Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Dr. Raphael Masunga Chegeni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Elimu pamoja na timu yake kwa kuwasilisha hotuba nzuri na yenye kukidhi mahitaji na matakwa halisi ya Watanzania. Naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti inayoisha kwa mwaka huu kwa kiwango kikubwa sana imejitahidi kutekelezwa kulingana na uwepo na upatikanaji wa fedha. Pamoja na yote, naomba niongelee elimu bure. Mpango huu umeleta faraja na matokeo chanya kwa mtoto na mzazi wa Tanzania kwani umesaidia kuwepo na ongezeko la watoto wengi kuanza masomo kwa idadi kubwa. Mpango huu uendelee kuboreshwa sambamba na miundombinu yake, vifaa vya kufundishia, motisha na maslahi stahiki kwa walimu na wadau wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujenzi wa madarasa ya shule za msingi, napongeza sana Serikali kupitia Wizara hii kwa kusaidia ujenzi wa vyumba vya madara ya shule ya msingi Nyamajashi – Lamadi na shule ya msingi Fogo Fogo - Kabita katika Wilaya ya Busega. Msaada huu umefanikisha kupatikana vyumba na vyoo stahiki kwa wanafunzi ambao kwa muda mrefu ilikuwa ni kero na hasa kwa kukosekana kwa miundombinu hii. Naiomba Wizara iendelee kuweka mikakati na kuboresha shule nyingi katika Wilaya ya Busega ambayo ina idadi kubwa sana ya wanafunzi na uhaba wa miundombinu. Nampongeza Mheshimiwa Waziri na namwomba msaada zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uanzishaji high school. Wilaya ya Busega haina high school. Napongeza sana msaada wa Wizara kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuanzisha shule ya A-Level Busega ambayo ni Mkula sekondari. Hadi sasa maandalizi yanaendelea vizuri na niombe tu Wizara ihakikishe masomo kwa wanafunzi watakaochaguliwa yanaanza. Sambamba na shule ya sekondari Mkula, naomba mwaka ujao wa fedha pawepo na mpango wa kuanzisha shule mbili zaidi za A-level kwani idadi kubwa sana ya wanafunzi hawapati fursa ya kuendelea na masomo kwa michepuo mbalimbali. Nashauri pawepo pia na shule maalum ya A-level kwa ajili ya watoto wa kike (wasichana) ambao wamekuwa wakiathiriwa na mila potofu na kunyimwa fursa ya kusoma.

Mheshimiwa Waziri, kuhusu Chuo cha VETA, tumetenga eneo kwa iliyokuwa kambi ya ujenzi wa barabara ya Nyanguge - Musoma ya Sogesca kwa ajili ya uanzishaji wa Chuo cha Mafunzo Stadi kwa Vijana (VETA). Tunaiomba Serikali kukubali kuanzisha chuo hiki kwa kuwa baadhi ya miundombinu ikiwemo karakana, mabweni na madarasa vipo tayari likiwemo na bwalo la chakula. Hii ni bahati nzuri na mpango nafuu licha ya faida pia eneo hili liko kandokando ya Ziwa Victoria, hivyo suala la maji na umeme tayari vipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhitimisha, naamini Mheshimiwa Waziri atanikubalia maombi yangu na kuonyesha utayari wa kuyatekeleza ikiwemo ya yeye mwenyewe kuja na kutembelea Busega.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.