Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumrudishia sifa na utukufu Mwenyenzi Mungu kwa kila jambo. Ninamshukuru Mungu kwa wema na fadhili zake kwa kutujaalia afya njema na uhai sisi Wabunge, viongozi na watumishi wote wa Bunge wa Bunge lako Tukufu na kwa kutuwezesha kumudu majukumu yetu ya kuwatumikia wananchi tukiongozwa na viongozi wetu wa wakuu wa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru wewe binafsi kwa kunipatia fursa hii adhimu ili niweze kuchangia mjadala ulioko mbele ya Bunge lako tukufu kwa kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wa mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kufafanua baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge kwa kadri muda utakavyoniruhusu ninapenda kuwapongeza Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakiongozwa na Mwenyekiti Mheshimiwa Mhandisi Atashasta Justus Nditiye na Makamu wake Mheshimiwa Kemirembe Julius Lwota kwa kuendelea kuishauri na kuisimamia Wizara yetu katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa katiba, sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru wananchi wa jimbo langu la Tunduru Kaskazini kwa kuendelea kuniamini lakini pia nashukuru familia yangu. Pia nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote waliopata fursa ya kuchangia kwa maandishi na kwa kuzungumza na sasa nianze kufafanua baadhi ya hoja zilizotolewa kupitia Taarifa ya Kamati ya Kudumu, Taarifa ya Kambi ya Upinzani na Waheshimiwa Wabunge mmoja mmoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Taarifa ya Kamati kutokana na muda niseme tu kwa ujumla kwamba maoni yaliyotolea kwenye Taarifa ya Kamati mengi ni maoni ambayo hakuna jambo tunaloweza kufanya isipokuwa ni kuyachukua na kwenda kuyafanyia kazi. Tunapokea maoni hayo na ushauri wote ulitolewa toka kwa Kamati kama yalivyoainishwa katika sehemu ya tatu sura ya sita ukurasa wa 22 mpaka 34 wa taarifa hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitapenda kuzungumzia tu mambo mawili kwa muda huu ulionipa. Kwanza nitazungumzia suala la WMAs ambazo kwenye Taarifa ya Upinzani limezungumzwa kwa kirefu hasa ukurasa wa 13 kuna hoja zimetajwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa hoja ya mgawanyo wa mapato katika WMAs kuwa haufuatwi ipasavyo kwa mujibu wa sheria au kanuni, iko hoja ya kwamba Serikali inachukua kiasi kikubwa cha fedha kinachotokana na mapato ya utalii kwenye hizo WMAs, iko hoja inasema Serikali inachukua asilimia 55 na kuacha kiasi cha asilimia 45 peke yake kwa WMAs.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipengele hiki napenda kusema kwamba Kambi ya Upinzani iende ikaangalie upya kule ambako wameweza kuchukua taarifa hizo na hasa takwimu ili waweze kuja na takwimu ambazo ni sahihi, kwa sababu kwa mujibu wa kanuni zilizosainiwa mwaka 2012 mgawanyo wa mapato yanayotokana na utalii kwenye WMAs hauoneshi kwamba WMAs zinapata mapato kama ilivyoainishwa kwenye taarifa hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapato kwenye utalii wa uwindaji yapo ya aina nyingi kama sita hivi, mimi nitaje haraka haraka tu, ipo block fees ambayo WMAs inapata asilimia 75, game fees WMAs inapata hiyo asilimia 45 na nyinginezo. Kutokana na muda kiufupi niseme tu kwamba mapato yanayotokana na shughuli za uwindaji wa kitalii WMAs zinapata mgao ambao si mdogo kulinganisha na ule ambao unakwenda kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia yapo mapato yanayotokana na utalii wa picha. Kwenye upande wa utalii wa picha kanuni zinasema kwamba WMAs zinapata asilimia 70 na wala si asilimia 45 kama ilivyoainishwa. Ninazo hizo takwimu hapa kwa mujibu wa hizo kanuni, Waziri Kivuli akizihitaji nitaweza kumpatia kwa rejea yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia lipo suala la WMA ya Burunge kwamba kwa mujibu wa taarifa hiyo ni kwamba WMA ya Burunge imepata mapato yafikiayo takribani shilingi bilioni sita na kwamba WMA hiyo inaambulia shilingi milioni 800 pekee. Ukweli ni kwamba kwa sababu mgawanyo wa mapato unakwenda kwa mujibu wa sheria, ni vema tukazingatia kwamba takwimu ambazo zipo sahihi ndizo peke yake zinazoweza kutoa mwelekeo juu ya mgawanyo wa mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kama nilivyosema pale awali kwamba takwimu zilizotolewa na Kambi ya Upinzani zinatakiwa zifanyiwe marejeo kwa maana ya kwamba tunawaalika waje wazitizame kwa sababu kosa kama hili haionekani kama lingeweza kutokea kwa sababu ni kosa kubwa