Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Anna Joram Gidarya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa mchango wangu wa maandishi katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na migogoro ya mipaka kati ya wafugaji na wakulima (vijiji). Kumekuwa na migogoro ya mipaka ya muda mrefu kati ya hifadhi zetu na wafugaji na wakulima ambao wako jirani na hifadhi. Migogoro hii imekuwa kero kubwa sana hata kusababisha madhara makubwa sana kwa wananchi, kupigwa risasi na askari wa hifadhi na kusababisha vifo vingi vya wananchi, wanawake wengi kubakwa na askari wa hifadhi. Katika kata za Aya Mango, Gedamara na Gijedabung’ walibakwa hadi kufa na mpaka sasa Wizara haikushughulikia jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ifanye mpango wa haraka wa kumaliza migogoro hii katika vijiji vya Gijedabung’, Aya Mango, Gedamara, Maweni, Mdori, Nkaiti, Mwada - Kisangaji na Sangaiwe ambao umedumu kwa takribani miaka kumi sasa. Kwa sasa hali ya mahusiano ya wananchi na wafanyakazi wa hifadhi ni mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sheria ya kulipa fidia na kifuta jasho, ni jambo la kawaida sana na la hatari sana kwa Wizara hii kwani mpaka sasa pesa inayotolewa kama kifuta jasho ni ndogo kwa waathirika walioathiriwa na wanyama. Kwa mfano, tembo kuharibu mazao, kuua watu, simba kuua watu na kukamata wanyama wafugwao. Naomba Wizara iangalie namna ya kuongeza kifuta jasho hicho kwani madhara ni makubwa sana ambayo haiendani na hiyo shilingi milioni moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Sheria ya Utunzaji wa Mazingira (EMA) na Sheria ya Ardhi kuhusu mita 60 kutoka katika kingo za mito na bahari.

(i) Sheria ya Ardhi (Land Act 4/5 1999) inaeleza juu ya mita 60,
(ii) Land Survey (Act Cap 324 RE. 2002); na
(iii) Planning Act (No. 8 2007).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Mazingira ya mwaka 2000 kifungu namba 57 imeelezea mambo haya ya utunzaji wa mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto tuliyonayo pamoja na sheria hizi ni nyingi sana, kumekuwa na uharibifu unaotokana na mmomonyoko wa ardhi katika maeneo mengi, hasa katika maeneo ya ukanda wa Bonde la Ufa. Kunapotokea hali hiyo ya tendo la asili la ardhi kumomonyoka, kingo zinasogea na zile mita 60 zinapungua, wakazi wa maeneo husika kusumbuliwa kuondolewa katika maeneo hayo, Wizara inajipangaje kuelimisha wananchi kuhusu madhara yatokanayo na mmomonyoko wa ardhi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni na ushauri; Wizara iandae utaratibu wa kujenga mahusiano mazuri katika kutangaza utalii na hifadhi zetu kwa kushiriki shughuli za kijamii katika maeneo yote yenye hifadhi. Kwa mfano, kujenga vyumba vya madarasa (shule), kujenga zahanati, huduma za maji, kuanzisha timu za mpira, michezo ya riadha na mashindano ya mavazi ya asili ili jambo hili liwe chanzo na mwanzo mzuri kwa Wizara hii kuwa na mahusiano mazuri na jamii inayowazunguka. Hili ni jambo muhimu ambalo litajenga mahusiano makubwa mazuri na kuwajengea uwezo mpana na uelewa juu ya hifadhi zetu, faida za hifadhi zetu kupitia huduma wanayopata kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii. Ahsante.