Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RIZIKI S. MNGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na ardhi kwa kutujalia sisi sote uhai, uzima na fursa ya kuwa hapa leo.
Pia nakushukuru wewe kwa kunipa fursa ya kuchangia mada ambayo iko mbele yetu leo hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nianze kwanza kwa kupongeza Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kwa taarifa yao nzuri kabisa na nipongeze Kambi Rasmi ya Upinzani kwa hotuba yao nzuri kabisa. Waingereza wanasema; they have said it all. Ni matarajio yangu kwamba Waziri atafanyia kazi document hizo mbili, kwa uadilifu ili Taifa letu lifike litakapofika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wala siachi kumshukuru wifi yangu Mheshimiwa Waziri kwa kazi anayoifanya na Naibu wako na timu yake yote. Pia nikupongeze kwa kuchagua partner ndiyo kwa sababu ulikwenda Kusini ungekwenda Kaskazini yale maneno leo usingeyasema hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli haya mambo kama alivyosema Mheshimiwa Mbatia yanaturudisha mle mle kila siku. Halafu tunafanya trial and errors hata kwenye elimu! Halafu Bunge kama imepanga ratiba vizuri, jana tumezungumzia mambo ya maji hapa, maji ni uhai, leo tunazungumzia elimu, elimu ni ufunguo wa maisha, lakini tunauchezea ufunguo huu, matokeo yake Taifa hili litaangamia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilikuwa najitahidi sana nipate fursa ya kuuliza swali la nyongeza wakati swali namba 199 likipatiwa majibu. Mimi muda wote nasema nchi hii tuna tatizo la ukosefu wa uadilifu, hatufanyi mambo kwa uadilifi. Mheshimiwa Mbatia kasema vizuri pale, hizi itikadi zetu za chama zitatupeleka pabaya. Ikisemwa hapa, ndiyoo, waliosema ndiyo wameshinda, waliosema sio wameshindwa halafu matokeo yake tunapitisha mambo mwisho wa yote yanaturudia wenyewe tunaangamia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ni mengi lakini nianze na hili la mambo ya vyuo kwa sababu limenigusa mimi binafsi. Hivi Wizara inapokuja kutuambia kuna vyuo visivyo na sifa lakini vilisajiliwa, vilisajiliwa vipi? Mimi nilikuwa Chuo cha Diplomasia, ni chuo cha Serikali, tulizungushwa miaka miwili na NACTE kwa sababu tu hatuna push door yaani mlango ule tunaambiwa mlemavu hawezi ku-access miaka miwili chuo cha Serikali kilichoanzishwa miaka karibu ishirini iliyopita. Vyuo binafsi hata mlango wenyewe haupo vinapata usajili, halafu hapa wanakuja kutuambia kuna vyuo visivyo na sifa vilisajiliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama vile haitoshi wanatumbia vitabu vyenye maudhui siyo vipo, hilo ni tatizo la uadilifu. Tunaona kwenye tv zetu hapa programu za kijinga kabisa, watoto wanazini pale mbele ya screen, lakini TCRA kuna Kamati ya Maudhui hawalioni hili? Tatizo ni uadilifu. Tunawaweka watu siyo kwenye taasisi ndizo, tubadilike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, NECTA na vyeti fake. Kwenye kikao cha mwaka jana hapa nilisema, mimi nimepoteza cheti changu cha form four na form six, nakwenda NECTA naambiwa nenda kule ulikosoma mwalimu wako mkuu akuandikie barua. Nikawaambia mimi nimetoka Kisutu mwaka 1977, huu mwaka 2011 Mwalimu Mkuu gani wa Kisutu ananijua mimi lakini wewe NECTA ndiyo uliyenipa mimi namba ya mtihani na ndiye unayejua kituo changu cha mtihani, you stand a better position and chance ya kuni-clear mimi kuliko huyo mwalimu. Sasa hapa mmeanzisha hili zoezi wenyewe mnaliita uhakiki wa vyeti fake, kisiasa kabisa watu wanaathirika, wengine wala hawahusiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niwaambie moja tu. Mimi sasa hivi naitwa Riziki Shahari Mngwali lakini hili nimelipata na nimelisajili rasmi kwa sababu nimeenda kutafuta deed poll. Watanzania wangapi wanajua hilo? Mimi miaka yangu yote naitwa Riziki Shahari, majina mawili tu. Hata nilipokwenda chuo kikuu kuomba niwe admitted kwa ajili ya programu nyingine nikaambiwa hilo jina la tatu hatulikubali kwa sababu ulisoma hapa digrii ya kwanza kwa majina mawili, tutakusajili tena kwa majina hayo hayo mawili. Sasa hivi vyuo vyetu vingesaidia hivi kuliko kuwaadhiri na kuwatesa watu bila sababu ya msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika lile swali nililolisema la jana namba 199 kulikuwa na issue ya wenyewe watalaam wanaitwa LOI - the Language of Instruction, imesemewa mpaka na programu maalum ilikuwepo chuo kikuu pale. Profesa Koro wame-research na wameandika bado tunali- discuss