Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Katavi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza hotuba ya Kamati kwa kutoa maelekezo ya mahitaji ya elimu kitaifa pamoja na kuonesha utatuzi wa changamoto za elimu kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu nafasi ya mwanamke katika jamii; ukimuelimisha mwanamke utaokoa jamii. Hivyo basi, hatua za haraka zichukuliwe katika kuongeza bajeti ya miundombinu katika shule za bweni za wanawake; kuboresha upatikanaji wa maji ili yawe ya uhakika; usalama kwa mabweni yasio na fence; huduma za afya katika mabweni ya kike na uboreshaji wa chakula kwa mabweni ya wanawake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muda mrefu sasa wananchi wa Katavi wamekuwa wakisubiri ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo. Tunataka majibu ya Serikali, ujenzi utaanza lini na tufahamishwe kama fedha zimetumika nje ya utaratibu au zimeliwa au chuo kilihamisha? Tatizo hili kuendelea kukaliwa kimya na Serikali na Halmashauri ambapo zaidi ya shilingi bilioni moja zimeliwa na chuo hakipo, inamaanisha kwamba Serikali ya CCM inalinda wezi au imehusika moja kwa moja kudhulumu Chuo cha Kilimo kwa Wana-Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, faida ya kuwa na Chuo cha Kilimo Katavi ni kwamba kundi kubwa la wananchi wa Katavi ni wakulima na wafugaji hivyo kupitia chuo hiki wangepata elimu bila kutakiwa kusafiri kwenda mikoa ya mbali na kupunguza gharama hususani kuleta mapinduzi ya kilimo cha kisasa mkoani Katavi, uwekezaji, ajira na uchumi wa viwanda kupitia chuo chetu kilichoyeyuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uchache wa vitabu Katavi, tunaomba viongezwe pamoja na shule za sekondari na shule za msingi. Pamoja na juhudi za walimu Mkoa wa Katavi kufundisha wanafunzi katika mazingira magumu lakini ufaulu wa wanafunzi shule za msingi tumekuwa na matokeo mazuri kimsingi. Naomba vitabu viongezwe kwani hali ni mbaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanafunzi wasioona katika Wilaya ya Mlele mmetenga vitabu 6014, vitendea kazi kwa wanafunzi wasioona ni vichache mno viongezwe ili kuleta motisha.Fedha zilizotolewa kama motisha kwa Halmashauri P4R, shilingi 78,777,349 Mpanda, Nsimbo shilingi 102,473,308 na Mlele shilingi 80,688,319. Bado kuna uhitaji mkubwa, mbona mikoa mingine mmepeleka kiasi kikubwa cha fedha? Je, mmetumia kigezo gani katika mgawanyo huu kama sio ubaguzi huu wa keki ya Taifa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa vitabu vya sayansi na biology. Mkoa wa Katavi (mgawanyo Kiwilaya, Mpimbwe - 0, Mpanda - 0), nini kimetokea mpaka Wilaya za Katavi kukosa vitabu vya kidato cha tano na sita katika mchepuo wa sayansi? Hamuoni kwamba mnapunguza molari ya wanafunzi kusoma mchepuo ya sayansi vitabu? Kidato cha kwanza, jumla ya vitabu 6,030 Mkoa mzima na kidato cha tatu jumla ya vitabu 3,780. Ukiangalia wingi wa shule na uwiano wa vitabu hivyo inaonyesha kabisa hakuna dhamira ya dhati ya kusaidia ufaulu kwa wanafunzi wa sekondari zetu za Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za sekondari ya wanawake za Mpanda Girls na Milala sekodari. Shule hizi hazina wigo (fence) kwa ajili ya usalama wa wanafunzi hawa. Je, ni lini Serikali itatenga bajeti itakayotekelezeka ili kunusuru wanafunzi wetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, naomba majibu ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Katavi, ni lini utaanza na kama fedha zilitumika hovyo Serikali inawachukulia hatua gani wahusika? Vilevile naomba michango kwa wanafunzi ipunguzwe kwani ni changamoto kubwa kwa wazazi wenye hali duni kiuchumi.