Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafia
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa hotuba yao nzuri ya bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ukanda wa Kusini (Southern Circuit) upo nyuma sana kiutalii pamoja na ukweli kwamba kuna vivutio vingi vya kitalii. Kwa mfano, Kisiwa cha Mafia katika Mkoa wa Pwani kimejaaliwa kuwa na vivutio vifuatavyo:-
Kwanza kuna whale shark, samaki huyu aina ya papa (potwe) wamebaki wachache sana na katika nchi chache duniani. Moja ya sifa nyingi za samaki huyu ni rafiki kwa mwanadamu kama livyo pomboke (dolphin) na watalii wanapenda sana kucheza na kuogelea naye. Kwa sasa samaki huyu anapatikana Australia, Philippines na nchi chache za Bara la Amerika ya Kaskazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na umuhimu wake na mvuto wake kwa watalii hakuna juhudi zozote kutoka upande wa Serikali katika kumtangaza samaki huyu. Juhudi pekee ni zile zinazofanywa na mmiliki wa hoteli na mtalii mwenyewe. Tunaiomba Serikali sasa itangaze kivutio hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili kuna scuba diving, hiki ni kivutio kingine kinachopatikana kisiwani Mafia. Mandhari ya chini ya bahari ya Mafia imesheheni samaki wa aina mbalimbali ambazo zinawavutia watalii kuja na kufanya uzamiaji wa bahari. Tunaiomba Serikali sasa itangaze kivutio hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu ni sports fishing ambapo ni uvuvi wa mchezo maarufu kama catch and release ambapo watalii wanavua samaki na kupiga nao picha halafu huwarejesha baharini akiwa hai. Ni kutokana na vivutio hivi pamoja na vivutio vingine vya Kusini vya Mji wa Kilwa na magofu yake, mbuga ya Selous na hot spring Utete Rufiji; Serikali sasa ije na mpango mkakati wa kutangaza vivutio hivi vya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni idadi ya watalii wanaotembelea nchi yetu. Ni ukweli usio na shaka kumekuwa na ongezeko la utalii nchini. Lakini kuna utata mkubwa namna ambavyo takwimu hizi zinakokotolewa. Nimeomba Mheshimiwa Waziri wakati anakuja kujibu atupe ufafanuzi juu ya kadhia hii. Je, watalii hesabu inachukuliwa kwenye mipaka yetu au viwanja vya ndege na mipaka ya bandari na bandari zetu au wakati wanaingia kwenye vivutio vyetu? Je, watalii wanaoingia Zanzibar moja kwa moja na kuondokea huko huko hawa wamo katika idadi ya watalii milioni 1.2 walioingia Tanzania mwaka wa jana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii na ninaunga mkono hoja. Ahsante.