Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Mussa Ramadhani Sima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kukushukuru. Namshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetuwezesha leo tuko hapa kujadili Bajeti hii ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya katika mchakato mzima wa kazi ambayo tumempatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Mawaziri; nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Elimu kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya. Hakuna ubishi kwamba Serikali inafanya kazi kubwa na mchango wake ni mkubwa sana kwenye eneo hili la elimu, hakuna ubishi kwenye hilo. Sina sababu ya kuelezea mafanikio ya elimu ambayo yapo na kila Mtanzania anajua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma kitabu hiki cha Bajeti ya Elimu. Nina Shule kongwe ya Sekondari ya Advance ya Mwenge. Katika ukarabati ambao Serikali inaufanya sasa hivi, lakini shule yangu ya Mwenge haipo kwenye ukarabati huo. Nataka nimweleze Mheshimiwa Waziri, shule hii mwaka 2016 ilifaulisha kwa asilimia 93, licha ya kwamba miundombinu hiyo hiyo tunaendelea nayo lakini Walimu wangu wanafanya kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mkoa wa Singida, ni Manispaa ya Singida Mjini pekee ambayo haina Shule ya Sekondari ya Kidato cha Tano na sita na ndiyo tunaitegemea Shule ya Sekondari ya Mwenge na ndiyo Shule ya Kitaifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nilieleze hili bayana ili Mheshimiwa Waziri aone umuhimu wa ukarabati wa shule hii kongwe ya Mwenge Sekondari. Kwa mazingira haya haya, sisi Singida Mjini tunalazimika sasa kuanza ujenzi wa shule nyingine za Advance ili kuweza kuwapunguzia mzigo wazazi na vijana ambao wanafaulu kwenda shule za sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukipewa fedha hii, ikikarabatiwa Shule hii ya Mwenge Sekondari itatusaidia katika mazingira ya kuanzisha hata Mwenge Day kwa sababu tunao uwezo huo. Yataongezwa madarasa, tunaanzisha advance ya Mwenge Day. Mheshimiwa Waziri nakuomba sana utupunguzie mzigo wazazi, nasi tuwe na kauli ya kuweza kuzungumza kwa wananchi waone umuhimu wa uwepo wa Advanced Level Singida Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule hii inao wazabuni mle ndani, wanadai zaidi ya shilingi milioni 500 na hao wazabuni ndio tunawategemea kutuchangia kwenye maabara na kwingine kwenye ujenzi kwa namna yoyote ile. Sasa Serikali lazima ione umuhimu wao, itusaidie na hao wazabuni wakilipwa wataendelea kutusaidia kwa kadri watakavyojaaliwa. Namwomba Mheshimiwa Waziri na hili nalo aliwekee umuhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Singida Mjini, Kata ambazo hazina Sekondari, wameanza kujenga na tayari Kata yangu moja ya Unyanga wamejenga Sekondari, inahitaji usajili Mheshimiwa Waziri. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri; tumeshakamilisha majengo ya maabara, naomba sana Shule hii ya Unyanga nayo iweze kupata usajili na tuweze kuwapa morale wazazi wa kuweza kuendelea kuchangia elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuzungumzie juu ya elimu bora (quality education). Hakuna ubishi kwamba Serikali inafanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha tunafikia malengo ya kuwa na elimu bora. Tayari tunayo elimu bila malipo, tayari kuna Responsibility Allowance inatolewa kwa ajili ya viongozi wetu, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Waratibu; hakuna ubishi kwenye hili. Katika mazingira haya haya, ziko changamoto ambazo hatuwezi kuziepuka ili kufikia malengo hayo. Hii ina-create gap kati ya wale viongozi kwa maana ya Walimu Wakuu, Waratibu wa Shule na Walimu wa kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu anayeingia darasani leo hakuna allowance yoyote anayoipata, lakini kiongozi anayemwongoza, anayo allowance. Serikali lazima ioneshe ni namna gani inam-promote na huyu Mwalimu anayeingia darasani ili tuweze kufikia quality education. