ilichelewa kutekelezwa mpaka tukapata uhuru, tulivyopata uhuru Mwalimu Nyerere akawatetea wafugaji kwamba hii mifugo sio mingi ukilinganisha na ukubwa wa nchi. Nchi bado tunayo kubwa sana, kwa hiyo, hawa wafugaji kama wanaharibu mazingira huko wanaweza wakasambazwa katika maeneo mengine ya nchi na wakapata huduma yao bila tatizo lolote la uharibifu wa mazingira. Na ndio maana Sikonge kukawa na wafugaji leo wengi na maeneo mengine wamekwenda mpaka Lindi kwa sababu ya order ya Mwalimu Nyerere ya mwaka 1961.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Mwalimu Nyerere aliwatetea, kwa nini sisi tumeweka sheria ambazo zinawanyanyasa? Kwa nini tumeweka Sheria ambazo zinakuja kuwabugudhi Watanzania hawa ambao walitetewa na Mwalimu Nyerere. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kosa la pili la Serikali; mwaka 1968 – 1974 operation vijiji kule Sikonge vijiji vya zamani vilivyokuwepo wakati wanapima maeneo ya hifadhi, vilikuwa mbali na maeneo ya hifadhi, wakati wa vijiji vya ujamaa, vijiji vya ujamaa vikapelekwa mita 100 kutoka kwenye hifadhi, unategemea nini kama umemuweka mwananchi mita 100 kutoka kwenye hifadhi, lazima ataingia kwenye hifadhi, kule kwenye hifadhi kuna miti, asali, nta, na mazao mengine ya misitu, ataingia tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima kuwa na utaratibu ambao unalinda maslahi ya wananchi kwa sababu Serikali yenyewe ndiyo imechangia kufanya makosa mengi, nataja maeneo kama Ngoywa, Kipili, Kilumbi, Kiloleli, Usunga, Igigwa, Nyahwa, Mole, Ipole, Chabutwa, Kisanga, kata kumi kati ya kata 20 zote ziko karibu na hifadhi au ziko ndani ya hifadhi, viijiji 29 kati ya vijiji 71 vya Wilaya vyote viko karibu na hifadhi au ndani ya hifadhi. Sasa unategemea nini na Serikali yenyewe ndiyo imewapeleka karibu na hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanafaya uchaguzi, wana shule, umeme, kila huduma imepelekwa kule, leo hii unakuja unaweka beacon unasema hili ni eneo la hifadhi mhame. Karibu nusu ya watu wa Sikonge utawapeleka wapi, na ndiyo maana hoja ya Mheshimiwa Nape ya kusema Serikali iteue Kamati Maalum na kwa Sikonge iwe case study ninawaomba mje Sikonge mkae na DC, sisi tuna DC mzuri sana, kwanza hata kama mtakaa naye tu mimi sipo, mimi naunga mkono kila mtakachofanya kwa sababu yule DC yuko makini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka nisisitize maeneo haya ya hifadhi yalipimwa mwaka 1954 na maeneo mengi upimaji ulikamilika mwaka 1956 wakati wanapima watu katika Wilaya ya Sikonge ya sasa watu walikuwa 16,000 leo hii kwa projection kwa kutumia formula ya NBS watu wanakaribia 300,000 katika Wilaya ya Sikonge. Sasa watu 16,000 wakati unapima, leo watu 300,000 eneo lako bado lilelile bado unadai kwamba watu waendelee kuishi kwenye eneo lile lile lenye ukubwa ule ule. Eneo la Wilaya ya Sikonge, kilometa za mraba 27,873 eneo ambalo watu wanaruhusiwa kuisha kisheria ni kilometa za mraba 1,049 asilimia 3.7; waende wapi hawa watu 300,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana Kamati hiyo ije Sikonge tukae nayo na tuwaelekeze maeneo mengine ambayo yamekosa sifa za kuendelea kuwa hifadhi na mapori ya akiba yaondolewe kwenye utaratibu ili wananchi wapate kujitanua. Ng’ombe wakati wanapima walikuwa 2,500 leo tuna ng’ombe karibu 200,000 sasa tufanye nini katika hilo na kwa nini wananchi wamekuwa wanadhalilishwa na wanaonewa kwa sababu ya makosa ya Serikali kama nilivyoainisha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mwisho kabisa naomba sana njooni Sikonge, tukae kwa pamoja, sisi wote lengo letu moja, tunataka tulinde maliasili zetu, tunataka tulinde mazingira yetu na wananchi wako tayari, isipokuwa tu ramani zile zipimwe upya na wananchi tutaelimishana namna ya kulinda mazingira namna ya kulinda hifadhi zetu, zile ambazo zitakuwa zimepunguzwa ili kusudi kila mtu aweze kupata...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)