Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Simanjiro
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nimshukuru saana Mungu kwa kunipa nafasi hii leo lakini niendelee kuwashukuru watu wa Simanjiro kwa kuniamini kuwa Mbunge wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kwenye Wizara hii na kuanza na maneno haya tu, kwamba ni lazima Wizara hii itambue pamoja na maslahi mapana ya nchi ni muhimu kutambua pia kwamba wale waliosaidia sekta hii ya kiuchumi ya maliasili kutunzwa mazingira yake na wenyewe waheshimiwe; maana imekuwa na fikra kubwa sana kwamba wale ambao wanaishi pale, maslahi yao sio mapana sana na sio makubwa kwa Taifa ukilinganisha na Taifa kubwa. Kwa hiyo, hilo Mheshimiwa Waziri naomba uliangalie sana kwasababu mimi ni mfugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niungane na Wabunge wenzangu, mipaka hii kuanzia mwaka 1954 mpaka leo haijaangaliwa tena, jamii imeongezeka na mimi niko kwenye msimamo mmoja kwamba haiwezekani tufike mahali kwamba kesho tukiwa bilioni moja kama Wachina tuseme na mbuga zetu ziliwe, haiwezekani! Ni lazima tukubaliane.Lakini wakati mipaka hii ikiandaliwa watu wetu walikuwa hawajui kinachotokea, hawajui thamani ya ardhi, hawajui nini maana ya mipaka hii na wanyama hawa. Ni muhimu sana Mheshimiwa Waziri na zile Wizara ambazo zimeungana Wizara tano, mifugo, kilimo tuje na wawakilishi (wote sisi wawakilishi) tukae pamoja tuweke mipaka ya kudumu na tuwafundishe wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Simanjiro vijiji vya Kimotoro, kijiji cha Lobosiret, Emboret na baadhi ya maeneo ambayo mbuga hizi zimezunguka nipo tayari kuwaongoza wananchi wangu tutakapokubaliana na Serikali kwamba mipaka hii sasa huu ndiyo uwe mwisho, kwa maisha ya sasa na maisha ya baadae ya watoto wetu. Ni muhimu sana tukae wadau wote tukubaliane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba nitambue kimsingi kazi kubwa iliyofanyika Ngorongoro, Loliondo. Nimeona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri lakini bahati mbaya nimeona pia kwenye Kambi yetu Rasmi ya Upinzani. Wananchi wamekaa na watumishi wa Serikali, wamekubaliana njia ya kwenda mbele ili kumaliza migogoro. Mheshimiwa Waziri ninaona hutaki kutambua nguvu hii. Mimi nafikiri ni vyema sana wanyamapori na Wizara yako ikae na wananchi tukubaliane wote kwamba kuanzia sasa na maisha ya baadae tunakaaje ili kuhifadhi wanyama hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mtalii, nikuambie tu ukweli, mimi nazunguka sana lakini namshukuru Mheshimiwa Nape na yeye siku moja nimeenda mbuga moja nikasikia na yeye yupo kwenye hoteli mojawapo. Ni lazima sisi kama Bunge, hii Wizara tuibebe, kazi kubwa tuifanye. Viongozi hamtalii, hamuendi mahali, lakini ni vyema sana Wizara hii iwepo Ngorongoro Conservation Area Authority, iwepo TANAPA kwa ujumla wake, kina KINAPA wote, mfanye juhudi za kipekee za kusaidia Watanzania watalii na viongozi wa nchi hii muanze kutalii kwenye mbuga zetu ili tupate mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nitambue leo Simanjiro, kijiji cha Kimotoro pamoja na kupoteza maisha ya mfugaji mmoja, kuuawa na wanyama, anafidiwa kijana wetu mmoja leo kwa mara ya kwanza tangu dunia iumbwe. Mimi naendelea kusema fidia hii haitoshi, lakini leo anafidiwa mmoja. Naomba Wizara muangalie uhalali wa binadamu, heshima ya binadamu vis a vis mnyamapori. Haiwezekani anapouawa, shilingi milioni moja tu! Badilisheni sheria hizi, tubadilishe ili tuheshimu ubinadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kubwa kwenye Wizara hii, leo mimi sitaongea sana against you,kubwa na imeandikwa kwenye Biblia na Qurani amri kubwa kushinda yote ni upendo. Ninyi wahifadhi kaeni na sisi, nami nitambue kazi kubwa ya Tarangire iliyofanya pale Kimotoro wakati mnapitapita pale Kimotoro tumeweka mahusiano mazuri, Mhifadhi na Afisa Uhusiano wa Tarangire ninaomba nitambue kwamba tumeanza kukubaliana vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niongelee Makumbusho ya Taifa. Bahati nzuri nimesoma mwaka 2006/ 2007 Misri, nimetembelea makumbusho yao. Watu hawa wanaingiza watalii wengi sana kwa Makumbusho ile ya Cairo. Lakini Ujerumani wanaongoza pia kwa ajili ya makumbusho.
Ukiangalia hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuanzia ukurasa wa 12 mpaka 51 inaongelea wanyamapori, ukiangalia ukurasa wa 53 mpaka 89 kurasa 36 na 39 inaongelea nyuki. Lakini Makumbusho yetu ya Taifa mnaongelea kwa kurasa saba tu, hamuipi uzito utamaduni wetu wa nchi yetu. Makumbusho ya Dar es Salaam hayana maana kubwa ukilinganisha na makumbusho mengine yanayotuzunguka kwenye nchi yetu. Ninaomba Mheshimiwa Waziri, weka nguvu kubwa kwenye makumbusho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Misri pale bajeti ya 2017/2018 wanapitisha almost one billion USD wamepata msaada kutoka JINCA wanaboresha makumbusho yao. Mwalimu Nyerere na ninyi bahati nzuri wazee kama ninyi mmeishi na Mwalimu Nyerere sisi wengine tunamuona kwenye makumbusho tu. Kwa nini hampendi kuutunza utamaduni wetu, alianzisha Makumbusho ya Taifa letu. Ninaomba kwa nguvu zote, bajeti ya Makumbusho iongezwe. Ninaombeni tuwape Watanzania heshima hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili kuna suala la utozaji, lakini Mabalozi wetu nimeshuhudia nchini Canada, Balozi wa Kenya anaenda kwenye shule za sekondari na vyuo vikuu vya nchini Canada anawaita watalii wakati wa low season wanafunzi anatangaza utalii, imefika wakati sasa nchi yetu tunapomteua Balozi wetu pamoja na hadidu za rejea za kumpa moja ni kutangaza nchi na kutangaza nchi yetu kwenye mataifa ambayo wanaenda. Haiwezekani Mabalozi wakakaa kule maofisini na ofisi kubwa na wanapewa kila kitu, lakini hawatangazi nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu hatupati watalii wa kutosha Zanzibar is just amazing, ukiangalia Ngorongoro ni nzuri, ukiangalia Mlima Kilimanjaro, hamna mlima kama huo duniani. Lakini hatutangazi vizuri, mabalozi wetu ni vizuri Serikali iweke hadidu za rejea za kusaidia utangazaji wa utalii katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika zangu mbili naomba nimpe Mheshimiwa Ester.