Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwa dakika tano hizo katika Wizara hiyo ya Elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niungane na Watanzania wote kutoa pole nyingi sana kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha kufuatia ajali ambayo imechukua maisha ya watoto wetu, walimu pamoja na dereva iliyotokea Wilaya ya Karatu Wilaya ambayo ninatokea, Mkoa wa Arusha ambao ninauwakilisha. Poleni sana na Mwenyezi Mungu azidi kuwapa nguvu familia. Pia nitoe pole kwa wazee wetu hawa ambao wametangulia mbele ya haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mchango mfupi kuhusiana na Wizara hii kwa sababu pia ya muda. Taifa lolote ambalo linachezea elimu ni Taifa ambalo linaenda kuangamia na Taifa ambalo linaenda kupotea. Nasema hivi kwa sababu kumekuwa na utamaduni kila Waziri anayekuja kwenye Wizara hii anakuja na style yake ambayo ama anafikiri inaenda kuboresha elimu au inaenda kuangamiza elimu kabisa.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mama Ndalichako umeingia hapa wewe, wewe ni mtaalam, hujawahi kuwa mwanasiasa, tunaamini utaenda kuweka mifumo thabiti, mifumo itakayoboresha elimu kwa watoto wetu, mifumo ambayo itawaandaa watoto wetu kuwa na Taifa ambalo litaendelea kuwa Taifa kama ambavyo nchi nyingine tumeona. Tunategemea utaenda kuweka mifumo ambayo hata wewe ukiondoka kesho, Waziri yeyote atakayekuja hataenda tena kucheza na elimu ya watoto na hataweza kwenda kucheza na elimu ya Watanzania. Kwa hiyo, Mheshimiwa Ndalichako tunategemea utaenda kuweka hiyo mifumo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie kuhusu mfumo wa mpango wa elimu bure. Serikali imekuwa ikitamba sana kuhusu suala la elimu bure na imesema imefanikiwa. Ukweli sio sahihi. Huwezi kuangalia mafanikio ya elimu bure kwa kuangalia idadi ya watoto waliojiandikisha, ndiyo mmekuwa mkisema hivyo. Idadi ya watoto waliojiandikisha kuanza darasa la kwanza kweli inaongeza, lakini hiyo sababu pekee ya kutamba ya kujigamba na kusema eti elimu bure imekuwa na matokeo chanya kwa Watanzania siyo kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna changamoto nyingi, kuna changamoto nyingi sana katika suala zima la elimu katika nchi hii, ambapo pia taarifa ya Kamati imeonesha. Kwa hiyo, tunategemea ama mje na mfumo mwingine wa kusema kabisa, ama mmeshindwa hiyo elimu bure kutoa, ambayo mnaita elimu bure kwa sababu hizo changamoto au muondoe hilo neno au muwaambie sasa Watanzania kwamba tulisema elimu bure, lakini kuna changamoto, tunahitaji kuwa-engage Watanzania na wao katika suala zima la kuondoa changamoto za elimu hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu wanafunzi waliopata mimba na kurudishwa mashuleni. Hatuelewi ni kwa nini kuna kigugumizi kuhusiana na watoto wa kike waliopata mimba wananyimwa kurudi shuleni. Mheshimiwa Kakunda amechangia hapa asubuhi, yeye ni mtaalamu mzuri sana, amekaa kwenye system muda mrefu anapinga hili jambo. Hivi, watoto wanapata mimba, hawarudi shuleni, hivi tunazidi kuondoa ujinga au tunazidi kuzalisha ujinga? Kwa sababu hawa watoto wanapata mimba wapo wanaobakwa, wapo ambao kweli inawezekana mazingira yanawalazimisha, wako wengine ambao tu ni watundu wanakuwa kwenye hiyo hali wanapata mimba. Hivi kupata mimba na kuzaa ni dhambi? Wavulana walowapa mimba wanaendelea, hawa watoto wa kike waliopata mimba wanarudi majumbani. Tunaendelea kuzalisha ujinga kwa Watanzania, na hatujui ni kwa nini Serikali mnapata kigugumizi. Mbona wenzetu wa Zanzibar wanaendelea hawa watoto wakipata mimba? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bunge la Kumi nilikuwa na Kamati ya Huduma za Jamii tulikuwa tunasimamia Wizara ya Elimu tulienda Zambia, wanarudi mashuleni watoto hawa. Kwa nini kwa Tanzania? Kwa nini mnapata kigugumizi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wewe ni mama, wewe ni mwanamke mwenzetu, tuwaonee huruma watoto wetu wa kike ambao wako kule vijijini wanapata mimba, wanarudishwa majumbani, hawawezi kuendelea na shule, halafu watoto wa kiume waliowapa mimba wao wanaendelea na shule.
Waheshimiwa Wabunge wanawake, Waheshimiwa Wabunge, Wajumbe wa TWPG, Wizara hii bajeti yao isipite mpaka tupate kauli ya Serikali ni lini wataruhusu watoto waliopata mimba waweze kurudi mashuleni. Kwa hiyo, tunategemea Mheshimiwa Waziri utakuja na majibu siku unahitimisha hoja yako na ujiandae kwa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru.