Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kawaida yangu, nataka nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia zawadi ya uhai, kunipa afya bora ili niweze tena kusimama kwenye Bunge lako na niweze kutoa mchango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niweke sawa kumbukumbu, katika Bunge hili kuna Wizara tatu zinachangiwa kwa mfumo wa aina yoyote mchangiaji anayotaka. Wizara ya kwanza ni Ofisi ya Waziri Mkuu, unachangia kwa hoja zozote unazojisikia Mbunge. Wizara ya pili ni TAMISEMI, unapiga kokote Mbunge unakotaka kupiga; na ya tatu ni Finance Bill, kwa hiyo, kama mtu huelewi, Mbunge ukisimama Wizara hizo, usiache kitu! Kula moto, tema madini, watu watakusikiliza. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Waziri Mkuu, amefanya kazi kubwa tangu ameteuliwa kuwa Waziri Mkuu. Tuna uhakika kwamba Rais hajakosea kukupa kiti hicho Mheshimiwa Majaliwa na wala sisi Wabunge hatujakosea kukuidhinisha. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, katika Majimbo ya Waheshimiwa Wabunge wengi hapa Tanzania likiwepo la Mtera, kuna baadhi ya miradi imekuwa ya muda mrefu, imekuwa miradi sugu. Tufanye utaratibu wa kila Mbunge akuandikie ni mradi gani umechukua muda mrefu haujatekelezwa, tukuletee ili kuwe na bajeti maalum ya kuondoa viporo vya miradi iliyopita. Tukifanya hivyo, tutakufanya uanze sasa kutekeleza miradi mipya wakati umekamilisha ile miradi ya zamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nilisema kwenye Bunge hili kwamba, ndugu zangu hawa wamechanganya mayai yote kwenye kapu moja, tupige. Nilizungumza nikiwa mahali hapa! Leo tumepiga, si mnaona biashara imekwisha?
Kwa hiyo, niwaambie tunampongeza sana Mheshimiwa Rais, kuna wengine wanasema anatafuta umaarufu; hivi ukimshinda mtu anayesema mafuriko hayazuiwi kwa mikono, wewe ukayazuia, unataka umaarufu gani tena? Mheshimiwa Dkt. Magufuli anatafuta umaarufu upi kama amekuwa binadamu wa kwanza duniani kuzuia mafuriko kwa mikono? Anatafuta umaarufu upi? Tuliwaeleza hawa na leo nataka niwathibitishie, nataka niseme na nchi, nataka niwaambie Watanzania kwamba hawa jamaa mliowapigia kelele, leo hii wameonesha wamefeli, hawana uwezo wowote hata ndani ya Bunge hawa! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Rais. Leo wanasimama hapa, watu wa Dar es Salaam mnisikilize. Anasimama hapa Kiongozi wa Upinzani anasema, Rais anafanya makosa kuamrisha pesa zilizokuwa ziende kwenye sherehe zijenge barabara ya Morocco. Wapinzani wanasema ni makosa. Hivi watu wa Dar es Salaam mnawapendea nini hawa? Hawa watu hawataki maendeleo! Wanataka domo! Mnawaona, wanataka waonekane kwenye TV wanasema bajeti ile na hela za kutengenezea barabara ya Mwanza, wanataka tukupe Mheshimiwa Nape halafu urushe live TBC ili waonekane hawa. Kutengeneza barabara na kuonekana kwenye TV lipi bora jamani?
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme hapa na nazungumzia hapa kwenye ukurasa wa 11, 17 kipengele kinachohusu demokrasia. Someni hapo! Mheshimiwa Waziri Mkuu huwezi kukuza demokrasia kama una Wapinzani wa jinsi hii. Haiwezekani! Utakuzaje demokrasia katika nchi kama Wapinzani ulionao ni wa aina hii?
TAARIFA
MBUNGE FULANI: Taarifa Mwenyekiti! Mwenyekiti taarifa!
MWENYEKITI: Mheshimiwa Lusinde kaa!..
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka kumwonya mzungumzaji anayezungumza. Mimi ni Mbunge senior na mwenye jina kubwa kuliko wewe. Unaposema kwenye Bunge hili, unamtolea mtu taarifa; wewe kama unaweza kusema umeambiwa, sema; kama hujafukuzwa Chama! Simama useme humu! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia kukua kwa demokrasia. Mimi hapa nataka leo nitoboe ndiyo maana nimesema leo najitoa muhanga. Katika maisha yangu nimewahi kuwa Kiongozi; Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la CHADEMA. Kule ndani kulikuwa na siri kubwa! Tulikuwa tumepanga siri wakati huo, niliyoikataa mimi, mpaka nikahama Chama hiki ya kuua Vyama vingine. CHADEMA wamefanikiwa kuua Vyama vyote hapa Tanzania.
Kwa hiyo, tunapozungumzia kukuza demokrasia tujue kwamba NCCR-Mageuzi ilikuwa na Wabunge watano na sasa ina Mbunge mmoja tu. Sijui ni maendeleo gani hayo? Wanaviua Vyama! Hawa wako kwa ajili ya kuua Vyama vingine! CUF walikuwa na Wabunge chungu nzima, sasa hivi Zanzibar sifuri. Hawa! Hawa wanaua Vyama vingine. Wanataka kubaki peke yao.
Kwa hiyo, nakuomba Msajili wa Vyama vya Siasa, endelea kusajili Vyama, ukifanya mchezo nchi hii demokrasia itakufa kwasababu kuna Chama kinataka kuhodhi Vyama vingine vyote viwe ndani yake. Hawa wanataka kufanya hivyo! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, CCM huko nyuma tulikuwa na zidumu fikra za Mwenyekiti. Tumetoka, hawa wameingia huko. Hawa sasa hivi zidumu fikra za Mwenyekiti, ndiyo maana unaona kila wakiambiwa kitu, wanafanya. Jambo la aibu sana! Unasimama kwenye Bunge hili, unasema Serikali imevunja Katiba, haiko Kikatiba, Serikali hii imekosea, kwa hiyo, hatutasema, lakini posho wanachukua, hawa! Yaani kama ni Waislamu; kama una Muislamu anasema hali nguruwe, anakula maini tu, ndiyo hawa! Wanasema Serikali hii imekosea, haiko Kikatiba, lakini mishahara na posho wanachukua hawa. Hawako tayari kusema! (Kicheko/Makofi)
Kwa hiyo, nakuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, sasa nimegundua siyo tu tuna wafanyakazi hewa, tuna Wabunge hewa; hawa! Bunge hili lina Wabunge hewa! Nataka nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Nape. Wizara yako Mheshimiwa Nape ilikuwa haijawahi kuchangia maendeleo yoyote vijijini zaidi ya habari, tunasikia michezo lakini kwa mara ya kwanza, pesa ulizozizuia ambazo mmeshauri, sasa zinaelekea kuchimba visima vya maji. Tunakupongeza sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanataka maji, hawataki kumwona Mbunge kwenye TV. Tunafahamu wamepata political mileage sana kwa sababu ya kusema mambo ya hovyo, watu wanayasikia, lakini kwa sasa watatakiwa kwenda kufanya kazi na kutoka jasho ili wananchi wawakubali. Ofisi ya Waziri Mkuu inashughulika na TASAF. Kwenye TASAF kuna malipo hewa. Wako watu wamekufa, lakini wanaendelea kupokea zile hela kama ambavyo tuna Wabunge wamekufa, hawazungumzi Bungeni, lakini wanapokea hela. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyakazi hewa wako wengi sana kwenye nchi hii, tuwashughulikie. Kuna watu hapo wanazungumza habari ya kumponda Rais kwamba anakurupuka kuchukua maamuzi. Rais, watu wote anaowafukuza na wanaosimamishwa ni kweli majipu. Kwa mfano, mchukulie ndugu yangu Kabwe. Mbunge wa Upinzani alisimama hapa, Mheshimiwa Wenje akasema Kabwe ni jipu hafai atolewe na hawa wakampigia makofi. Leo kasimamishwa, hawa wanasema anaonewa. Huwezi kuwaelewa hawa! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu wana-CCM pamoja na Waheshimiwa Mawaziri, kwa Baraza hili aliloliunda Mheshimiwa Rais, kule Mheshimiwa Majaliwa, pembeni Mheshimiwa Nape, kule kuna Mzee Handsome boy, hapa Mheshimiwa Mavunde, Mheshimiwa Jenista Mhagama; hawa hawachomoki, ndiyo maana mnaona wanapiga kelele! Mnawaona wanapiga kelele hawa, anazungumza habari ya shule wakati CHADEMA ilimsimamisha Rajabu Jumbe kugombea Umakamu wa Rais akiwa darasa la saba, wewe umesahau? Sasa kama ninyi mlitaka kuleta Makamu wa Rais darasa la saba, itakuwa Mbunge! