Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Edwin Mgante Sannda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kondoa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza kabisa naanza na itifaki ya pongezi kwa Rais wetu, Waziri Mkuu kwa mpango mzuri na timu yake nzima ya Mawaziri na Manaibu Waziri.
Kwa ujumla mpango huu ni mzuri sana, nami nimeupitia, nimeuangalia kwa kina, kwa upana wake na kwa ujumla wake ni mpango mzuri kweli kweli; wanastahili pongezi sana. However, kuna marekebisho kadhaa yanahitajika katika maeneo mbalimbali ili mwisho tuweze kuunga mkono hoja kikamilifu. Marekebisho hayo ndiyo yataukamilisha mpango huu uwe bora zaidi ya ulivyo sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichangie maeneo mawili tu kwa leo; la kwanza ni lile la uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Tukienda ukurasa wa 15, wanasema Serikali itaendelea kutoa mafunzo ya ujasiriamali na kuwadhamini wajasiriamali wenye miradi inayokidhi vigezo kwenye taasisi za fedha ili wapate mikopo yenye masharti nafuu.
Haya mafunzo pamoja na mpango ule ambao upo ukurasa wa 16 wa shilingi milioni 50 kila kijiji, nafikiri mpango ni mzuri, utekelezaji wake ndiyo huwa tatizo.
Sasa ili tuweze kusaidia, nasi Wabunge kwanza tushirikishwe katika mpango wa utekelezaji mapema, tuwe nao. Tutakachofanya, kikubwa zaidi tunaenda kuandaa watu wetu, kwa sababu mpaka sasa hivi, wana matumaini makubwa kweli kweli, wanasubiri, wana kiu na kadri wanavyosubiri, tunatoa fursa ya maneno ambayo huenda siyo sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge tukiupata mapema kama Wawakilishi wa wale wananchi, tukaenda kule, tukauangalia, tukaanza kuujaribu, tukaanza kuustadi kwa kina, tutaweza kubaini upungufu na kuufanyia marekebisho. Kwa hiyo, kabla ya utekelezaji, tutakuwa tumeweka kila kitu kimekaa sawasawa na hatimaye muda wa utekelezaji unapofika, bajeti inakuwa imekaa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine napenda kushauri na hili lipo kwenye Wizara ya Fedha nafikiri kuna umuhimu sana katika maeneo ya kuboresha, ni kutengeneza mechanism ya monitoring na control, watu watakuwa wameshapata zile fursa, fedha zimetolewa lakini unawezaje kuhakikisha na kutengeneza mfumo wa kwamba tunawakagua hawa watu kadri wanavyokwenda? Vinginevyo hizi fedha zitatoka, mikopo itatolewa, lakini lile lengo tunalotaka lifikiwe mwisho, watu wafanikiwe, wapunguze umaskini, wainue uchumi, tutakuwa tumekwama kama hatutatengeneza mfumo na muundo imara wa monitoring na control.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale wanapokosea, kweli watu wetu sio wote wana ujuzi wa ujasiriamali, wanafundishwa leo, halafu unamkabidhi hela mtu ambaye huenda hajashika kiwango hicho cha hela kwa muda mrefu au labda toka azaliwe, halafu ukategemea atafanikisha kadri tunavyotegemea, inaweza ikawa mtihani mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri Serikali, tutengeneze mechanism nzuri sana ya kuweza kuwachunguza na kuwasimamia hawa mpaka mwisho tuone matokeo yake. Hapo kweli tutakuwa tumefanikisha zoezi na azma yetu ya kuwawezesha wananchi wetu kiuchumi ili tuweze kupunguza umaskini. Hili ndilo eneo ambalo tukiwawezesha hawa wananchi wa kawaida tunaosema ni maskini, ile macro-economy itakuwa supported vizuri sana na wananchi wa kawaida kwa sababu kila mmoja sasa atakuwa kidogo ana nguvu yake na anaweza kuendesha maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo moja la uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, naomba niachie hapo, nafikiri Waziri wetu wa Fedha na Mipango amelipata na Naibu wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia suala zima la elimu. Mpango wa elimu ni mzuri, maeneo yote yameelezewa. Hili lipo kwenye ukurasa wa 49, naomba nisome kidogo mwone jinsi ambavyo inatakiwa iwe. Anasema:
“Hatua zinazochukuliwa zinalenga kuhakikisha kwamba elimu ya Tanzania ni ya viwango vya ubora wa hali ya juu ili kuwawezesha vijana wetu kukabiliana na changamoto za maisha ya kujiajiri wenyewe na kumudu ushindani katika soko la ajira la ndani kikanda na Kimataifa.” Mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kauli ni nzuri sana na imewasilishwa vizuri kweli kweli, lakini lazima tuangalie kwa ujumla wake, ule mfumo, muundo na taratibu za utoaji wetu wa elimu kuanzia awali zinamjenga mtu kwa namna gani. Tunataka practically ziweze kutoa matunda au matokeo ya wanafunzi ambao ni competent, kwenye soko la ajira tukienda huko, tunaona namna tunavyo-perform.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukilinganishwa tu na wenzetu wengine wa nchi za jirani na hapa tumezungumzia kikanda na tumezungumzia Kimataifa, competence yetu kwa kweli inahitaji kuboreshwa sana. Hili ndilo eneo ambalo kwenye hotuba hii ya Waziri Mkuu, kuna umuhimu sana wa kuliboresha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ubora tuuteremshe chini practically, tuhakikishe mifumo, muundo na utaratibu wetu wa kutoa elimu kuanzia chini, unamjenga kijana awe na uwezo, ajiamini, ajitambue kwenye suala zima la nidhamu ya mafanikio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumze jambo moja ambalo kwa kweli linanisikitisha na Naibu Waziri wa Elimu nafikiri yupo hapa. Watu wanaopata Division IV wanachukuliwa kwenda kuwa Walimu.
Sasa kipindi chote hiki ambacho tulikuwa na Walimu waliopata Division IV ndio wanakwenda kufundisha watu, halafu tunataka kujenga matunda ya watu ambao wana kiwango bora cha elimu, hapa kidogo pana mtihani, lazima tubadilishe hili, haiwezekani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatumia neno failure, kwamba Division IV ni failure ingawa kwa sasa kiwango cha Division IV inaonekana ni ufaulu. Sitaki kuamini kama ni ufaulu na ipo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza pia tubadilishe, ufaulu uishie Division III. Unapozungumzia Division one, two, three, ndiyo ufaulu. Sasa tunapiga mahesabu mpaka Division IV mtu anaaminika kwamba amefaulu halafu ndio hao wanaenda kufundisha, halafu tunategemea watoe product ambazo ni nzuri! Siyo rahisi! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka tujenge uwezo, tujenge wanafunzi wanaotoka wanajiamini huko nje; akienda anajieleza, anajiamini. Akiambiwa afanye kazi, ana competence ya kutosha.
Kwa hiyo, napenda nitumie fursa hii kuwasilisha marekebisho kwenye hii hotuba kwamba, suala zima la elimu, dhana ni nzuri sana, lakini ni lazima tuboreshe mfumo na muundo, utujengee na kutoa competence katika elimu yetu kuanzia elementary mpaka Chuo Kikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, kubwa nataka niwasilishe hili la Division III kuendelea kuwa ufaulu, nashauri libadilishwe. Sasa tukishafanya maboresho hayo yote, kimsingi nitakuwa sina shida ya kuunga mkono hoja hii. Ahsante sana.