hapa. Jana likaja hapa linasemwa na leo hivyo hivyo ndiyo tunaona vitabu hapa vinakwenda kushoto kulia, kulia kushoto, pembeni kati, tatizo hatujui tunataka nini. Basi hata kuamua tu lugha gani tutumie kufundishia watoto wetu kwenye ngazi zote za elimu yetu lakini pia tuweke msisitizo wa kuwafundisha foreign languages not only English, French, Spanish, Arabic na bado watoto watafaulu watatoka na elimu nzuri na bado watakuwa na qualification za foreign languages tunazozitaka, tujipange tu vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la hizi programu maalum kwenye ukurasa 77, 78, P4R, TESP na mengine, nitoe tahadhari ile ile ambayo nilishawahi kusema kwingine this is donor dependence ya kutisha kabisa. These are very special programs (programu maalum) na ni nzuri kwa kutengeneza mfumo wetu wa elimu, lakini zinafadhiliwa kwa sehemu kubwa kabisa kama siyo sehemu yote. Ni kama vile wewe ili umlee mtoto wako mzuri atoke jirani huku aje akuambie mwanao akiwa na afya nitakupa pesa, mwanao akisoma vizuri nitakununulia gauni, mambo gani haya? Hebu haya mambo mengine tujiwekee sisi wenyewe tuone tunakwenda wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisije nikaishiwa muda bila ya kusema suala la motisha kwa walimu na baadaye tutali- discuss kwa watumishi wetu wote wa umma. Jamani mwalimu anafanyiwa stihizai, anapandishwa cheo mwezi huu analipwa mshahara, mwezi unaofuata halipwi, kimya, hapelekewi barua wala hajulishwi chochote, hivi tunategemea hawa watu wafanye kazi namna gani? Mwalimu mnamtoa Kigoma mnampeleka akafundishe Mafia, hapewi nauli wala stahiki zake nyingine, mnatarajia atafanyaje kazi, hata kweli atakuwa na moyo wa kufundisha watu huyu? Watu wengine mnazungumzia mazingira magumu, wana allowance nyingine hazina hata na majina lakini walimu wanasahaulika. Nani awatetee hawa walimu na siyo kwamba hawana watetezi, watetezi wapo wanasema hapa lakini nani anajali kushughulikia hayo ambayo yanasemwa kwa ajili ya mustakabali wa nchi yetu hii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani Mheshimiwa wifi hebu badilikeni. Kweli tunakuona mfanyaji kazi, mara hii tunazo kweli timu za akina mama, mmekaa kwenye Wizara, Mheshimiwa Ummy yuko pale na wewe na Naibu wako mmewekwa Wizara moja hebu fanyeni kazi tuone kweli wanawake mtaleta mabadiliko ambayo kweli sisi tutakaa tujivunie. Elimu tukiichezea, Taifa tumelichezea na kuliangamiza. Jamani tubadilike na tufanye kazi inavyotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Waziri Kivuli amezungumzia suala la wataalam wa TEHAMA na mimi pia niliseme. Mimi nilishtuka kwamba eti tunaenda kuazima wataalam kwingine waje watutengenezee programu yetu sisi, mimi nikasema what a shame! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa kwenye Tume ya Warioba, tulipata vijana wa IT mashallah walitengeneza programu pale ya kurekodi zile taarifa zote, mikutano tunayofanya, Hansard tulichukua wataalam wa hapa Bungeni, kulitokea programu mpaka siku moja Waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa Salim Ahmed Salim, mwenyewe alikuwa ananiita jirani maana ofisi zetu zilikuwa floor moja, akaniambia jirani hawa watoto ni wa Tanzania? Nikamwambia tena mmoja ni Mpemba, walitengeneza programu mpaka mtu unashangaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo tunaenda kuwatafuta watu wa Rwanda, sijui na watu gani. Hivi tutawasifia lini watoto wetu, tuta-recognize lini sifa zao na tutawa-motivate vipi watoto hawa? Watoto excellent kabisa wengine wame-graduate hapo St. Joseph, hapo hapo mlipopafunga mwaka jana, watoto wazuri, watoto ambao TTCL wanawagombea. Ukipeleka mtoto kufanya field TTCL wanamuuliza wewe ni wa St. Joseph au wa chuo gani, kwa sababu wanajua watoto wale wamefundishwa sio elimu ya darasani lakini hands on, ile competence base ni kweli wamejifunza, lakini yote haya hatuyaangalii tunazidi kuwakatisha tamaa watoto wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nilisema hapa tunahitaji an integrated process, budgeting, planning and even understanding. Tukiwa na uelewa wa pamoja tunapanga mambo yetu pamoja, migongano gongano hii haitakuwepo tatizo kila kipande kinatengenezwa peke yake halafu kinakuja kulazimishwa kukaa kwenye kipande kingine. Kwa namna hii hatutafika na kila siku tutakuwa tunaanza palepale kwa sababu mambo yetu tunayapanga kipande kipande halafu tunakuja kulazimisha kuwa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.