Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Goodluck Asaph Mlinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mweyekiti, ahsante sana. Kwanza kwa namna ya pekee naomba kutoa pole kwa Mbunge mwenzangu, jirani yangu Mheshimiwa Hadji Mponda kwa kufiwa na mpiga kura wake, Mkuu wa Mkoa wa zamani wa Mkoa wa Ruvuma Mheshimiwa Mwambungu. Pili, naomba kutoa shukurani za pekee kwa Baba Askofu Agapitus Ndorobo wa Dayosisi ya Mahenge kwa shule zake za Regina Mundi, Kasita Seminary, St. Agness na St. Joseph zimekuwa Kinara kwa kuitangaza Ulanga kwa ufaulu. Kwa hiyo, mnaposikia Kasita Seminary kuna watu wanaisikia inafaulisha lakini hawajui kama ipo Ulanga kwa Mlinga.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia kuipandisha elimu ni pamoja na barabara kwa Majimbo yetu ambayo yana mazingira magumu kama Jimbo la Ulanga. Sasa hivi kuna maeneo hayafikiki kabisa. Kwa mfano, kuna eneo linaitwa Isaka hata baiskeli haiendi na ni zaidi ya kilometa 25, kuna eneo linaitwa Lyandu hakufikiki, kuna eneo linaitwa Majengo kilometa zaidi ya 27 hata baiskeli haifiki, kama Waziri wa barabara upo na unanisikia, naomba uli- note hilo kuwa kinachochangia elimu katika Wilaya ya Ulanga kushuka ni pamoja na miundombinu mibovu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa shukrani na kuwapongeza Maafisa Utumishi wa Wilaya ya Ulanga. Mheshimiwa Spika hapa alilipongeza Bunge kwenye suala la vyeti fake kuwa hakuna hata mtu mmoja nami naomba niwapongeze Maafisa Utumishi wa Wilaya ya Ulanga kwani Mtumishi mmoja tu ndiye aliyepatikana kwenye suala la vyeti fake na bahati nzuri alilala mbele kabla Rais hajatoa agizo kuwa hawa watu wafukuzwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine katika Jimbo langu la Ulanga wananchi wamejitolea kuna maeneo wamejenga shule, iko shule ya Mikochi, iko shule ya Kipingo na shule ya Mbenja katika kata ya Ilagua lakini suala zito limekuwa kwenye usajili. Wazazi wamejitolea, wajenga majengo, wametafuta walimu, wanawalipa wenyewe Serikali suala la kuisajili wanasema eneo hilo mpaka wapate kibali cha maliasili yaani Serikali hiyo hiyo, Mawaziri hao hao, wameteuliwa na mtu huyo huyo mmoja, lakini kutoka ofisi moja kwenda nyingine inachukua miaka mitatu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba unisaidie unisajilie shule zangu ili tuweze kupata walimu wa Serikali na tuweze kupata vituo vya kufanyia mitihani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu lingine ni madai ya walimu, hivi naomba niulize, nilishawahi kumuuliza ofisa mmoja mkubwa Wizara ya Elimu akasema tatizo zinalochelewesha madai ya walimu kwa sababu walimu wapo wengi. Nikamuuliza walimu wengi kwa sababu sisi tunazaa sana? Tungekuwa na watoto wachache walimu