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumzia kulipa madeni ya Walimu yasiyokuwa ya mishahara. Sasa hayo yaliyokuwa na mishahara ni nani aliyasababisha na ni nani ataenda kuwalipa? Naomba Serikali isibague, tunahitaji kulipa madeni yote na tuondokane na mpango huu wa Walimu kuendelea kudai, inashusha morale ya kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwalimu leo haendi likizo, fedha ya likizo haipo. Mwalimu anahamishwa, hapewi fedha ya uhamisho, haipo. Mwalimu anawezaje kufanya kazi fedha ya matibabu haipo? Naiomba Serikali ilete fedha kwa wakati Walimu waweze kwenda likizo, Mwalimu anayehamishwa apewe fedha, tuondokane na mpango huu wa madai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la madaraja. Habari ya madaraja miaka mitatu, sijui OPRAS, kila kitu kimeletwa hapa, lakini hakina msaada kwa Mwalimu. Walimu lazima wapandishwe madaraja kwa wakati. Hii ndiyo motisha yetu sisi Walimu wala hatuna kitu kingine. Serikali inapaswa izingatie. Kama tumeamua kwenye Open Performance Appraisal System, basi tuamue. Habari ya kukaa miaka mitatu na yenyewe haitimiii, jambo hili linatupa mzigo mkubwa sana. Naiomba Serikali iliangalie vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inapaswa iangalie teaching allowance, hatuwezi kuepuka. Huwezi kutoa allowance kwa Walimu hawa ambao ni viongozi, subordinate wao ukawaacha. Hatuwezi kuepuka hili! Serikali lazima ije na mpango huu, itusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Nidhamu; tunazungumzia elimu bora. Tumeunda Tume ya Utumishi ya Walimu hapa kwa Sheria Na. 25 ya Mwaka 2015, wameizungumza Kambi ya Upinzani pale. Ni ukweli usiofichika, tumefuta Mikoa, Halmashauri, tukapeleka Mamlaka ya Nidhamu hii Tume ya Utumishi kwenye Wilaya. Leo watumishi watatu kwenye Wilaya ambayo ina Halmashauri mbili, wameshindwa Walimu 1,200 watawezaje Walimu 3,000? Mamlaka ya Nidhamu haijapewa kipaumbele. Niiombe Serikali iliangalie hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo mamlaka, TSC kwenye Ofisi zao haina vitendea kazi, haina fedha, haina chochote. Sasa unatarajia inawezaje kusimamia jambo hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, tujue umuhimu wa quality education, tunahitaji kuwashirikisha wadau wote wakiwemo TSC. Kama inashindikana, tuwape semina Waratibu na Walimu Wakuu waweze kuifanya kazi hii kwa pamoja ili tuhakikishe kabisa kama tunazungumzia uadilifu kwenye utumishi uwe ni uadilifu ambao unawagusa watu wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TSC kama imeshindikana, tuirudishe sheria hapa ili tuweze kuirekebisha. Leo wale maafisa wa TSC wanafanya kazi, hawana vyeo. Haieleweki mishahara yao ikoje, wanafanyaje kazi hii? Naomba sana Serikali iliangalie jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni community participation. Serikali ina kila sababu ya kuwashirikisha wazazi na wananchi kuweza kushiriki kwenye hili. Baada ya kuanzisha elimu bila malipo, wengi wamerudi nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kila sababu ya kuanzisha programu maalum ambayo itainua ubora wa elimu. Training; kutoa mafunzo maalum kwa ajili ya wazazi. Tutoe mafunzo maalum kwenye Kamati za Shule, tutoe mafunzo maalum kwa Walimu; hii itatusaidia kufikia malengo ambayo tumeyakusudia ya kuwa na elimu bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu kwa kuiomba Serikali ione elimu ndiyo kila kitu. Tusipomwangalia Mwalimu huyu kama stakeholder namba moja, hatuwezi kufanikiwa malengo ya kufikia elimu bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja ya Serikali.