Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Abdallah Majurah Bulembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi wanazozifanya, kazi ni kubwa, Wizara ni kubwa na ina mambo mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu umenipa dakika tano nitaongelea maeneo mawili. Suala la kwanza nitaongelea eneo la wawindaji na kwenye eneo la uwindaji kwenye vitalu miaka minne iliyopita tulikuwa tunaweza kukusanya kama dola milioni 20, jana wakati tunaangalia tuko kwenye dola 4,000,000 hapa kuna tatizo. Suala langu naliomba Wizara ya Mheshimiwa Profesa Maghembe hebu kaa na watendaji wako wakuambie ukweli, maana yake wewe ni Waziri, wao ndiyo wanatenda, bahati mbaya hawa watendaji siku zote huwa wapo tu, mambo yakichachamaa ninyi wakubwa ndiyo mnaangaliwa, hebu ingia mwenyewe ndani huku ujue tatizo liko wapi ili uweze kupata ufumbuzi angalau vitalu hivi visiwe tena kama mapambo. Vitalu vipo vinatakiwa vilipiwe viingize hela kwenye nchi, watu wakiingia leo, kesho wanarudisha wanaondoka lazima kuna tatizo hapa ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisemi tatizo ni ninyi Mawaziri au Katibu Mkuu, lakini kuna watendaji wa chini wanaoshughulika na eneo hili wakae na ninyi chini wawape maelezo ya kutosha ili Bunge lijalo angalau tuweze kuwa na kitu kizuri cha kuongelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu yangu ya pili ni utalii. Utalii katika nchi yetu ni shida, tunapata watalii milioni 1.2 nchi kama Tanzania yenye vivutio kila eneo, kwa nini Wizara hii haiwezi kuwekeza moja kwa moja kwenye Balozi zetu zilizoko nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda nje ukaangalia Balozi za Kenya utakuta kuna dawati la utalii na kwa sababu hawa wana ndege wanatafuta watalii unalipia risiti hata miezi sita, watu wanajaa kwenda kule. Kwa nini sisi kwenye eneo la utalii tunaweka pesa kidogo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kitabu cha Waziri bajeti kwenye utalii tumeweka bilioni mbili, wenzetu wa Kenya wameweka bilioni nane kwa nini? Ukienda pale TANAPA, Ngorongoro yale maeneo ni kwa ajili ya watalii. Kama tunaweza kukusanya bilioni 200, tunashindwaje kutoa hata asilimia kumi ya makusanyo yetu kwa ajili ya utalii? Kwa ajili ya matangazo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo Balozi nyingi, kwa nini Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje isione suala la utalii ni eneo lake? Kila Balozi ikapewa amri na masharti kwamba utaitangaza Serengeti, utatangaza Ruaha, utatangaza Ngorongoro, tukienda kwenye Balozi zetu watu hawana habari. Mwingine amepelekwa kwenye Ubalozi kama mchumi, lakini hawezi kuongelea utalii anaona siyo eneo lake, lakini ni Mtanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa nini Wizara hii, Mheshimiwa Waziri, usiombe kwa wenzenu kwenye Cabinet, kama makusanyo ya TANAPA ni shilingi bilioni 200 chukua asilimia 10, kama Ngorongoro 150 chukua asilimia 10, yale maeneo yote. Tukipata 50 billion shillings kwa ajili ya kwenda kutangaza watu watajaa, maana mtaji wetu ni watalii. Utakuta kwenye utalii tunaweka gharama nyingi, mambo mengi. Je, huyu ng’ombe anakamuliwaje kama hawezi kupewa chakula? Chakula nenda China kuna watu wangapi? Nani anatangaza utalii? Nenda Urusi, nenda Amerika, lakini Balozi zetu ajenda hii siyo yao! Wizarani watu wa utalii au TANAPA au Ngorongoro ukiwauliza nini wanafanya, hata matangazo, tukipita njiani pale tunaona Tigo, tunaona Vodacom, tunaona nani, ninyi mnatangaza wapi, utalii wa ndani? Vipindi mnatoa wapi? Watu hawajui! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima Serikali iwape hela mkafanye matangazo. Kuna CNN, kuna BBC, kuna maeneo mengi hujawahi kuiona Serengeti. Mheshimiwa Hasunga amesema pale, mnaitangaza timu ya Serengeti, hata kuwapa jezi ambazo zimechorwa maana ya Serengeti ni nini, hamuwezi! Sasa huko mnakotangaza ni wapi au Mawaziri muingine ndani muangalie hizi hela zinazotangazwa zinatangaza kweli?

Mheshimiwa Mwenyekiti, timu ya Taifa ya Wanawake imekwenda Uganda pale, hata ku-brand tu kuiweka Serengeti ile gari peke yake moja, haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hatuwezi kuwekeza kwenye utalii tutalaumiana kila siku kwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya bosi wangu.