wangekuwepo wengi? Kwa nini tunawanyanyapaa? Wabunge leo hii maslahi yetu yakicheleweshwa macho yanatutoka na tunaibana Serikali na wanawahi kututekelezea, kwa nini kwa walimu iwe tatizo hili na wakati Walimu ndiyo waliotufundisha? Huwezi kuoa bila kuandika barua ya uchumba, lakini walimu ndiyo waliotuwezesha sasa hivi tunawasahau. Humu Wabunge wengine ni maprofesa, wengine madaktari kwa sababu ya hawa walimu, lakini inapofika suala la maslahi yao tunaongea, kwenye kuibana Serikali hatuibani, inaishia kupiga makofi tu yamekwisha. Naomba kwa uchungu kabisa nitajitolea kuwa Balozi wa Walimu katika Bunge hili, yaani sitoki mpaka masuala ya walimu yaeleweke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano suala la nauli, walimu wanaenda likizo nadhani kwa miaka miwili mara moja na hapewi nauli, lakini Maofisa wengine kila mwaka wanaenda likizo na wanapewa nauli, tena nauli zenyewe ni ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vyeo katika Jimbo la Ulanga kuna walimu miaka 15 kafanya kazi hajapandishwa daraja ukiuliza kwa nini? Wanasema hatujapata bajeti, hivi wakati mnamuajiri mlikuwa hamjui kama atatakiwa apandishwe cheo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la ukaguzi; kinachochangia Wilaya ya Ulanga elimu kushuka Wakaguzi hawana gari, kwanza ofisi yenyewe ukiiona huwezi kutamani, hawana usafiri, Jimbo lina mazingira magumu mnategemea wataendaje! Mheshimiwa Waziri naomba unisaidie gari Wakaguzi wa Elimu wa Ulanga ili waweze kwenda kuzikagua shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kuna chama kimoja kinaitwa CWT (Chama cha Walimu), naomba nitumie kauli ambayo siyo nzuri, hiki chama kimekuwa kinawakandamiza walimu; kwa sababu mwalimu anapoajiriwa anatakiwa achangie humu kwa lazima, kuna Walimu Ulanga hawajui hata CWT ndiyo nini, anaiona kwenye salary slip kuwa amekatwa hela lakini hajawahi kupata chochote na hajawahi kusaidiwa chochote na hiki chama. Nilitoa pendekezo hapa mwaka jana kuwa walimu wajiunge kwa hiari kwenye huu mfuko ilia one kama una msaada ndiyo ajiunge, kama hauna masaada asijiunge. Wizara mnaliona, mnalifhamu na mnaliachia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI nadhani upo, kuna shule inaitwa Kwiro sekondari nilisoma hapa ndipo nilipoanzia form one, hii shule ina wanafunzi 520 wa sayansi lakini haina mwalimu wa hesabu, hawa ni wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita hivi mtu anasomaje sayansi bila kusoma hesabu? Alipangiwa mwalimu mmoja kwenda hapo na mpaka leo hii haja-report, kwa hiyo, hawa wanafunzi wanasoma lakini somo la hesabu hawasomi, sasa watafanyaje mtihani wa kidato cha sita hawana mwalimu wa hesabu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shule ya sekondari hii imechukua jina la Mama yangu Waziri mwenzenu wa zamani, Celina Kombani. Hii shule inatarajia kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita lakini haina bwalo la chakula na haina jiko na nimeshaandika barua kwako, naomba unisaidie hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la VETA; Mheshimiwa mmoja hapa alichangia kuwa wanafunzi wanaofeli waende VETA, naomba nimpe taarifa kuwa VETA siyo pango la vilaza, wako watu wana akili zao kule. Mheshimiwa Waziri, VETA walikuja Ulanga, tuliwapa eneo, walilikagua na walikubali lakini sasa hivi wameingia mitini, naomba tulifuatilie suala hili ili waje kujenga hiki chuo na eneo tulishawapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la mwisho ni suala la mikopo ya elimu ya juu. Tumeongeza asilimia kufikia 15, Mheshimiwa Waziri naomba ufanye assessment, nenda kaangalie hiki kilio cha wafanyakazi hii asilimia 15 inavyowaumiza, tuwaonee huruma. Mimi naomba tuleteile sheria hapa Bungeni ili tufanye marekebisho, kwa sababu

wote ni mashahidi mfanyakazi yoyote anapopata ajira cha kwanza kwenda kuchukua mkopo na anachukua mkopo mpaka kwenye cealing ya mshahara wake. Mkopo wa Bodi ya Mikopo walikuwa wanachukua asilimia nane sasa hivi asilimia 15, hebu fikirieni maisha yakoje huko uswahilini na sasa hivi hakuna posho zozote sasa hivi ninyi wenyewe mnajua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho kabisa, Serikali imesema kuwa haitoajiri tena walimu wa masomo ya arts; Mheshimiwa Waziri Serikali hii ndiyo ilikuwa inasimamia hawa wanafunzi waende wakasomee ualimu masomo ya arts leo hii inasema hawawaajiri, sasa hawa watu watakwenda wapi? Watakwenda kuajiriwa sehemu gani?

Kwa hiyo, naomba mlifikirie upya, ninyi ndiyo muwatafutie alternative “B” kuwa watafanyaje. Wataendelea kukaa uswahili hivi na wameshasoma halafu sasa hivi mnawaambia lazima walipe mikopo baada ya muda fulani, hizi hela wanatoa wapi? Wakiwa wakabaji sheria zinakuwa kali mtaani. Huo ndiyo mchango wangu mdogo kwa leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.