sana. Hii ni kwa sababu jumuiya ya hifadhi ya wanyama pori moja haiwezi kupata pato la shilingi bilioni sita ingawa hakutaja ni kipindi gani. Kwa sababu kwa mujibu wa kumbukumbu tulizonazo kama Serikali pato la shilingi bilioni sita ni pato la WMAs zote nchini, tena si kwa mwaka mmoja, ni kwa miaka mitatu yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa mapato yote ya WMAs kwa muda wa miaka mitatu, 2014/2015, 2015/2016 na 2016/2017 ni shilingi bilioni 5.515. Kwa hiyo, kwa upande huo wa takwimu niseme tu kwamba tunamkaribisha aje aweze kuchukua takwimu sahihi ili aweze kujenga hoja zake sawasawa kwa mujibu wa kumbukumbu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini iko hoja moja iliyozungumzia kuhusu ucheleweshaji wa fedha kwenda kwenye zile WMAs. Kwenye hoja hii tunauona ukweli, kwamba ni kweli kutokana na utaratibu uliopo kwa mujibu wa kanuni muda unaotumika unaweza kufanyiwa kazi na tukaweza kuupunguza ili WMAs zikaweza kupata ule mgao wao kwa wakati ambao ni pungufu ya ule wanaoupata hivi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ninaloweza kulizungumzia kwa sasa ni suala hili la mahusiano au mwingiliano baina ya wanyamapori na shughuli za kibinadamu, hasa mashamba lakini pia makazi ya wananchi, mahali ambapo wakati mwingine hutokea wanyama huharibu mazao mashambani lakini wakati mwingine hudhuru hata wananchi; na baadhi yao hujeruhiwa na pengine wengine hupoteza maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa ninachoweza kusema ni kwamba kwanza napokea pongezi kutoka kwa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Nsanzugwanko akiwa mmojawapo ambaye ameipongeza Serikali kupitia Wizara kwa kudhibiti ujangili ambao matokeo yake ni kuongezeka kwa idadi ya wanyamapori hasa tembo. Tuna idadi kubwa ya tembo sasa hivi ambao wanavinjari kwenye maeneo mbalimbali, wengine walikuja mpaka UDOM juzi. Hiyo ni mafanikio kwa upande mmoja, lakini kwa upande mwingine wa pili kuna changamoto zinazotokana na ongezeko hilo la wanyamapori hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kumekuwa kukizungumzwa jambo linalohusiana na vifuta jasho na vifuta machozi. Hapa napo pia kama Serikali kupitia Wizara tumefanya kazi kubwa kwa kulipa sehemu kubwa ya madeni yaliyodumu kwa muda mrefu ambayo kwa muda wa miaka mingi yalikuwa hayajalipwa bado. Hata hivyo, mpaka ninavyozungumza hivi sasa jumla ya fedha takribani shilingi bilioni 2.08 ambazo ni mkusanyiko wa madeni ya mpaka Disemba, 2016 yamelipwa kwa maana ya vifuta jasho na vifuta machozi. Hadi kufikia sasa deni la jumla tulilobaki nalo la vifuta jasho na vifuta machozi ni shilingi milioni 500 peke yake fedha ambazo kwa mujibu wa mpango tuliojiwekea na malengo tuliyojiwekea ndani ya mwaka wa fedha huu tulionao tunatarajia kumaliza kuzilipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema changamoto niliyonayo ni ya muda, lakini kwa ufupi nilitaka nizungumze hoja hizo mbili. Hata hivyo niseme ya mwisho inayohusiana na WMAs kwamba Taarifa ya Kambi ya Upinzani imezungumza kwa kina juu ya changamoto zilizopo kwenye WMAs. Kwa kweli baadhi ya hoja zilizotolewa lazima niseme ukweli kwamba ni hoja ambazo ni za msingi na zinapaswa kufanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini imekuwa bahati nzuri kwamba na sisi Serikali kwa upande wetu tarehe 9 Mei, 2017 tumekabidhi taarifa iliyofanya uchambuzi baada ya kufanya uchunguzi wa WMAs zote nchini kuangalia changamoto zao na changamoto kwa ujumla kwa mujibu wa sheria tuliyonayo na kanuni zake zinazoendesha WMAs na kwa hiyo tumeorodhesha baadhi ya hatua ambazo Serikali ni lazima ichukue ili kuweza kuboresha utendaji wa WMAs zote nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, WMAs zote nchini ambazo kwa ujumla wake zipo 38, kwa sababu ya madhumuni ya msingi ya kuanzisha WMAs ambayo kimsingi ni kuboresha usimamizi, ushirikishaji wa wananchi katika kusimamia uhifadhi nchini, Serikali itahakikisha kwamba tunaongeza mikakati zaidi, mbinu zaidi lakini pia kuwekeza zaidi ili kuweza kuhakikisha kwamba madhumuni hayo ambayo tumeyaainisha kwa mujibu wa sheria yanaweza kutekelezwa kwa manufaa ya uhifadhi nchini lakini kwa lengo la juu kabisa ni pamoja na kupata yale manufaa yanayotokana na shughuli za utalii nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu yale ambayo niliona nikikadiria kwa muda niliopewa yanaweza yakatosha kwa muda huu nimekwisha yakamilisha napenda kuishia hapa na ninaunga mkono hoja, ahsante sana.