Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Zainabu Nuhu Mwamwindi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kuwa na afya njema na kushiriki katika Mkutano huu wa Saba wa Bunge la Bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nimpongeze Spika, Mheshimiwa Job Ndugai, Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas Kashililah, Wenyeviti wa Bunge na watendaji wote wa Bunge kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yenu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumpongeza Rais wangu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa pamoja na Baraza lote la Mawaziri kwa kazi nzuri wanayoifanya kwa kuwaletea maendeleo wananchi katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua jitihada kubwa zinazofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya Waziri, Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe, Naibu Waziri, Mheshimiwa Injinia Ramo Makani na watendaji wote wa Wizara hii, mfano, katika kupambana na majangili katika hifadhi zetu, kuendelea kutatua migogoro kati ya hifadhi na vijiji vilivyo jirani na hifadhi na kutangaza utalii wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Taifa ya Ruaha iliyoko umbali wa kilometa 130 kutoka Mjini Iringa ina sifa za kipekee kuliko mbuga zote nchini na katika Bara la Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na sifa hii bado haijatoa tija inayostahili kwa Taifa. Miundombinu hasa barabara itokayo Iringa Mjini siyo rafiki kwa watalii wa ndani na nje ya nchi. Ujenzi wa barabara ya lami kutoka Iringa Mjini kuelekea mbugani hadi sasa uko katika kilometa zisizozidi 15 kutoka Iringa Mjini. Siyo rahisi kwa watalii wengi kuvutiwa na safari ya kilometa 115 katika barabara yenye vumbi hivyo tunakosa mapato mengi ambayo yangeweza kupatikana kwa kukosa wageni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili, tunalo jengo la kumbukumbu ya Chifu Mkwawa (Mtwa) liko umbali usiozidi kilometa 3 kutoka Kijijini Kalenga, njia inayoelekea katika kumbukumbu hii haina lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali, iboreshe uwanja wa ndege ili ndege kubwa na ndogo ziweze kutua na kuruka jambo ambalo litavutia watalii wengi. Aidha, ujenzi wa barabara ya lami kwenda Ruaha National Park uharakishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba TANAPA iendelee kusaidia maendeleo hasa katika maeneo ambayo vivutio vya utalii vinakopatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante.