Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai na leo hii tunaweza kujadili bajeti hii ya mwaka 2017/2018. Pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuonesha azma yake ya kuwa muumini mzuri wa elimu na kupata Ph.D yake akiwa kwenye lile Bunge la Tisa kama Waziri. Pongezi kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilio changu ni tumrudishie mwalimu heshima yake. Madeni ya walimu yalipwe, walimu wapewe motisha, walimu wapatiwe vifaa vya kufundishia, walimu wapatiwe/wajengewe nyumba za kuishi hasa vijijini, walimu wapandishwe madaraja kwa wakati, walimu waruhusiwe kujiendeleza na kadhalika. Kwa kuwa walimu ndio wanaofundisha fani zote, mishahara yao iboreshwe. Ualimu ni wito utunukiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lugha ya kufundishia iwe kiingereza kuanzia shule ya msingi ili tuweze kuingia kwenye soko la ajira la Afrika ya Mashariki (East Africa) na kwingineko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ni mazingira duni ya kujifunzia yanayosababishwa na miundombinu katika maeneo husika kama maji, umeme, vyoo pamoja maabara. Ninaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kumaliza zoezi la madawati, lakini nalo limezaa tatizo la madarasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali Kuu isiziachie Halmashauri tatizo hili kwani si sahihi sana hasa ukizingatia kuwa uwezo wao ni mdogo na mambo ya kutekeleza ni mengi sana kwenye Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu bila malipo, juhudi za Serikali kutoa elimu bila malipo kwa watoto wote zinaendelea na mimi ninaziunga mkono na kuzipongeza sana. Wadau wa elimu na jamii wanazo hoja kuhusu ubora wa elimu wanayopata watoto, mjadala huu ni wetu sote. Ni jambo jema hasa tunapoelekea awamu ya nne ya mapinduzi ya viwanda inayoitwa exponential age.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha elimu hii inabidi wadau wote washiriki kikamilifu na kwa uaminifu mkubwa. Aidha, ninaomba Serikali itoe hela za kutosha kwenye Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, naomba kuwasilisha.