Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi ya kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kuhusu nyumba za walimu. Sehemu za vijijini pamezidi kuwa na uhaba wa walimu, unakuta shule moja ina walimu wawili tu. Tatizo hili linatokana na kwamba unakuta mwalimu ametoka nyumbani kwake kwenye mahitaji yote anapangiwa shule za vijijini anakuta hakuna nyumba za walimu hata zikiwepo ni nyumba zisizokuwa na mahitaji yote jambo linalopelekea walimu wengi kukata tamaa kwenda vijijini sababu ya tatizo hilo. Nyumba za wakazi huwa mbali sana na shule. Je, Serikali ina mpango gani wa kupambana na changamoto hii ya uhaba wa makazi ya walimu? Sababu mwalimu asipopata makazi mazuri hatakuwa na morali ya kufundisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni madai ya walimu. Suala hili limekuwa ni jambo la kawaida kwa walimu kutolipwa stahiki zao kwa wakati. Kila mara tumeshuhudia walimu wakienda kudai fedha zao hawalipwi na madeni kuzidi kuwa makubwa. Tatizo lipo kwa walimu waliopo kazini na wakistaafu bado wananyanyaswa. Zaidi ya wastaafu 1,000 wanadai shilingi bilioni 138 ambazo ni mafao ya michango yao kwa NSSF na PSPF. Je, Serikali ina mikakati gani ya kutenga fedha kwa ajili ya wastaafu hawa?
Tatu, ni kuhusu wanafunzi wa kike wanaopata ujauzito wakiwa bado masomoni. Pamoja na kutenda kosa hilo lakini mtoto wa kike anaadhibiwa kwa kutoendelea na masomo wakati unakuta pengine aliyempa ujauzito wapo shule moja na anaendelea na masomo. Ni vizuri Serikali iliangalie suala hili kwa kuwaruhusu kuja kuendelea na masomo yao baada ya kujifungua lakini kuwe na special school kwa ajili yao ili wenzao wasije wakawanyanyapaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, ni kuhusu vyeti vya kughushi. Zoezi hili limewaathiri wafanyakazi wengi hadi kupelekea wengine kupata mishtuko ya moyo. Ni vizuri zoezi hili lingepangwa kwa madaraja, kuna wale walioghushi cheti kabisa, lakini kuna wale wametumia cha ndugu yake aliyeshindwa kuendelea kutoka darasa la saba na akaendelea kusoma na kufauli mpaka akapata Ph.D. Aidha, mtu huyu unakuta amefanya kazi kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo kama naunga mkono kutumia vyeti fake, lakini naisihi Serikali iwe na jicho la huruma kuwasamehe na kuwalipa mafao yao. Kama Serikali iliweza kuwasamehe mafisadi wa EPA iweje ishindwe kuwasamehe hawa? Kwa nini Serikali iliifumbia macho dhambi hii ya kutumia vyeti fake na wahusika walioajiri watu hawa wamewajibishwa vipi?
Nashauri kwa wale wanaolalamika wameonewa basi Serikali ifungue milango kwa watu hawa kwenda kulalamika na Serikali iwastaafishe kwa manufaa ya umma na walipwe posho zao zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwa na vyeti fake pia kuna elimu fake. Unakuta mtoto anaingia kidato cha kwanza hajui kusoma, kuandika wala kuhesabu. Kuna vitabu vya kufundishia vinachapwa na makosa tunategemea nini katika elimu ya watoto hawa?