Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Mgeni Jadi Kadika

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kuchangia hotuba hii. Elimu ni ufunguo wa maisha, kila mtu atahitaji elimu ili aondoe ujinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uhaba wa walimu, kuna shule nyingi katika nchi hii na mikoa mbalimbali zina uhaba wa walimu hasa walimu wa sayansi. Tatizo hili ni kubwa na hasa shule za vijijini kwa sababu walimu wengi wanataka kufundisha mijini kutokana na matatizo yaliyoko vijijini, mfano, nyumba za kuishi, umbali wa shule na hawana vipando na kukosekana kwa miundombinu ya barabara au mwalimu mwanamke kuwa mbali na mume wake au mume kupangiwa kusomesha mbali na mke wake. Tunaomba maslahi yaboreshwe angalau waweze kujikimu na maisha. Walimu hawa wana kazi kubwa, sisi humu Bungeni tusingefika kama si kazi ya walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iwaangalie sana walimu wenye tabia mbaya wanaoharibu wanafunzi kwa kuwapa mimba au kumpasisha mwanafunzi kwa kufanya naye ngono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo walimu wanawapa wanafunzi adhabu kubwa kupita kiasi. Kama vile mtoto kupigwa mpaka kupoteza fahamu au kupata ulemavu na wengine mpaka kuwapoteza maisha na wengine kutoroka shule au kufungiwa chumbani. Walimu hao watakapobainika wachukuliwe hatua zinazostahiki ili iwe fundisho kwa wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto waliopata mimba mashuleni ni wengi na wengi wao ni wale waliokuwa hawana uwezo kwa kudanganywa na wanaume kwa kupewa chips au matumizi madogo madogo. Kwa hiyo, naiomba Serikali watoto wakibeba mimba warudishwe shuleni ili waendelee na masomo. Naomba waige mfumo wa Zanzibar. Pia naomba shule ziwe na mabweni ili kuwapunguzia watoto wa kike tatizo la kubakwa na kupata mimba zisizotarajiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za Serikali ambazo hazina matundu ya vyoo vijengwe vyoo na miundombinu ya maji kwa sababu watoto wa kike wanapokuwa katika siku zao wengi wanakosa masomo na hii ni changamoto kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango huo, naomba kuwasilisha.