Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Goodluck Asaph Mlinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza naomba nitoe pole kwa Wana-Ulanga wakatoliki kwa msiba wa Father Mdai ambaye amefariki Ijumaa. Suala langu la pili, naomba nitoe pole kwa wananchi hawa wa Ulanga kwa barabara mbovu zilizotukuka lakini naomba niwahakikishie kuwa Mbunge wao nipo na nitapambana mpaka kieleweke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ni-declare interest, mimi nitakuwa upande wa binadamu maana maliasili wao wamejisahau kama siyo Watanzania na kama si binadamu, wanawachukia binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jimbo langu la Ulanga kuna tatizo kubwa la wanyama waharibifu hasa aina ya boko katika kata za Ketaketa, Ilonga, Mwaya, Iyuga na Chilombola. Boko hawa wamekuwa wakiharibu kwa kiasi kikubwa mazao ya wananchi mazao ya wananchi na kupelekea njaa, lakini wananchi wanapowagusa wale boko Maafisa Wanyamapori wanawakamata wanawafungulia mashtaka wanawapa kesi za kuhujumu uchumi. Wanyama wanapovamia tukiwaambia Maafisa Maliasili hawa–responds katika muda ambao unatakiwa. Tumeomba watuongezee ma–game kwa ajili ya kupiga hawa wanyama hawataki, tukitaka tuwavune hawa boko ili wananchi nao wapate kitoweo hawataki.

Sasa mimi naomba niiombe Wizara ya Maliasili mimi kama Mbunge nita–recruit ma–game wa kienyeji katika kila kata kama wao hawatafanya; katika kila kata ambao kazi yao kubwa itakuwa kufukuza hao boko ambao wanaharibu mazao ya wananchi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, katika Jimbo la Ulanga mazingira yake eneo kubwa ni milima na maeneo machache yaliyoko tambarare yote ni maeneo ya maliasili. Upande mmoja lipo eneo tepe tepe wanaliita eneo oevu ambalo kwa kiingereza analiita buffer zone, upande mwingine liko Ilumo na upande mwingine iko Selous Game Reserve.

Kwa hiyo, sasa mshangao wangu mkubwa wakati Wizara inafanya utafiti mwanzo inaweka hiyo mipaka walisahau kama wananchi wanazaliana. Kwa hiyo sasa hivi wananchi ni wengi na eneo ni dogo na hivyo wananchi wanakosa eneo la kulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaposogea katika maeneo ya hifadhi kidogo watu wa maliasili wanakuwa wakali. Waziri Mkuu aliyepita Mheshimiwa Mizengo Pinda alipendekeza na aliunda Tume ifanye mchakato ili kuwaongezea wananchi maeneo ya kulima, lakini mpaka leo hakuna majibu. Mwaka jana baada ya mimi kuwakomalia Wizara wakaja wakatuchukua Wabunge wakatuzungusha na ndege kipindi cha kiangazi, wakasema mnaona wananchi wanavyoharibu maeneo? Mimi nikawakatalia niawaambia kwa nini mnatuzungusha kipindi cha kiangazi? Kwa nini msituzungushe kipindi cha masika. Kwa hiyo, sasa naomba Wizara kupitia hiyo tume yake itoe majibu haraka ili wananchi wapate maeneo ya kulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, nilikuta suala la Operation Tokomeza. Nimeenda nimekuta wananchi wana majonzi makubwa, wananchi wengi wa Ulanga wamekamatwa na mpaka sasa hivi wako ndani na hawajafunguliwa mashitaka yoyote. Kwa hiyo, nilikuwa naomba Wizara kupitia ofisi ya DPP waharakishe ili watu wenye hatia wahukumiwe na watu ambao hawana hatia waachiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo mambo yangu yalikuwa ni machache, hayo yanatosha.