Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Kiteto Zawadi Koshuma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naomba nitumie nafasi hii kurekebisha jina langu naitwa Mheshimiwa Koshuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunipa nafasi ili na mimi niweze kuendelea kutoa michango yangu katika Bunge lako Tukufu hususan katika Wizara ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kuhusiana na suala la ubora wa elimu. Nimewasikiliza Waheshimiwa Wabunge wengi sana wamekuwa wakichangia kuhusiana na ubora wa elimu kila mtu kwa kadri ambavyo ameweza na ni jambo zuri sana kwani kazi yetu sisi Wabunge ni kuishauri Serikali ili kuona kwamba watoto wetu wanapata elimu iliyo bora na sio bora elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende moja kwa moja upande wa vitabu na vitabu hivi vimegaiwa sasa kwa uwiano ambao mimi nauona kabisa kwamba hatuelekei kuzuri. Ukiangalia katika Mkoa wa Mwanza, Wilaya ya Ilemela, kwa mfano, darasa la pili wanafunzi ni 71,000 lakini vitabu ambavyo vimepelekwa katika Wilaya ya Ilemela ni vitabu 10,465. Wilaya ya Magu idadi ya wanafunzi wa darasa la pili ni 100,000 lakini vitabu ambavyo vimepelekwa ni 12,893 na hivyo ni vitabu vya hisabati. Wilaya ya Sengerema wako wanafunzi 151,000 na vitabu ambavyo vimepelekwa ni 13,965 na hivyo hivyo na Wilaya zingine. Waheshimiwa Wabunge kama mtapenda kuendana na mimi ni ukurasa wa 152 na 153.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ugawaji huu wa vitabu siamini kabisa kwamba wanafunzi wataweza kupata elimu iliyo bora. Kwa mfano, kwenye somo hili la hesabu vitabu ambavyo vimepelekwa ukiangalia idadi yake ni vichache ukilinganisha na idadi ya wanafunzi waliopo darasani wa darasa la pili. Hivyo, kwa mahesabu ya haraka haraka utakuta kitabu kimoja wana-share wanafunzi hata 30 hadi 40.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali kujaribu kuwaeleza wazazi ukweli. Kutokana na hii Sera ya Elimu Bure ya mwaka 2016 wazazi wengi sasa wamekaa wanasema kwamba Serikali inatoa elimu bure wamesahau kwamba wao pia wanaweza wakachangia katika upatikanaji wa elimu nzuri ya watoto wao. Naomba niwashauri wazazi wote nchini kwamba na wao pia waweze kuisaidia Serikali, lakini pia na Serikali itusaidie sisi Wabunge kwa kupeleka elimu kwa wazazi kupitia Walimu Wakuu na Bodi za Shule wawasaidie kuwaeleza wazazi na wao pia wasaidie kuchangia. Kwani wazazi wakichangia vitabu watasaidia watoto walau kila mmoja kuwa na kitabu chake kama inawezekana au kitabu kimoja kutumiwa na wanafunzi hata watatu hadi watano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia shule nyingi ambazo zinafanya vizuri hapa nchini Tanzania hususan shule za msingi katika elimu ya darasa la kwanza mpaka la saba ni shule za private lakini shule za Serikali zimekuwa ziki-lag behind. Kuna sababu nyingi tu ambazo zinazosababisha shule za Serikali kutokufanya vizuri zikizidiwa na shule zile za private.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kabisa wazi kwamba mimi ni mmiliki wa shule za private, lakini ukiangalia katika shule za private tunaletewa miongozo mingi sana na mnaambiwa kitabu kimoja kitumiwe na wanafunzi watatu. Kwa kweli shule za private zimekuwa zikijitahidi sana kuzingatia hilo na ndiyo maana wanaofaulu kwa ufaulu mkubwa wanatoka katika shule za private. Naomba Serikali sasa iweke mkazo katika shule zetu, ndio tumetoa elimu bure lakini sasa kama vitabu vinakuwa ni vichache wanafunzi hawawezi kupata elimu iliyo bora wanatapa bora elimu na kuondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni upungufu wa madarasa na miundombinu mingine. Ukiangalia mwaka kwa 2015/2016 uandikishwaji wa wanafunzi mashuleni uliongezeka kwa asilimia kubwa sana. Hiyo ni kutokana na sera nzuri ambayo imetengenezwa na Serikali yetu, Sera ya Elimu Bure. Sasa miundombinu bado ipo ile ile ambapo zamani wazazi walikuwa wanaogopa kupeleka watoto shuleni, madarasa ni machache, wanafunzi hawatoshei kwenye darasa yaani unakuta darasa moja wanakaa wanafunzi zaidi ya 100, mwalimu ni mmoja na wengine bado wanakaa chini. Kuna shule ambazo mpaka leo bado wanafunzi