Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Profesa Joyce Ndalichako na Naibu Waziri, Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya, Makatibu Wakuu na watendaji wote wa Wizara kwa kuwasilisha bajeti yao ili tuijadili. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kumteua Dkt. Ave Maria Semakafu kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara hii, hongera sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kuunga mkono hotuba ya Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na hasa ukurasa wa 29 wa kitabu chao. Serikali itoe tamko rasmi juu ya wanafunzi wa kike ambao wamekuwa wakifukuzwa shule kutokana na kupata ujauzito kurudishwa shuleni ili waendelee na masomo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madeni ya walimu, niipongeze Serikali kwa kulipa madeni ya walimu kwa kuanza kulipa shilingi billion 33.1 sawa na asilimia mbili. Naiomba Serikali iongeze kasi ya ulipaji madeni hayo.

Katika Mkoa wa Iringa, walimu wanaidai Serikali shilingi 1,238,841,517.00, lakini tangu wamehakikiwa hakuna hata Wilaya moja iliyolipwa kabisa. Naomba kujua utaratibu unaotumika au vigezo vinavyotumika kulipa haya madeni katika mikoa na Wilaya zetu. Inakatisha tamaa sana kuona mwalimu anafundisha bila ari na chama kinataka kuandaa maandamano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu bure, niipongeze Serikali kwa ujenzi wa mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Niipongeze Serikali kwa programu hii, imeonesha kuwa kuna changamoto nyingi sana zilizojitokeza katika utekelezaji wa sera hiyo, lakini bila kuanza tusingezibaini changamoto hizo. Lakini ni vema Serikali iwe na mkakati wa kuzishughulikia changamoto kwa wakati ili azma ya Serikali iweze kutimia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuta Kodi ya Ujuzi (SDL) na uchangiaji wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) katika vyuo vikuu binafsi, ukisoma ukurasa wa 33 katika kitabu cha Kamati, unazungumzia kwa kirefu kuhusu hilo, naomba niunge mkono hoja. Hivyo vyuo havifanyi biashara bali vinatoa huduma kwa manufaa ya nchi yetu. Kuwepo kwa tozo hizi kunapelekea kuwa na changamoto ya kupanda kwa ada na kupungua kwa ajira ili vyuo viweze kujiendesha, Serikali iliangalie upya jambo hili na kwa umakini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto za elimu zilizopo katika vyuo vyetu vya Iringa, bei za nyumba katika maeneo yanayozunguka vyuo vya Iringa ni kubwa mno, ni vema Serikali ingetoa bei elekezi. Mikopo bado inachelewa sana, hasa wanafunzi wa elimu ya vitendo (field and research).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miundombinu ya watu wenye ulemavu, niipongeze Serikali kwa kusambaza vifaa vya kujifunzia na kufundishia lakini bado miundombinu katika shule nyingi si rafiki na watu wenye ulemavu kabisa. Mazingira ya vyoo vya shule nyingi bado si rafiki kwa watoto wa kike hasa wawapo kwenye siku zao. Uwiano uliopo kati ya idadi ya wanafunzi na idadi ya matundu ya vyoo bado si ya kuridhisha kwa viwango vya Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hali mbaya sana ya majengo ya shule; hali ya majengo ni mbaya sana, mfano katika Mkoa wetu wa Iringa shule nyingi tangu zijengwe hazijawahi kukarabatiwa, sera ipo vipi? Mtoto anasoma katika mazingira magumu sana, hakuna vioo, hakuna floor, hakuna ceiling board.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maktaba katika shule zetu, sera inasemaje kuhusiana na hili? Hali ya maktaba za shule za msingi na sekondari si nzuri, watoa huduma za maktaba (wakutubi) hawapati ajira kwenye maktaba za shule. Shule inapohamishwa inatakiwa iwe na maktaba lakini si shule zote zenye maktaba. Kama tusipozisimamia hizi maktaba hatutakuwa tumemtendea haki huyu mtoto tunayetaka kumjenga kielimu na kuwa na mazoea ya kujisomea ambayo ingemsaidia hata akienda elimu ya juu kuwa na utaratibu wa kusoma.