Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa nami kuchangia katika bajeti hii ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuleta sera ya elimu bure, sambamba na hilo naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara ya Elimu kwa bajeti hii ambayo imeletwa mbele yetu ambayo leo hii tunaizungumzia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina baadhi ya masuala ambayo ningependa kuyachangia na iwapo kama muda utaniruhusu basi nitaendelea zaidi, lakini katika mambo ambayo ningependa kuyachangia ni pamoja na udhibiti wa elimu, suala la upatikanaji wa vitabu shuleni ambalo wengi wetu wamegelizungumzia, sambamba na hilo ni uanzishwaji wa bodi ya kitaalam ya walimu, suala la programu ya lipa kulingana na matokeo pamoja na elimu ya kujitambua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 85 amezungumzia kuhusu kuboresha mazingira ya elimu kwa wadhibiti ubora wa elimu. Kwanza niipongeze sana Serikali kwa kuamua kwamba watajenga ofisi 50 kwa ajili ya udhibiti wa elimu. Pamoja na pongezi hizo bado kuna changamoto nyingi sana na naamini kabisa Mheshimiwa Waziri analitambua hilo hasa kwenye ofisi zetu za udhibiti wa elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mimi natokea Mkoa wa Dodoma, tuchukulie ofisi yetu ya Udhibiti wa Elimu Kanda ya Kati. Kwa kweli baadhi ya vifaa hakuna, suala zima la samani, vitendea kazi na kadhalika. Hali kadhalika magari hayatoshelezi, sasa hapa tunazungumzia kuhusu kuboresha elimu, bila kuwa na vifaa vya kutosha je, tutafikia hili lengo kweli? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba niishauri Wizara hebu haya ambayo tunayazungumza hapa wayafanyie kazi, pamoja na kwamba katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri amesema kwamba watanunua kompyuta 100, lakini sambamba na hilo kwamba kuna baadhi ya Wilaya mpya ambazo zimeanzishwa, mimi naona idadi hii bado ni kidogo ni budi Wizara ikaongeza vifaa vingi zaidi kwa ajili ya utendea kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwamba ofisi nyingi za Udhibiti wa Elimu ni za kupangisha, kumekuwa na changamoto kubwa sana kwa sababu kwanza ya ucheleweshaji wa OC, wale watendaji wanaokaa katika ofisi hizi kwa kweli wamekuwa wakipata taabu sana na karaha kwa sababu OC imekuwa ikichelewa pengine miezi sita mpaka miaka miwili, kwa hiyo hii kwa kweli inawaletea karaha sana. Ninaishauri Wizara ni vizuri sasa ikaweka mkakati wa uhakika wa kupeleka OC kwa muda unaotakiwa ili kusudi watu hawa wasipate karaha hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kuna hili suala la elimu bure ambapo kwenye sera ya elimu bure inatakiwa kwamba kila mwanafunzi wa sekondari katika ile capitation fee inatakiwa shilingi 1,000 ipelekwe kwenye Idara ya Ukaguzi au Udhibiti wa Shule. Kwa masikitiko makubwa naomba niseme kwamba pesa hizi mara nyingine huwa hazifiki na hivyo kuchelewesha kabisa utendaji wa udhibiti elimu. Ninatoa ushauri kwa Mheshimiwa Waziri kwamba pesa hizi zimekuwa zikikatwa, lakini zikikatwa zimekuwa zikipelekwa katika akaunti ya Wizara na baadaye ndiyo zinakuja kupelekwa kwenye akaunti za Kanda. Hebu waone ili kupunguza urasimu ni vizuri kwamba pesa hizi zikikatwa zipelekwe moja kwa moja kwenye Ofisi za Kanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia suala la upatikanaji vitabu pia na udhaifu. Wenzangu wengi sana wamelizungumzia na hapa nina kitabu cha Steps in Primary Mathematics Book Four for Tanzania. Kitabu hiki kimetungwa na Mtunzi ambaye anaitwa Kireri K.K.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu kina maajabu sana, maajabu yake ni kwamba hapa nina vya huyu mtu mmoja ambaye amevitunga Ndugu Kireri K. K. Katika vitabu hivi ukweli ni kwamba yaliyoandikwa humu huwezi ukaamini, naomba jamani kwanza nilikuwa najiuliza hivi kweli EMAC ipo? Kwa sababu kuna baadhi ya vitabu vina ithibati ya EMAC, lakini kuna vitabu vingine havina ithibati ya EMAC. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ina maana kwamba hapa kuna issue ya pirating, tuone Wizara ifanye utaratibu wa kwenda katika kila shule na kufanya ukaguzi wa kujua kwamba vile vitabu halali ni vipi na visivyo halali ni vipi. Nina-declare interest mimi ni mwalimu by profession na nimekuwa Afisa Elimu Vifaa na Takwimu kwa zaidi ya miaka kumi, hiki kituko ninachokiona hapa ni cha ajabu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kutoa ushauri wangu kwamba Mheshimiwa Waziri, wenzangu wengi wamelizungumza hili, ninaomba sana iundwe Tume Maalum ambayo itakwenda kila shule kuona vitabu hivi kama vipo sahihi. Pia walimu na Maafisa Elimu wajaribu kuangalia hivi vitabu kabla hawajavinunua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani tulikuwa na utaratibu wale wachapaji na wachapishaji wakiwa wanataka kukuuzia vitabu, lazima wakuletee sample, na wakikuletea sample ni lazima ile sample lazima uipitie kabla hujainunua, jambo la kushangaza ni kwamba hivi vitabu ukiviona hakika ni kituko kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumzie kuhusu hii Teachers Professional Board, hili jambo limekuwa likizungumzwa kwa muda mrefu sana, ukurasa wa 80 katika hotuba ya Waziri imezungumzia lakini niseme kwa masikitiko makubwa sana hili jambo limeanza kuzungumzwa tangu mwaka 2009 na leo hii tuko 2017. Sasa ndugu zangu kwa kweli hili jambo itabidi kulifanyia haraka kwa sababu nilitegemea kwamba katika Bunge lijalo huu Muswada uwe tabled, lakini inaonyesha kwamba katika huu ukurasa wa 80 kwamba watakamilisha utaratibu wa uwanzishwaji, ina maana kwamba hata taratibu hazijakamilika, hebu naomba niishauri Wizara kuharakisha hii Professional Board ili walau walimu waweze kuona hii Professional Board ili kusudi tuepuke hao walimu ambao wanaingia katika hii fani bila utaratibu maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake pia ukurasa wa 88, kwenye suala la Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo. Niipongeze sana Serikali kwa kuamua kujenga shule ya kisasa kabisa katika Mkoa wa Dodoma, najua kwamba sasa hivi Dodoma ndiyo imekuwa Makao Makuu ya Chama na Serikali, ninapenda tu nimuombe Mheshimiwa Waziri kwamba isiwe shule moja tu, kwa sababu sasa hivi ujio wa watu katika Mkoa wa Dodoma utakuwa ni mkubwa sana. Kwa hiyo, Serikali na Wizara ione isiwe shule moja tu ziwe shule zaidi ili kusudi kuweza ku-accomodate wale watu ambao watakuwa wamefika katika Mkoa wa Dodoma.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo wenzangu wengi wamelizungumzia ni kuhusu elimu ya kujitambua. Niungane na Waheshimiwa Wabunge kwamba suala la mimba za utotoni ni tatizo kubwa sana katika jamii yetu. Sambamba na hilo kila mtu ana mtazamo wake wa kulibeba jambo hili, ila tu ninachoweza kushauri ni kwamba…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.