Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu na naunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia kuhusu hali ya utalii nchini. Sekta ya utalii ni moja kati ya sekta ambazo huliingizia Taifa mapato makubwa na pia hutupatia fedha za kigeni. Pamoja na umuhimu wake bado bajeti yake ni ndogo, lakini pia Serikali haijakuwa na mipango mizuri kiasi kwamba ushindani kati yetu na nchi jirani unakua siku hadi siku. Kwa kukosa mipango mizuri, imefikia leo Tanzania pamoja na mbuga nyingi na kubwa, mapango, maporomoko, maziwa, wanyama wengi, ndege, wadudu na samaki, mapato yetu bado hatuifikii Kenya, Ethiopia, Botswana, Zambia, South Africa, Rwanda na kadhalika, bado mapato yetu ni madogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Wizara ya Maliasili na Utalii ishirikishe wadau mbalimbali katika kutoa mchango wa mawazo katika sekta ya utalii ili yatapatikane mawazo mengi yenye manufaa na yataisaidia Serikali. Kwa mfano, advertisements (matangazo), bado Tanzania hatujatangaza utalii wetu katika mataifa ya nje kiasi cha kutosha ukilinganisha na washindani wetu Kenya, Uganda, Malawi, Namibia, Rwanda na kadhalika. Tuwatumie Watanzania wanaoishi nje (diaspora) washirikiane na Mabalozi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunadhani utalii ni wanyamapori na hoteli tu, sivyo. Katika ukurasa wa 12 – 59 wa hotuba ya Waziri anazungumzia wanyamapori tu. Je, Makumbusho, Olduvai Gorge, Tongoni Ruins, Amboni Caves, Michoro ya Kondoa Irangi, Magofu ya Pangani, Amboni Sulphur Bath, yote haya tunayaacha bila ya kuyatangaza. Nashauri sasa tufanye matangazo ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Tanga na utalii; Tanga ni mji wa kihistoria, una majengo mengi ya kihistoria, una bandari, railway na hata makazi ya kale, kuna visiwa vilivyokuwa na magofu na makaburi yaliyodumu kwa zaidi ya miaka 200. Hivyo, naishauri Serikali itenge eneo la Posta na Uhindini kuwa eneo la kihistoria kama lilivyo eneo la Stone Town, Zanzibar. Tanga tunayo Mapango ya Amboni (caves), Tongoni Ruins na Amboni Sulphur Bath.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sports tourism kama football, basketball, netball, golf, cricket, etc ni michezo ambayo nchi za wenzetu wanaitumia na kuingiza mapato kwa kufanya mashindano ya kimataifa, mfano Dubai Open, golf umekuwa ni mchezo mkubwa unaoingiza fedha nyingi katika sekta ya utalii na pia surf (swimming and fishing) ni michezo ambayo tukishirikiana na sekta binafsi tutaweza kufanya vizuri kwa kuwa wenzetu wa nchi za Kenya, South Africa na Mauritius wanafanya vizuri, tusibaki nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mali kale na makumbusho, hadi leo mjusi wa Tanzania dinosaur yupo Ujerumani na anaiingizia fedha za kigeni nchi ya Ujerumani. Kwa nini asirejeshwe kama fuvu la Mkwawa na awekwe katika Makumbusho ya Taifa? Tunahitaji mjusi wetu arejeshwe Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna 1424km3 za bahari kuanzia Jasini (Mkinga District - Tanga) hadi Msimbati (Mtwara), amegundulika samaki kisukuku (coelecanthy) ambae alikosekana zaidi ya miaka 80 iliyopita, Tanga – Kigombe (Muheza) amepatikana. Taasisi za kimataifa kupitia Mradi wa Coast Zone wameweka kambi na wanaendelea na kukusanya taarifa zake. Je, Wizara wana habari? Habari ndiyo hiyo.