Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kigoma Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuwapongeza Waziri na Naibu Waziri kwa kazi kubwa na nzito wanayokabiliana nayo. Niwatie moyo kuwa mnaweza na muendelee kuchapa kazi na kutatua kero zilizopo ndani ya Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuzungumzia hifadhi ambazo zipo karibu ya makazi ya wananchi na kwa miaka mingi hifadhi hizo haziendelezwi badala yake hifadhi hizo zimekuwa mapori. Mfano, Hifadhi ya Lukunda Pachambi, msitu huu unaingia kwenye kata tatu; Kata ya Mtego wa Noti, Kata ya Mganza na Kata ya Nguruka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hifadhi kama hizi za Lukunda Pachambi na Tandala Ilunde ziwekewe mikakati maalum ikiwezekana baadhi ya maeneo yatengwe kwa ajili ya wafugaji ili kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie migogoro ya baadhi ya vijiji na hifadhi zetu. Naona Mheshimiwa Waziri kwenye kitabu hiki cha bajeti kazungumzia tatizo hili la migogoro ya hifadhi na vijiji (ukurasa wa 61) kuwa timu iliundwa ya kutatua migogoro ya wafugaji na wakulima na ilifanya kazi kwenye mikoa mitano. Kamati ilihusisha Wizara ya Maliasili na Utalii, TAMISEMI, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hapa nizungumzie mgogoro wa Hifadhi ya Mahale na vijiji vya Sibwesa, Kalilani, Lubilisi na vijiji vingine vilivyopo karibu na hii Hifadhi ya Mahale. Mgogoro wa Hifadhi ya Mahale na vijiji viwili kati ya hivyo hapo juu, kijiji cha Kalilani na kijiji cha Sibwesa una miaka zaidi ya 30 na vijiji hivi vimesajiliwa kwa mujibu wa sheria. Natambua zoezi la uwekaji wa beacons ni agizo la
Mheshimiwa Waziri Mkuu lakini vijiji hivi vilitangazwa kwa mujibu wa sheria na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumshauri Mheshimiwa Waziri kwa nini suala hili la vijiji viwili vya Sibwesa na Kalilani ambapo mgogoro wake umedumu kwa takribani miaka 30; kwa nini basi usuluhishi usifanywe na Wizara ya Maliasili, wananchi kwa maana ya Serikali za Vijiji vya Sibwesa na Serikali ya Kijiji cha Kalilani, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi na TAMISEMI?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri hili ili mazungumzo yafanyike kwa utaratibu wa Serikali na siyo hivi sasa Hifadhi ya Mahale inavamia na kuweka beacons pasipo ushirikishi wa Serikali za Vijiji na TAMISEMI, kwa sababu GN za vijiji zinaingiliwa na beacons hizi. Namuomba sana Mheshimiwa Waziri, natambua ni mtu sikivu sana na muelewa kwa miaka mingi sana. Hivyo, tuombe haki ya wananchi hawa wa vijiji hivi ilindwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuishukuru TANAPA kwa kutoa shilingi bilioni 1.6 za kujengwa madaraja matatu. Daraja la Rukoma, Daraja la Lagosa na sasa wanaendelea kujenga daraja la mwisho. Kwa niaba ya wananchi wa huu Ukanda wa Ziwa Tanganyika tunaishukuru sana TANAPA kwa msaada huo na bado tunaomba msaada wa ujenzi wa barabara inayokwenda Mahale kilometa 30.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.