Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia Wizara hii muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu. Kwanza kabisa nianze kuzungumzia changamoto za elimu kwenye jimbo langu la Tarime Mjini. Licha ya Tarime kuwa mjini lakini tuna shule moja ya kidato cha tano na sita (A-Level) ambayo ipo tangu miaka ya 1960, na shule hii ni ya wavulana tu. Hivyo tunaomba ombi letu ambalo limekuwa ni la muda mrefu lipatiwe ufumbuzi kwa kupandisha shule za Nyamisangura na Mogabiri kuwa na A-Level kwa kuwa miundombinu yake inakidhi vigezo na pia tuna walimu wa kutosha wa kufundisha masomo ya A-Level. Tunaomba Serikali ione umuhimu wa kuanzisha hizi shule ili kutoa fursa. Kuna watoto wetu wa kike ambao humaliza na kukosa fursa za masomo ya A-Level. Limekuwa ni ombi la muda mrefu tunaomba lifanyiwe kazi mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Halmashauri ya Mji wa Tarime tuna changamoto za shule za msingi, kitu ambacho kinapelekea uhafifu na ubora wa elimu kwa sababu ya mazingira mabaya ya kufundishia na kujifunzia. Kumekuwa na uhaba mkubwa wa madarasa licha ya juhudi za wananchi pamoja na mimi Mbunge wao ambapo nimeweza kujenga maboma kadhaa, lakini Serikali inashindwa kuweza kukamilisha majengo yake ili yaweze kutumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Elimu inaelekeza kuwa na ratio ya wanafunzi 45 kwa darasa, lakini jimboni kwangu uwiano wa mwanafunzi kwa darasa ni darasa moja kwa wanafunzi 120 au 150 au 200. Hii haikubaliki na ni aibu kwa nchi yetu kwani ni dhahiri hapo kutakuwa hakuna mawasiliano kati ya mwalimu na mwanafunzi.
Naomba sana Serikali ilete fedha ili kuweza kumalizia maboma na kupunguza adha ya madarasa jimboni kwangu na hivyo kutoa elimu bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ni kuhusiana na uhaba wa nyumba za walimu ambapo walimu wanapanga nyumba mbali na shule zao kitu ambacho kinafifisha ufundishaji kwani walimu wanachelewa kurudi au kuja shuleni hasa kipindi cha mvua. Hii ni aibu na Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema walimu wawe na nyumba shuleni. Naomba Serikali ielekeze kwenye nyumba za walimu ili kuweza kutoa ufanisi kwenye kufundisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika jimbo langu kuna uhaba wa ofisi za walimu ambapo inapelekea walimu kukaa nje, chini ya miti hasa shule za Sabasaba, Azimio pamoja na Mapinduzi. Wengine kugeuza madarasa kuwa ofisi huku wakiwa hawana samani au makabati ya kuhifadhia vitabu. Kwa kweli hali ni mbaya sana, tunaomba Serikali ione haja ya kuboresha mazingira ya walimu ya kuandaliwa, kufundishia na kuishi. Hizi zitatoa motisha kwani walimu wana matatizo mengi sana kama vile madeni, kutokupandishwa madaraja, malimbikizo ya fedha za likizo na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ni kuhusiana na mahitaji au vifaa vya kufundishia. Kuna uhaba mkubwa sana wa vitabu kwenye jimbo langu, yaani uwiano wa kitabu ni 1:100, hii inaleta ugumu sana kwa mwanafunzi kuelewa. Inatakiwa kuwa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja, lakini sasa ni kitabu kimoja kwa wanafunzi 100 au 150; hii ni mbaya sana. Sasa cha kusikitisha ni juu ya vitabu vilivyogawiwa hivi karibuni kwa darasa la pili na la tatu, takribani 13,680,981 hivi vitabu vina makosa. Tunaenda kujenga Taifa la wajinga, maana mtoto huamini alichofundishwa au kusoma kwenye kitabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Wizara ione umuhimu wa kuweka nishati ya umeme kwenye shule zote ili kurahisisha ufundishaji na kutoa fursa ya wanafunzi kujisomea.
Pia tuweze kuboresha miundombinu ya vyoo kwenye shule zetu kwa ili ya kuboresha mazingira ya kujifunzia na kupunguza magonjwa kwa walimu na wanafunzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni juu ya elimu bure ambayo kwa kiasi kikubwa haijatoa nafuu kwa mwananchi na zaidi ime-affect, maana wazazi wamegoma kutoa michango ya chakula, hata wengine kwenye ujenzi. Lakini pia bado wazazi wanaochangishwa fedha za kulipa walimu wa sayansi wa kujitolea michango ni mingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nichangie Kitaifa juu ya nini kifanyike ili kuboresha elimu ya Tanzania na kujenga Taifa lenye watu walioelimika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kuomba Serikali ilipe madeni yote ambayo walimu wanadai, fedha za likizo, kupandishwa madaraja na stahili zote ikiwepo kuongezewa mishahara. Hii itatoa motisha na hamasa kwa walimu wetu na hivyo kuwa na ufundishaji bora na hivyo kuwa na elimu bora kwa wanafunzi wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wakati sasa Serikali ione umuhimu wa kuhakikisha makundi mawili, kwa maana ya wale wasiojiweza pamoja na watoto wa kike wapewe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni makundi muhimu sana ambayo yamekuwa sidelined. Vilevile tuwe na uwajibikaji kwenye elimu ya watoto wetu na hii ni kwa wadau wote maana ya wazazi na walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wakati sasa Serikali iwekeze kwenye majengo. Kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri anaonyesha ni madarasa 2,000 tu yatajengwa kati ya madarasa 158,674. Hii inaonesha dhahiri Serikali bado haijadhamiria kuondoa tatizo la msongamano mashuleni kwa kuwekeza kwenye miundombinu ya madarasa kwa sababu kwa speed hii itachukua miaka 79 kuweza kutatua tatizo la madarasa/msongamano. Pamoja na upungufu wa matundu ya vyoo 200,000 (Best 2016).
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba vifaa vya maabara jimboni kwangu maana majengo mengi yamekamilika lakini hatuna vifaa na wataalamu wa maabara hadi majengo yanageuzwa kuwa madarasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.