Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Peter Joseph Serukamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Elimu. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge, tunakwenda kuandika historia kwamba na sisi tunashiriki mazishi ya kuua elimu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya nina vitabu hapa na namshukuru sana Mheshimiwa Biteko aliyeanza kulisema hili jambo. Waheshimiwa Wabunge ukiangalia vitabu hivi kwa namna yoyote ile huu ni wizi. Kwa namna yoyote ile hii ni kuua kizazi cha kesho, lakini vitabu hivi vimepitiwa na vimewekewa ithibati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi hawa watu wa Tanzania Institute of Education, naomba leo niliombe Bunge hili tuazimie wote walioandika vitabu hivi waende gerezani, haiwezekani! Vitabu hivi wamekaa watu ma-specialist wamevitunga, wameviangalia, wanavipitisha, vinasomwa na watoto wetu, haiwezekani. Waheshimiwa Wabunge ukichukua vitabu hivi, nitawasomea sentensi chache, ‘which is wrong between a pen and a ruler’, 21st Century? Huku ndani kila unakoenda unajiuliza ni Tanzania hii kweli? Haiwezekani Waheshimiwa Wabunge. Nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge suala la vitabu hivi tusilifanyie mzaha hata kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sehemu hapa wanasema, ‘When, End and How”. Hata neno ‘and’ hawawezi kuandika na ni specialists walikaa wamepitisha vitabu hivi, vina makosa. Hiki kitabu cha Kingereza, hiki ni kitabu cha Jiografia. Kuna sehemu carbon dioxide imeandikwa canon dioxide, kweli jamani! Hapa kuna kitabu, standards wenyewe mmesaini, lazima kiwe na gundi, hapa wamebandika tu stepple pin na hiki chenyewe cha kujifunza na kusoma hakina hata ithibati, kina mhuri tu wa Tanzania Institute of Education. Waheshimiwa Wabunge, ukisoma makosa hapa ni mengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, makosa haya ni aidha hawa walioandika hivi vitabu na waliovipitisha, nadhani watakuwemo kwenye orodha ya watu wa vyeti fake. Kama hawa hawamo, then tuna tatizo kubwa zaidi. Maana haiwezekani mmekaa na mnajua Waheshimiwa Wabunge zimetumiwa shilingi ngapi, shilingi bilioni 108. Shilingi bilioni 108 za Watanzania zimeandika vitabu ambavyo havisomeki. Hivi siyo vitabu! Halafu mnataka Wabunge tukae hapa tushangilie kama mambo ni mazuri, hili lazima tulikatae. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ukishakosea kwenye kitabu tunaua generation ya kesho unless tumeamua kuwa wabinafsi. Naomba sana tuache ubinafsi, tuombe kwanza vitabu hivi viondolewe kwenye circulation ya Wizara ya Elimu. Pili, naomba sana, watu wote walioshughulika na vitabu hivi lazima waende kwenye mkondo wa sheria. La tatu, tuombe Waziri wa Elimu anapokuja hapa, hawa watu lazima walipe shilingi bilioni 108 za Watanzania, haiwezekani. Haya yanatokea kwa sababu hatujali na inawezekana kwa sababu watoto wetu hawasomi huko ndiyo maana hatuoni kama ni jambo kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini liko suala hapa linasemwa la shule za binafsi. Nataka niwarudishwe kwenye historia, siku za nyuma miaka ya 80, 90 shule za sekondari za Serikali hazikuwepo zilikuwa chache hawa watu wa private wakaja wakatoa huduma kwa Watanzania hawa. Leo tumejenga Shule za Kata, haiwezekani sasa zile hazifai tuzitupe kwamba wale ni wafanyabiashara tuachane nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono tuanzishe Regulatory Authority ya kusimamia standard za elimu Tanzania ili kama shule iwe na wanafunzi 45 ndiyo standard, iwe ya Serikali iwe ya private ambayo imezidisha ichukuliwe hatua. Maana sasa zinazochukuliwa hatua ni za private, zile za Serikali hawana vyoo ni sawa, hawana Walimu ni sawa, wanafunzi wako 300 ni sawa, haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nasema lazima tufike sehemu tutoe huduma lakini pia naomba shule hizi za private tuziangalie kwa jicho lingine. Jamani, watu hawa kwanza wanatoa service kwa Watanzania, lakini pia wanaajiri watu na wanalipa kodi. Kwa hiyo, tutengeneze utaratibu tuwapunguzie mzigo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni suala la kurudia darasa. Mimi nimesoma seminari wakati tunaanza tulikuwa wanafunzi 51, by the time tunafika form three tumebakia 28. Wengine wanabaki huko nyuma kwa sababu pale seminari ili upande darasa ni lazima upate wastani wa 50. Wakati tunafanya mtihani wa form two ili upande form three Serikali ilikuwa wastani ni D, seminari waliweka wastani ni C, wameamua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha msingi ambacho tumesema kwenye Kamati, Serikali muweke standards ili mtoto anayekwenda shule ya private anapoanza tu ile form one aambiwe kwamba hapa usipopata marks hizi hupandi darasa, mzazi akikubali amechukua choice yake yeye mzazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kweli mnataka liwe Taifa ambalo watoto wanasoma moja kwa moja mpaka form four? Wakipata division four tunasema mwaka huu kufaulu ni kwingi sana lakini ukifanya analysis ya kufaulu ni division four. Hili Taifa ni letu wote, naombeni Waheshimiwa Wabunge tulisimamie, tusiache kuna watu pale Wizara ya Elimu wanafanya wanayoyataka sisi tunanyamaza, haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana Wizara ya Elimu ukienda kila mtu anatoa circular. Zinakuja circular nyingine hata Waziri hajui, lakini circular ilishakwenda. Ukienda TAMISEMI wanafanya wanachotaka, kila mtu anafanya anachotaka, hapana. Jamani Taifa lolote ili lionekane limeendelea ni elimu ya watu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naombeni sana tuzisimamie vizuri lakini tupunguze utitiri wa kodi kwenye shule za private, hawa wanatoa huduma, wanasomesha Watanzania. Kazi hii wamefanya kwa muda mrefu, haiwezekani leo ghafla tuwaache, wameajiri watu. Naombeni sana Serikali, nendeni mkakae muwaite watoa huduma hawa muongee mkubaliane vitu vya kufanya vile ambavyo Serikali inaweza kusaidia isaidie kwa sababu tutapata kwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niwaombe Waheshimiwa Wabunge, Waziri anapokuja kuhutubia leo aje na majibu ya kutuambia hivi vitabu vinatoka kwenye circulation. Aje na majibu ya kutuambia kwamba haiwezekani hivi vitabu vinasomwa na watoto wa Kitanzania. Lazima hawa walioandika vitabu hivi, nasikia kuna wengine mpaka vyeo wamewapa, how?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli, unampa cheo kwa kitabu hiki cha Kiingereza au ndiyo maana wanataka kila mtu aongee Kiswahili saa hizi maana Kiingereza imekuwa tabu. Ndiyo maana kila mtu anasema Kiswahili, Kiswahili, Kiswahili, Kiswahili, ni kwa sababu wameshafanya haya? Waheshimiwa Wabunge tusikubali kuingia kwenye historia na sisi tulishiriki kuua kizazi kijacho. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba nisiunge mkono hoja mpaka Waziri atakapokuja hapa kuniambia hivi vitabu wanavifanyaje? Nakushukuru sana.