Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona jioni hii, nami nitumie fursa hii kumpongeza tena Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Magufuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nimpongeze kipekee Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa uwasilishaji wake mzuri wa hotuba iliyogusa maeneo mengi ambayo kwa nchi hii tunahitaji viongozi kama hawa ambao walithubutu kutumbua jipu ambalo lilikaa muda mrefu la watu ku-bypass bomba la kushusha mafuta bandarini, lakini kuzima mita kupima kiwango cha mafuta kinachoingia nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imegusa maeneo yote muhimu ikiwemo elimu, afya, maji, miundombinu na maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza kipekee Waheshimiwa Mawaziri wanaomsaidia Mheshimiwa Waziri Mkuu; Mheshimiwa Jenista Mhagama na Mheshimiwa Abdallah Possi. Ni watu ambao wamekuwa na ushirikiano mkubwa, mimi niko katika Kamati ambayo ipo chini ya Wizara yake; Kamati ya UKIMWI na Masuala ya Madawa ya Kulevya. Wamekuwa karibu sana nasi pale tulipowahitaji na wamekuwa wakitushauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze sasa kuchangia kwa kuomba mambo machache yaweze kufanyiwa jitihada za makusudi. Suala zima la ajira kwa vijana wetu, lakini na akinamama ambao nchi hii ndiyo inawategemea sana katika suala zima la kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema sasa tukaelekeza mawazo yetu katika kubadilisha kilimo hiki cha kutegemea mvua; tukatoka hapo tukaanzisha kilimo cha umwagiliaji; kilimo ambacho kama kitatiliwa mkazo, nchi hii tutatoka kule ambako tuko na tutakwenda kule ambako tunatolea mifano nchi za wenzetu; Malaysia, Vietnam na nchi nyingine ambazo tulikuwa nazo level sawa ya uchumi. Lazima tuthubutu kidogo, tuwekeze katika kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu kuna bwawa la Itagata, zuri tu, Serikali imewekeza pesa za kutosha, lakini lile bwawa linavuja. Naomba sasa ifanyike juhudi za makusudi liweze kuzibwa ili wananchi; vijana wa pale wapate ajira, wajiajiri wenyewe kwa kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kuajiri vijana wengi, ni lazima pia tufungue miundombinu ya barabara; waweze kujiajiri kwa kununua mazao na kuuza. Pia katika maeneo mengi ni wakulima wazuri, waweze kutoka na kufika haraka katika masoko ambayo yako katika maeneo ya miji likiwemo Soko la Kimataifa la Kibaigwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna hili suala la elimu bure. Naipongeza sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya chama changu, Chama cha Mapinduzi kwa kuliona hili. Kuna changamoto kadhaa ambazo naamini zikifanyiwa kazi zitakwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika milioni 50 kwa kila kijiji. Kabla ya hizi shilingi milioni 50, kulikuwa na mabilioni ya Mheshimiwa Kikwete katika Serikali iliyopita. Kulikuwa na changamoto kadhaa. Sasa tujifunze kutokana na changamoto zile! Mabilioni yale hayakufika katika vijiji vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mmojawapo katika Jimbo langu, watu wangu hawakupata kukopeshwa hata kikundi kimoja. Kwa bahati nzuri hili linalenga vijiji na mitaa yetu. Kwa maana sasa utengenezwe utaratibu mzuri wa namna gani na watu gani watakopeshwa na urejeshaji utakuwa katika utaratibu gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikishauri mara nyingi vijana wangu wa maeneo yetu kwamba mabenki siyo rafiki sana hasa kwa vikundi vya vijana kwa sababu riba, mara nyingi ndiyo inakuwa faida ya wale ambao ni wajasiriamali. Kwa hili, naipongeza sana Serikali lakini iangalie tu changamoto ambazo zitajitokeza ili lisijekuwa gumu kama lile ambalo limepita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala hilo hilo la ajira kwa vijana, napenda sana nizungumzie suala la mbolea. Tumekuwa tukizungumzia ruzuku ya vocha za mbolea katika baadhi ya maeneo. Napendekeza kwamba, ni vizuri sasa tukabadilisha mtazamo, badala ya kutoa vocha ya mbolea, sasa Serikali iwekeze moja kwa moja katika mbolea yoyote ambayo itauzwa nchini iwe imepewa ruzuku. Tutaondoka mahali hapa pa kuweza kusukumana; huyu kaiba, hapa halikutekelezwa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi nzima ikauza mbolea ya ruzuku, itaondoa gharama hizi za kusafirisha mbolea kwa Sh. 3,000/= kutoka Dar es Salaam mpaka Tabora. Itaondoa msukumano ambao upo, watu badala ya kufanya kazi nyingine, tunafutilia nani alipewa vocha na hakuifikisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfuko wa mbolea wa kilo 50 au 25, ni sawasawa na mfuko wa cement. Mfuko wa cement kuutoa Dar es Salaam mpaka Tabora, unapita pale kwangu Itigi, unapelekwa kwa Sh. 500/= tu, lakini ulizia mfuko wa mbolea, utafikiri umebeba tani; mifuko sita ya cement inasafirishwa sawa na mfuko mmoja wa mbolea kwenda katika mikoa yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inatokana na udhaifu wa sera. Naomba tubadilishe, hakuna haja ya kuweka vocha, mbolea yote iwekewe ruzuku, ndiyo mahali ambapo Serikali itawekeza, kila mkulima anayetaka kununua mbolea, akute bei iko pale. Tutaondoka katika hili wazo la kuanza kusukumana na kutafuta nani kala na nani kafanya nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala zima la ulinzi na usalama, Jimbo langu ni Jimbo ambalo lina jiografia ngumu kidogo. Kutoka Makao Makuu ya Jimbo mpaka mwisho pale Rungwa kuna kilomita 190 karibu 200, Kituo cha Polisi kipo Itigi, hakina gari. Naomba sasa, Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo ina Serikali, Mawaziri wake wasikie, watuletee gari mpya. Mara nyingi wamekuwa wakiwapa vijana wale magari makuukuu. Njia ni mbaya, barabara mbaya, gari bovu; huwezi kufika mahali popote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali yangu hii ni sikivu, naamini wamesikia. Vile vile kuna jambo dogo tu la usikivu wa redio ya Taifa katika maeneo ambapo mimi natoka. TBC haisikiki katika masafa ya FM. Kuna redio ambayo imeweka busta yake pale; Redio Mwangaza, ni redio ambayo inasikika vizuri sana. Sasa wakati mwingine mtu anahitaji kusikia habari kama hizi za Bunge.
Pale kwangu hawasikilizi, labda itokee mtu ana runinga kwa ule muda ambao umeamuliwa. Naomba sasa Serikali ilifanyie kazi hili la masafa ya Redio ya Taifa. Hizi nyingine tutaachia wawekezaji wenyewe, wataangalia namna gani ambayo watatusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana Mawaziri wote wa Serikali hii ya Ma-Doctor na Maprofesa ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri wanayofanya, inapelekea hata rafiki zetu, watani zetu sasa wanafika mahali wanakuwa hawana cha kusema, wananyamaza tu na matokeo yake sasa tunawasemea sisi kuwaombea katika Majimbo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja.