Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Eng. Atashasta Justus Nditiye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii adhimu kabisa. Mimi nitaongelea masuala matatu, suala la kwanza nitaanza na suala la Hifadhi yetu ya Taifa ya Ngorongoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kwamba tunawashukuru sana wananchi ambao wanaishi maeneo ya Ngorongoro kwa kutulindia Hifadhi yetu ya Ngorongoro ambayo ni alama ya Kimataifa, kwa maana ya urithi wa Kimataifa. Ni wazi kwamba sasa Sheria Namba 284 iliyoanzisha Ngorongoro imepitwa na wakati. Sheria ile wakati inaanzishwa mwaka 1959 ilihusu kuwahudumia wakazi 8,000 waliokuwa wanaishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, lakini kwa sasa hivi tunavyozungumza watu wanaoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro wamezidi 87,000. Ni wazi kwamba Ngorongoro Conservation Area hawawezi tena kuwahudumia wananchi wanaoishi mle na matokeo yake tunashuhudia migogoro ya kila siku kati ya wananchi wanaoishi eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba sana Serikali, Mheshimiwa Waziri ulete Sheria ya Hifadhi ya Ngorongoro tuihuishe, ili iende na wakati. Ngorongoro hawana uwezo tena wa kuwanunulia chakula wananchi wanaoishi mle, hawana uwezo tena wa kuendelea kuwahudumia huduma
za afya, zaidi ni migogoro ya kila siku tunayoishuhudia na kuiona kila wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Ngorongoro licha ya kwamba inahudumiwa kwa maana ya wananchi kwa sheria iliyopo, lakini kuna Baraza la Wafugaji. Juzi wakati tunatembelea Ngorongoro na Loliondo, Baraza lilikuja na ajenda kwamba, hela wanayopewa haitoshi. Kusema ule ukweli Wajumbe wa Kamati wengi walishangaa kwamba kuna Baraza tu la Wafugaji ambalo linapewa 2.7 billion shillings kuhudumia wananchi wa Ngorongoro ambao ni Wilaya inayojitegemea ambayo Serikali inapeleka pesa kwa ajili ya kuwahudumia. (Makofi)

Kwa hiyo, ndiyo umuhimu wa kuitaka Wizara ilete Sheria ya Ngorongoro tuiangalie upya, tuifanyie marekebisho kwa kuwa mmeshindwa kuwahudumia wananchi wanaoishi mle ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la hifadhi zetu, TANAPA. Kwa upande wangu naona kwamba, kazi zinazofanywa na TANAPA na kazi zinazofanywa na Ngorongoro, ukiondoa lile suala la uhifadhi mseto, zinafanana. Vilevile kuna ile Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA). Kazi zinazofanywa na TAWA, TANAPA na Ngorongoro zote zinafanana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Wizara iangalie namna ya kuzijumlisha hizi taasisi zote tatu kiwe kitu kimoja kikubwa kiweze kuwa manageable kirahisi kuliko migogoro ambayo tunaishuhudia kila siku katika taasisi hizo. Wakati fulani nimewahi kwenda kule Pori la Moyowosi, katika hali ya kawaida wale watu walikuwa hawajui majukumu yao na majukumu ya TANAPA ni yapi na majukumu ya TFS ni yapi. Ukimuuliza suala hili huyu, anakwambia hili ni suala la TFS, ukimuuliza huyu anakwambia hili la TAWA, ukiwauliza hawa wanasema kama TANAPA wangekuwepo hapa, hili lingekuwa limepatiwa ufumbuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni yangu ni kwamba Mheshimiwa Waziri, angalia namna ya kuunganisha hizi taasisi tatu ambazo zote zinafanya kazi ya aina moja kwa lengo moja, ziwe kitu kimoja ambacho kitakuwa na bodi moja na tutakuwa tumemsaidia Rais katika kupunguza hata baadhi ya matumizi yasiyokuwa ya lazima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nitaongelea kidogo hii migogoro ya mifugo na hifadhi zetu. Hakuna asiyekubaliana kati ya Wabunge kwamba, umuhimu wa kuhifadhi hifadhi zetu ni mkubwa sana. Kila Mbunge ninaamini anakubaliana kwamba lazima hifadhi zetu zihifadhiwe, tumezikuta kutoka kwa babu zetu ni vizuri tukubaliane kwamba tunaziacha kwa wajukuu zetu wazione na waziendeleze, nina mashaka na seriousness ya Wizara.
Serikali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono.