Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Maria Ndilla Kangoye

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Nianze kwa kuipongeza Wizara kwa hotuba nzuri yenye ufafanuzi unaoeleweka kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) imekuwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa wataalamu wa kutosha, ninashukuru hotuba imelitambua pia suala hili ni imani yangu kuwa Serikali itaongeza wataalam ambao wengi wapo mitaani hawana kazi na wengi wao pia ni vijana ambao wamekuwa wakihangaika kutafuta kazi kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto hiyo ya ukosefu wa wataalam wa kutosha, bado taasisi hii ya TAWIRI inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vitendea kazi, suala ambalo ni muhimu katika kukamilisha majukumu ya taasisi. Pamoja na hilo bado vitendea kazi vilivyopo ni vichakavu na hivyo basi nipende kuiomba Serikali kuipa kipaumbele taasisi hii kwa kuipatia fedha za kutosha ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufasaha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hotuba hii na Mkoa wa Mwanza, kwanza kabisa nianze kwa kuelezea masikitiko yangu makubwa kwa namna Wizara ilivyoutenga Mkoa wa Mwanza. Ukipitia hotuba yote toka ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho, hakuna sehemu yoyote utakayokuta mpango wa kuboresha, kutangaza au kuendeleza utalii Mkoani Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni suala la aibu sana ukizingatia masuala yaliyopo Mwanza ambayo yangeweza kuvutia watalii wengi na kuliingizia Taifa fedha kupitia utalii. Ni muda mrefu sasa Serikali imekuwa haiuweki Mkoa wa Mwanza kwenye mpango wa kuendeleza utalii nchini, tunajiona kama vile tumetelekezwa na Serikali ukizingatia Awamu hii ya Tano Serikali imebakiza miaka mitatu tu na kwa miaka miwili hii ya mwanzo bado haijaona umuhimu wa utalii wa Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niikumbushe Serikali kuwa Mkoa wa Mwanza una Hifadhi ya Saanane Island ambapo wanyama wengi wapo na kuna kilele kirefu ambacho mtu huweza kuliona Jiji la Mwanza na uzuri wake kwa ujumla. Zipo pia sauti za makumbusho mbalimbali kama Bukumbi ambayo inajenga historia ya dini ya kikristo na muhimu kwa kumbukumbu ya uanzishwaji wa dini hiyo kwa Uganda na Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo pia makumbusho ya Kageye ambapo kuna makaburi ya watafiti au explorers Frederick Barker ambaye alifariki mwaka 1875 kwa kuugua kipindupindu na Dkt. Junker ambaye alitumwa na nchi ya Urusi kuja Afrika kutafiti nchi za Sudan na Egypt.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kipo pia kituo cha makumbusho cha kabila kubwa kabisa la Wasukuma maarufu kama Bujora Sukuma Museum ambapo kuna historia ya chiefdoms zote za kabila hilo lililosambaa katika mikoa minne ambayo ni Simiyu, Mwanza Shinyanga na Tabora. Na kila mwaka kituo hiki huandaa tamasha la kitamaduni maarufu kwa jina la Bulabo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka enzi za utoto wangu kijiji changu cha Bujora kilikuwa kinasheheni watalii kutoka pembe mbalimbali za dunia kuja kujionea ngoma za Kisukuma katika tamasha hili la Bulabo na kwa mwaka makumbusho hayo yalikuwa yanatembelewa na watalii sana. Kama sijakosea na kwa ufahamu wangu duniani kuna jiwe moja tu linalocheza na lipo Wilayani Ukerewe. Pamoja na vyanzo hivyo vya utalii bado Mkoa wa Mwanza unapakana na nchi za Uganda na Kenya, ukivuka Ziwa Victoria na kwa kutangaza utalii wa Mkoa wa Mwanza tungeweza kuvutia wengi kutoka nchi hizo na nyinginezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Serikali ni kuhakikisha kuwa masuala haya ya utalii Mwanza yanatangazwa na ukweli itafika kipindi na sisi tutachoka kuona Serikali inatusahau kila mwaka na huku vijana wa Mwanza wanahangaika kwa kukosa ajira wakati wangeweza kuajiriwa ama kujiajiri kupitia sekta hii ya utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kulitazama ombi langu kwa ukaribu kwani tunapoteza mapato mengi mno kwa kutokujali kuendeleza utalii wa Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango wangu huu naunga mkono hoja.