Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi ya kuchangia. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha siku hii ya leo kukutana katika Bunge hili Tukufu kujadili mambo muhimu kwa maslahi ya Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kupongeza jitihada za Rais wetu wa awamu ya tano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli za kuboresha maisha ya Watanzania, lakini za kupambana na rushwa, kujenga nidhamu na uwajibikaji kwa wananchi na watumishi wa umma. (Makofi)
Aidha, kwa muktadha huo ninaishauri Serikali iimarishe Taasisi ya Kupambana na Rushwa ili iweze kufanya majukumu yake vizuri na kwa weledi. Sanjari na hilo, Serikali iweze kuimarisha Taasisi za Kutoa na Kusimamia haki ili kulinda haki za Watanzania wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kipekee nimpongeze Waziri Mkuu kwa kasi yake katika usimamizi wa Serikali, lakini pia kwa ziara yake aliyoifanya Mkoani Kigoma. Hakika ziara yake imeacha manufaa makubwa sana na hasa katika ulinzi na usalama wa Taifa letu hili. Pia imewaacha Watanzania na wananchi wa Mkoa wa Kigoma wakiwa na ari na imani kubwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi; Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujielekeza katika ukurasa wa 46 wa hotuba ya Waziri Mkuu ambayo inazungumzia nishati. Ni dhahiri kwamba katika maendeleo ya viwanda nchini, haitowezekana maendeleo hayo kufanikiwa pasipokuwa na nishati ya umeme na umeme wa kutosha na wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, nangependa kuchukua fursa hii kupongeza jitihada za Serikali za kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme kutoka Megawatts 1226.24 katika mwaka 2015 mpaka Megawatts 1,516.24 kwa Januari, 2016, ambalo ni ongezeko la asilimia 24 na ambalo limetokana na maamuzi sahihi ya Serikali ya kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la gesi. Pamoja na mradi wa kufua umeme wa Kinyeresi I ambao unazalisha Megawatts 150. Aidha, napenda kuunga mkono ujenzi wa Kinyerezi II ambayo itazalisha Megawatts 240.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani kabisa lile lengo la Serikali la kipindi cha miaka mitano la kuhakikisha kwamba kuna uzalishaji wa umeme wa kufikia kiwango cha Megawatts 4,915 linafikiwa pasipo na shaka. Nami nina imani kabisa kwamba itakapofika mwaka 2020 asilimia 60 ya Watanzania wataweza kupata nishati hii muhimu ya umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani mafanikio makubwa sana ya mikakati hii ya kuzalisha umeme utafaidisha sana vijana. Utawafaidisha kwa sababu utaweza kukuza uchumi na tutaingia katika uchumi wa viwanda. Uchumi wa viwanda utaweza kuleta ajira kwa vijana, kwa maana wataweza kuajiriwa katika viwanda, lakini wao wenyewe wataweza kutumia nishati hii ya umeme kuanzisha viwanda vidogo. Kwa mfano, kuanzisha mashine za kukoboa, viwanda vidogo vya kukamua juisi, kukamua mafuta ya alizeti, ufyatuzi wa matofali kwa kutumia mashine za umeme. Kwa hakika mipango hii madhubuti sisi kama vijana tunaiunga mkono kwa sababu inatunufaisha sisi vijana moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kupongeza jitihada za kipekee za Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa Profesa Muhongo, za kupunguza bei ya umeme. Punguzo la umeme linapelekea punguzo katika gharama za uzalishaji na gharama za uzalishaji zinapopungua, zinaleta upatikanaji wa faida; na faida inayopatikana inaweza kukuza uchumi zaidi, lakini kurahisisha na kuhakikisha kwamba ajira za vijana zinaendelea kuwepo, kwa sababu biashara hazitakufa, viwanda vitaendelea kuwepo, lakini na wao wenyewe vijana kwa faida wanazopata katika biashara zao, wataweza kunufaika na kukuza zaidi uchumi wa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo naomba sana jitihada hizi za Serikali ziendelee na Serikali itambue kwamba sisi vijana tunathamini na kuunga mkono jitihada hizi, maana sisi ni wanufaikaji wa kwanza kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza sana jitihada za Serikali kupanua mradi wa REA awamu ya pili, kufikia katika vijiji 1,669 katika kipindi kifupi cha mwaka mmoja 2015/2016. Vijana wa Mkoa wa Kigoma Wilaya Kakonko, Buhigwe na Uvinza wananufaika sana na jitihada hizi kwa sababu wamesogezewa nishati ya umeme; na hivyo wao wenyewe wanaweza kufanya shughuli mbalimbali za kijasiriamali, ambazo zinahitaji nishati hii muhimu ya umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kupongeza jitihada ya Serikali katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya kuanzisha Mfuko wa Shilingi milioni 50 kwa kila Mtaa na kila Kijiji. Napenda kuishauri Serikali kwamba iweke maandalizi mazuri na nafahamu kuna jitihada zinazofanywa na Serikali kuandaa maandalizi mazuri ya Mfuko huu. Napenda kuishauri zaidi Serikali, iboreshe na kuimarisha Mfuko wa Maendeleo wa Vijana (Youth Development Fund). Katika Mfuko huu, tumeona vijana wengi wameweza kufaidika kwa kupata mitaji ya kuendesha shughuli zao za kijasiriamali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kumejitokeza changamoto mbalimbali, hivyo napenda sana Serikali ichukue mfano au itumie uzoefu na changamoto ilizopata katika kuendesha na kusimamia Mfuko huu wa Youth Development Fund ili iweze kutengeneza mfumo bora zaidi utakaosimamia Mfuko huo wa shilingi milioni 50 kwa kila Kijiji na kila Mtaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kupongeza mipango endelevu ya kukuza uchumi wa viwanda, lakini inabidi tufahamu kwamba katika mipango hii endelevu ya kukuza uchumi wa viwanda, ni lazima mipango hii iende sambamba na uzalishaji wa nguvu kazi yenye weledi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kutoa elimu ya bure kuanzia shule ya msingi mpaka sekondari. Imani yangu ni kwamba tunapoelekea katika uchumi wa viwanda, inabidi tufanye jitihada zinazoonekana za kuandaa nguvukazi kwa kuwapatia wanafunzi wetu elimu ya kutosha na yenye ubora wa kuwaandaa kupokea na kukabiliana na changamoto na uchumi wa kati na ushindani wa ajira, biashara na taaluma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatutegemei hapo haadaye tutakapokuwa na uchumi wa viwanda vijana au ajira ziende kwa watu wa nje. Tunategemea sana kwamba uchumi wa Viwanda utawanufaisha vijana wetu wa ndani ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.