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza sana Serikali. Nataka niwaambieni, katika siasa duniani, mimi ni Mwanafalsafa, nikija kufa ndiyo mtaelewa kwamba yule mtu alikuwa wa namna gani. Katika watu ambao wanajua siasa na wamefanya, nawaambieni Tanzania hatuwezi kusonga mbele. Wana-CCM tujigawe; wawepo Wabunge wa Upinzani kutoka CCM, tuisaidie Serikali. Hawa tuachane nao! Hakuna kitu wanachokifanya hawa! Tukiendelea kuwaamini hawa, tutapoteza point nyingi sana. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, duniani kote, Chama cha Upinzani kinakuwa na hoja moja tu. ANC wameshinda uchaguzi pale, hoja yao ilikuwa Ubaguzi; lakini hawa umeme, barabara, maji nini, hawa Wapinzani wa wapi? Hakuna Wapinzani wa namna hiyo! Mpinzani anakuwa na hoja moja tu. Anaijenga na anaaminika kwa watu. Hawa hawaaminiki, wanazungumza kila kitu! (Kicheko/Makofi)
Nakuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, maendeleo katika nchi yetu kuna mikoa imechelewa kupata maendeleo kwa sababu resources zetu kuwa ndogo, igeukieni hiyo, acheni mikoa ambayo wananchi wameshiba, wanachagua Mbunge kuja kunyamaza tu Bungeni, achaneni nayo! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, wakati wa kutekeleza hoja hii, fanyeni kazi kwa Waheshimiwa Wabunge waliochangia shida zao; hawa walionyamaza achaneni nao, hawana shida hawa. Mbunge anatoka nyumbani anakuja kukaa hivi, hasemi shida yoyote halafu baadaye wanakuja kwenye viti vya Mawaziri kunong’ona; Waziri mtu mzuri. Unafiki wa namna hiyo haukubaliki! Tunataka waseme wazi. Wakisimama hapa, wanakashifu Mawaziri, wanawatukaneni, halafu wanakuja kwenye kiti, naomba umeme. Tunataka maombi wanayoyaleta mezani kwenu, wayaseme wazi. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri wa Fedha, tunakufahamu, wewe ni mtaalam; umekuwa Bwana Mpango, umeongoza maeneo mengi. Tunataka safari hii, Serikali ya Awamu ya Tano, mipango yenu yote mliyoipanga na mkatupa asilimia 41 ya pesa, zishuke kwa wananchi ili maendeleo yapatikane, tuwakate mdomo hawa. Sasa hivi tutafanya!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie, tutatengeneza umoja wa kutembea Jimbo kwa Jimbo kuwaambia hawa wasichaguliwe tena 2020. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuzungumzie barabara. Ukitoka hapa kwenda Iringa, kuna kipande cha barabara ambacho Mheshimiwa Rais ameshakiahidi kutoka barabara ya lami inayokwenda Iringa ipite barabara ya lami mpaka Hospitlai Teule ya Mvumi. Naomba kipande hicho mkikamilishe ili mimi niwe Mbunge wa maisha wa Jimbo lile. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie, katika wanasiasa wanaoniuma; nazungumzia demokrasia, lazima niwe mkweli; ananiuma sana kaka yangu Mheshimiwa James Mbatia. Mheshimiwa Mbatia ni mwanasiasa wa siku nyingi kuliko Mheshimiwa Mbowe. Sijui kalishwa nini, siku hizi anaambiwa na Mheshimiwa Mbowe, nyamaza! Naye ananyamaza kweli! Ananyamaza! Yaani sielewi kilichotokea!
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mbatia ni Mwanasiasa wa siku nyingi, Chama chake kilikuwa na Wabunge watano. Akanambia yeye amesoma, mimi sijasoma, sasa anakwenda mbele. Kutoka watano kuja mmoja! (Kicheko)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Lusinde inatosha kwa leo, muda wako umemalizika!
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Kweli hata mimi ambaye sijasoma siwezi kufanya ujinga kama huo! Hata mimi ambaye sijaenda shule, siwezi kufanya kitu cha namna hiyo. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Hawa tunawamudu, hamna kitu na tutahakikisha tunawafagia. Ahsante sana.