Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi mchana wa leo ili niweze kusema maneno machache juu ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu. Nimpongeze sana mama yangu pale Mheshimiwa Profesa Ndalichako na Naibu Waziri Injinia Stella kwa kazi kubwa sana mliyoifanya pamoja na uongozi mzima wa Wizara ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina maeneo mengi ya kuchangia lakini nitaanza hasa na pongezi hususan ya ujenzi wa hosteli ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hili ni jambo jema sana kwa sababu Mheshimiwa Rais pengine na ushauri wako ameona awaondolee usumbufu watoto wetu. Wizara iliamua kujenga hosteli za Mabibo lakini Mabibo na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pana umbali kidogo lakini hili lengo la Mheshimiwa Rais kujenga hosteli pale ameondoa usumbufu mkubwa sana kwa sababu hosteli hizi zimelenga hasa watoto wa maskini. Wapo wenye uwezo ambao wana magari ya kwenda na kurudi vyuoni mfano Waheshimiwa Wabunge hapa wana watoto wanaosoma pale wana uwezo/magari ya kwenda na kurudi vyuoni lakini hosteli zile zitasaidia sana watoto wetu na kuondoa usumbufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri kwa sababu Mheshimiwa Rais ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi hosteli za chuo kikuu aangalie sasa namna ambavyo anaweza kusaidia kujenga hosteli katika shule zetu za kata. Waheshimiwa Wabunge wanazungumzia hapa watoto wetu kupata mimba lakini sisi tunaotoka katika majimbo ambayo ni ya vijijini kule tunaona watoto wetu wanatoka mbali sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu nimwombe sasa Mheshimiwa Waziri, najua Wizara ya Elimu na TAMISEMI wanashirikiana lakini leo hii lawama zinakuja kwa Waziri wa Elimu. Nimwombe, tuone umuhimu wa kujenga hosteli hususan kwa watoto wetu wa kike katika shule za vijijini hususan katika shule zetu za kata. Hii itaongeza uwezo wa ku-perform watoto wetu ufaulu utaendelea kwa sababu watapata utulivu wa kusoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nizungumzie juu ya suala la udhibiti na ukaguzi wa elimu. Wabunge wengi wamelizungumzia hapa na pengine kitendo hiki cha kukosa udhibiti wa elimu katika shule zetu hizi za sekondari na shule ya msingi ndiyo imepelekea vyeti feki. Leo hii ni takriban wafanyakazi 11,000 au 12,000 wana vyeti fake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri hili jambo lisipite hivi hivi, tuone umuhimu wa kufanya tathmini na kufanya research ndogo tatizo lipo wapi, ni NACTE au ni nani kakosea? Kwa sababu haya tunayozungumzia hapa tunazungumzia Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kati, tunazungumzia ajira, leo hii inaonekana Watanzania wengi wana vyeti fake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri aone namna ambavyo itanyika research ndogo na taarifa ije Bungeni hapa tuone tumekosea wapi aidha ni NACTE au ni nani ametufikisha hapa tulipo. Pia naomba wale wote ambao wameshiriki katika kutufikisha hapa sheria ichukue nafasi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kuchangia ni juu ya ujenzi wa vyuo vya VETA. Tunakwenda kwenye nchi ya viwanda. Sio wote ambao watapata fursa ya kwenda sekondari au kwenda katika vyuo. Vyuo vya VETA vitasaidia watoto wetu ambao hawajapata fursa waweze kusoma. Ukiangalia hapa maeneo mengi katika wilaya zetu hayana vyuo vya VETA mfano katika Jimbo langu la Kilindi toka 2010 tunazungumzia kujenga chuo cha VETA katika Wilaya ya Kilindi. Mwaka wa fedha mwaka jana walisema kwamba Wilaya ya Kilindi itakuwa ni miongoni mwa wilaya chache ambayo itajengewa chuo cha VETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha aniambie nini hatma ya Chuo cha VETA katika Wilaya ya Kilindi. Kwa sababu Halmashauri ya Wilaya Kilindi ilishatenga eneo kubwa sana takriban heka 20 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA. Tunahitaji Chuo cha VETA kwa sababu kitasaidia vijana wetu wa Wilaya ya Kilindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo suala la kidato cha tano ni muhimu sana. Sisi tunatoka maeneo ambayo miundombinu ni mibaya sana wapo vijana ambao wamefaulu lakini wameshindwa kwenda kidato cha tano katika maeneo mengine kwa sababu wazazi hawana uwezo lakini Wilaya ya Kilindi haina shule ya kidato cha tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna shule nyingi sana takriban tano ambazo zina sifa ya kuwa na kidato cha tano. Mfano shule ya Kikunde, Mafisa, Kilindi Asilia, hizi shule zina sifa, zina Walimu wazuri na miundombinu mizuri. Hivi tatizo liko wapi Mheshimiwa Waziri, kwa nini hatuna shule ya kidato cha tano? Nimwombe sana aone namna ambavyo na sisi tunaweza tukapata shule ya kidato cha tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni motisha kwa Walimu wetu. Nimepitia katika hotuba hii hapa ni kwamba wanatoa motisha kwa Walimu Wakuu lakini hawa Walimu wengine vipi? Kwa sababu motisha siyo pesa tu unaweza ukampeleka semina, ukawapeleka Walimu kusoma, hizo ni motisha. Tusitengeneze gap ya Walimu, tuwape motisha Walimu wote na hii itasaidia pia kuinua kiwango cha elimu Tanzania hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka pengine Mheshimiwa Waziri aliangalie ni suala la uwiano wa upangaji wa Walimu, hapa pana tatizo kubwa sana. Kwa mujibu wa taarifa ya CAG ya performance auditor aliyoifanya ni kwamba kuna mikoa Tanzania hii Mwalimu mmoja anafundisha darasa la watoto 26 lakini maeneo mengine mwalimu mmoja anafundisha watoto 46 maana yake ni nini? Maana yake maeneo yale ambayo Mwalimu mmoja anafundisha watoto 46 elimu haitakuwa nzuri na Walimu wengi sana wako mijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri kwa kushirikiana na TAMISEMI pitieni tena kuona uwiano na upangaji wa Walimu ulivyokaa kwa sababu Walimu wengi wako mijini, vijiji kule hakuna Walimu. Kuna baadhi ya shule Walimu wanagawana topic ya somo moja labda la historia au sayansi, hili haliwezekani. Hebu tuone namna ya ku-balance uwiano wa Walimu Tanzania nzima ili maendeleo ya nchi hii yawe kila kona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo machache, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.