Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hotuba iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Wizara kufanya kazi kubwa Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri na Watendaji wake, kwa sababu ya muda nijielekeze tu kwenye eneo la Wilaya ya Kaliua na changamoto zinazotokana na hifadhi kwa sababu Kaliua imezungukwa na hifadhi maeneo yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napata mashaka, naendelezea alipomalizia Mwenyekiti wa Kamati yetu. Napata mashaka kama Serikali ina dhamira ya dhati kuondoa migogoro ya wananchi ndani ya Tanzania, napata mashaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napata mashaka kwa sababu huu ni mwaka wangu wa 12 kuwepo ndani ya Bunge hili, tumeunda Kamati nyingi sana na Kamati ya mwisho ambayo nilijua itaondoa migogoro ya wafugaji na wakulima; ya hifadhi na wananchi ni Tume Teule ya Bunge ambayo mimi nilikuwa Mjumbe wake, ilikuwa ina Maazimio tisa muhimu sana, nilijua kuanzia pale tunaondoa kabisa migogoro ya wananchi Tanzania. Bahati mbaya hakuna kinachofanywa, ukiangalia yale Maazimio tisa ya Tume Teule ya Bunge hakuna hata moja ambalo limefanyiwa kazi mpaka sasa hivi.

Leo tumeunda tena Kamati nyingine. Tume ambayo inahusisha Wizara nne na wataalam, jambo la kusikitisha wakati Wabunge tunasubiri tupate majibu namna gani ya kuondoa migogoro hii, tupate ushauri wa ile Kamati, huku wananchi wetu wanateswa, wanapigwa, wananyanyaswa, wananyang’anywa mifugo yao. Nataka Mheshimiwa Waziri atwambie leo, kulikuwa na umuhimu gani wa kutengeneza ile Kamati ambayo ilitumia fedha za walipa kodi wakati majibu hatutajapata ya uhakika? Naomba nipewe majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili; Serikali hii ndiyo imesajili vijiji ndani ya hifadhi, Wilaya ya Kaliuwa ina vijiji 21 ndani ya hifadhi. Wamekwenda kwenye vile vijiji watu wa maliasili wamekwenda kunyang’anya certificate za usajili wa vijiji. Naomba Mheshimiwa Waziri aniambie vile vyeti vya vijiji walivyong’anywa, watu wake wamekuja kuchukua ndani ya vijiji vyetu, viko wapi? Kwa nini hawarudishiwi? Kwa sababu Serikali ni moja, unless niambiwe leo kwamba ndani ya Tanzania kuna Serikali mbili. Serikali inayosajili vijiji na inayokuja kunyang’anya certificate! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba leo Mheshimiwa Waziri unipe majibu vile vyeti virudi kwenye vijiji, vimesajiliwa viko kwenye GN ya Serikali na vitongoji vyake. Naomba vyeti vyao virudi, msijidanganye kuwanyang’anya ili muendelee kuwaadhibu, hatukubali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza hapa Bungeni wiki iliyopita, bahati mbaya sana hata Mheshimiwa Waziri nimezungumza naye siyo mara moja siyo mara mbili, jamani mimi kwanza ni Mhifadhi by professional, lakini uhifadhi wa kutesa watu, kuumiza watoto, kulala kwenye mvua, kuchomewa vyakula, kuchomewa nyumba, hii siyo Tanzania tunayoiamini Tanzania ya amani, siyo kabisa. Wale siyo wakimbizi, kwa nini wakimbizi ndani ya Taifa hili wanaishi vizuri? Kama mlikosea Serikali ikaenda likizo, wakakaa ndani ya hifadhi mkawasajili, watoeni kwa utaratibu, kwa nini mnawatesa watu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nimeongea na wewe mara nyingi suala hili, bahati mbaya sana huchukui hatua zinazotakiwa. Leo Mkuu wa Wilaya anakuwa na power ya kuruhusu watu wakanyanyaswe, nimeongea na wewe hufanyi kazi. Hujafuatilia suala hili hata kidogo! Naongea na watu wa Kanda wanasema hatujui, ukiongea na mtu wa Kaliua anasema hatujui, naongea na Waziri anasema napiga simu kule. Mheshimiwa Waziri wale watu mtuambie mliowasajili ndani ya hifadhi kule Kaliua ni Watanzania au? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtuambie leo, nataka majibu hapa leo, Mheshimiwa Waziri tutagawana mshahara wako leo hapa, hatuwezi kukubali watu waendelee kuteseka kila siku. Bahati mbaya sana ukiuangalia mjadala wa maliasili kila mwaka, almost nusu unajadili migogoro. Nafikiri mngejidhatiti mkaiondoa migogoro wakati wa bajeti tukawa tunajadili namna gani ya kukusaidia Mheshimiwa Waziri kuendeleza utalii, kuendeleza uhifadhi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.