wanakaa chini. Pamoja na kwamba Mheshimiwa Rais amesisitiza suala la kuwa na madawati na akasema Wakuu wa Wilaya ambao hawatawajibika katika shule zao kuhakikisha kwamba madawati yanapatikana watafukuzwa kazi lakini bado kuna shule zingine bado wanafunzi wanakaa chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote mimi nachosema na mawazo yangu ambayo nafikiria, ni afadhali wanafunzi wakae chini, lakini wale wanafunzi wakapata walimu wa kuwafundisha na madarasa yakatosha. Walau basi tufanye kama ambavyo shule za private zinafanya, unakuta darasa moja la kwanza linakuwa na wanafunzi labda 45 kwenye shule za private na hiyo yote ni kutokana na kwamba tunafuata vizuri miongozo inayotolewa na Serikali kwa shule za private lakini kwenye shule za Serikali unakuta darasa moja wapo wanafunzi 100 hadi 120.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imejitokeza sehemu nyingi sana kama ningesema nitoe mifano nina mifano mingi hata kwa shule za mjini. Kwa mfano, kuna shule moja ipo pale Mwanza, Wilaya ya Ilemela inaitwa shule ya Isenga, darasa la kwanza mpaka la tatu wanafunzi 120 darasani. Naomba Serikali ijitahidi sana kuweza kuwekeza katika kuongeza madarasa ili wanafunzi wawe wachache na hata kama mwalimu atakuwa mmoja katika darasa ambalo lina wanafunzi wachache tunaamini kabisa wanafunzi hao wataweza kujua kusoma, kuandika na kuhesabu. Kwa sababu tunaona unapoweka idadi ndogo ya wanafunzi na mwalimu akawa anaweza kumpitia kila mwanafunzi moja mmoja darasani basi wanafunzi hao wataondoka pale wakijua kusoma, kuandika na kuhesabu na hivyo kuelekea kwenye upatikanaji wa elimu bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu bado utaendelea kwenye upatikanaji wa elimu bora na sasa nizungumzie kuhusu motisha za walimu. Walimu wanapokosa motisha kwa kweli inawa-demoralize. Unakuta walimu wanakuwa hawana moyo wa kufundisha kwa sababu hawapati motisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Serikali ilikuja na mpango mzuri sana wa Big Results Now na uliwasaidia walimu wakawa wanafanya kazi kwa kujitoa wakiamini kwamba mwisho wa siku watapewa motisha. Sasa mpango huu umeenda unalegalega tu. Naomba Wizara ya Elimu warudishe mpango huu wa Big Results Now na kuuwekea mkazo ili uweze kusaidia walimu kufundisha wanafunzi vizuri na hatimaye kutoa elimu iliyo bora ili waweze kupewa motisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la hardship allowance. Wameongea Waheshimiwa wengi sana kuhusiana na maslahi ya walimu, unakuta mwalimu anatolewa kituo kimoja kupelekwa kituo kingine na anapelekwa kule ni kijijini, lakini anapofika kule anakuta hakuna nyumba, kama kuna nyumba hakuna umeme, hakuna choo yaani unakuta mazingira ni magumu kiasi kwamba huyu mwalimu hawezi kuwa na moyo hata wa kuingia darasani. Inampasa huyu mwalimu asubuhi akiamka atume wanafunzi kwenda kuteka maji kwa ajili yake. Hivi kweli tunategemea hapo tutapata wanafunzi ambao wanajua kusoma na kuandika, tutawapata wapi wakati wanafunzi hao wanatumika kwenda kuchota maji? Naomba sasa Serikali isaidie kutoa hardship allowance kwa walimu ambao wanapelekwa katika mazingira magumu ili waweze kupata moyo wa kufundisha wanafunzi wetu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la kubadilika kwa mitaala, hiyo yote pia inapelekea kwenye kupata elimu iliyo bora. Mitaala imekuwa ikibadilika mara kwa mara, anapokuja Waziri huyu anabadilisha mfumo wa elimu na mitaala, anapokuja Waziri mwingine anabadilisha mfumo wa elimu na mitaala, suala hili linawachanganya wanafunzi. Siyo tu kuwachanganya wanafunzi bali wananchi pia wanabaki wamechanganyikiwa hawajielewi hivi wafuate mfumo au mtaala upi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia mitaala inapokuwa inabadilika vitabu pia inabidi vibadilishwe. Kwa hiyo, naiomba Serikali inapobadilisha mitaala vitabu viende kwa haraka sana. Kwa mfano, mwaka huu vitabu vimechelewa sana kwenda ndio kwanza vimetoka juzi tu vimesambazwa, vimechelewa sana tayari walimu walikuwa wanatumia vitabu vya zamani, wanashindwa jinsi ya wakuwafundisha wanafunzi... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Koshuma.