Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana na nichukue fursa hii kuunga mkono Bajeti Kuu ya Serikali, lakini kabla ya hapo nichukue fursa hii kwako wewe Mheshimiwa Spika na Bunge lako Tukufu kuwakaribisha kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoanza tarehe 28 Juni, 2017 na yatakwenda mpaka mwezi wa saba tarehe 8 Julai, yakishirikisha nchi za Kimataifa kama 30 na makampuni 2,500. Tutaonesha bidhaa ya Tanzania, bidhaa kama nilizovaa, siwezi kutembea, ninacho kiatu kutoka Karanga Prison na hizi nguo kutoka 21st Century Morogoro na mshonaji ana kiwanda kidogo; kwa hiyo, nitumie fursa hii kuwakaribisha Sabasaba, mje muone bidhaa ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yaliyozungumzwa kwenye Bajeti ya Serikali Kuu. Bajeti hii ni ya ujenzi wa uchumi wa viwanda. Bajeti hii kwa ujumla wake ni ya ujenzi wa uchumi wa viwanda, si ya ujenzi wa viwanda tu, ni ya ujenzi wa uchumi wa viwanda. Nichukue fursa hii kuwatoa wasiwasi watu waliokuwa na mashaka kwamba hatutajenga viwanda kwa sababu mwaka uliopita Mheshimiwa Mwijage alitengewa shilingi bilioni 40 akapewa saba, lakini viwanda havitajengwa; la hasha angalia upande wa pili nilipopewa shilingi bilioni 40 zikaja shilingi bilioni saba nimetengeneza viwanda vya shilingi trilioni 5.2, kwa hiyo hayo mambo hayahusiani.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo katika kipindi hicho tumetengeneza miundombinu wezeshi na ile miundombinu saidizi itakayopunguza transaction cost na production cost, ndipo uchumi utakavyoweza kuchangamka.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la viwanda kuna watu wana mashaka kwamba hatujui changamoto za viwanda, si kweli tutendeane haki, kama kuna watu wanajua Serikali hii inajua changamoto zote. Tunajua mimi na Wizara yangu tunakutana na wawekezaji kila siku, pia viko vikao vya ubia kati ya mimi na Waziri wa Fedha tunakutana tukiwa wenza kuzungumza na wawekezaji wote, tunajua changamoto zao. Hata hivyo wawekezaji wanaweza kuwa na matakwa yao Serikali haiwezi kuyatimiza kwa wakati mmoja. Bajeti hii naipongeza imejibu hoja za Wabunge na wananchi wote.

Mheshimiwa Spika, nilipokuwa nawasilisha hapa nilikuja na vitabu vingi, nikawaonesha kitabu kimoja cha mawasiliano yangu mimi na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na yote yaliyosemwa ambayo yametokana na Dawati la Wepesi wa Kufanya Biashara ambalo nalisimamia mimi mengi mengi yametekelezwa.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kuwaomba wananchi wote wakiwemo Wabunge na wafanyabiasha, tunaanza upya, leteni mawazo yenu kwa kile ambacho mnadhani akikutekelezwa au kile ambacho kimeibuka. Kwa sababu biashara ni dynamic siyo static upepo unabadilika. Kwa hiyo, leteni mawazo yenu nitayapeleka kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Tumekubaliana na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mawaziri wengine tutawaalika, tutakutana mara nne kwa mwaka ili kuhakikisha kwamba tunaweza kwenda kwa pamoja.

Mheshimiwa Spika, kuhusu vivutio vikubwa vya uwekezaji ni mazingira bora ya kufanya biashara, the easy of doing business. Naomba nieleze sasa hivi wakaguzi wa wepesi wa kufanya shughuli ndio wanapita kuangalia nchi gani ndiyo inafanya vizuri. Msipige kelele msizungumze kama kwamba nchi hii inawaka moto, hapana, sisi ni miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri ila tuna tamaa ya kufanya vizuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu wepesi wa kufanya biashara timu ya Serikali kwa kushirikiana na private sector imefanya kazi nzuri na ripoti hiyo ndiyo inafanyiwa kazi, yale yote mliyoyasema yataondolewa. Mheshimiwa Tizeba amesema kuna tozo zimeondolewa lakini tunataka ziondoke zaidi. Tutakwenda hatua kwa hatua Idara za Serikali, Wizara zote na wote wawe tayari kuondoa kile ambacho kila Mtanzania ataona kwamba kinamkwamisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lipo suala la bidhaa bandia na bidhaa zisizokidhi viwango. Nilizungumza kwenye bajeti yangu kwamba ndiyo kazi ninayokwenda kuifanya, hii kazi si rahisi, inahusu change of mind na kwamba wale wanaokwenda kukamata na wao lazima uwabadilishe. Hata hivyo niwaambie hakuna jiwe litakalobaki bila kugeuzwa. Kama Jemadari Mkuu anapambana na makinikia mimi nitashindwa je kupambana na panya hawa? Nitapambana nao, bidhaa bandia Tanzania hazitaiingia.

Mheshimiwa Spika, tuna tatizo la vifaa vya vitenzi vinakuja bandia, waende majenerali wapambane kule juu na mimi nitapiga hawa panya.

Mheshimiwa Spika, juu ya aina ya viwanda kwamba sisi hatujui aina ya viwanda hakuna, Mheshimiwa Rais amesema jengeni viwanda ambavyo vinachakata maliasili au mazao ya wananchi, ndivyo tunavyojenga. Kesho kutwa nakwenda Kibaha, Mkuu wa nchi anakwenda kuzindua kiwanda cha kuchakata matunda. Limeni matunda kuna viwanda vimetengenezwa vya kuweza kuchakata matunda yote.

Mheshimiwa Spika, lakini msiende mbali sana, hapa Dodoma kuna Kiwanda cha Asante kinaweza kuchakata matunda yote yanayoweza kulimwa Ukanda wote wa Kati, kwa hiyo tunajua, lakini tumeelekeza tuwekeze nguvu katika viwanda ambavyo vinaajiri watu wengi. Ila niwaeleze kiwanda cha vifaa vya ujenzi kama vigae kinachukua muda mfupi kujengwa kuliko kiwanda kinachoajiri watu wengi. Mpaka sasa nina viwanda ambavyo vikianza kazi Morogoro na Kigoma tutaweza kuzalisha sukari zaidi ya mahitaji ya nchi hii, lakini viwanda vya namna hiyo vinachukua muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mchengerwa nikuambie umesema, umelalamika nimekusikia, Mheshimiwa Waziri Mkuu amekusikia, Waziri wa Ardhi amekusikia waliochukua ardhi Rufiji lazima niende nilale nao mbele kama nikishindwa nitapimwa kwa hilo. Ardhi ya Rufiji inaweza kuzalisha sukari, Mbunge anasema njoo Waziri anasema njoo, nani anapinga? Nakwenda kufanyakazi juu ya Rufiji na Mchengerwa usiache kupinga kelele piga kelele na mimi nakusikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu Bandari ya Bagamoyo. Tume ya Serikali imeshapokea ripoti ya mwekezaji kuhusu Bagamoyo, Bagamoyo mwekezaji yuko tayari kumaliza kila kitu. Ni juu yetu sisi Serikali kukubaliana naye ili tuweze kumruhusu aendelee.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru karibu Sabasaba, karibu uone bidhaa ya Tanzania. Kwa mara ya tatu tena naomba kuunga mkono hoja bajeti ya Mheshimiwa Mpango na Mama Kachwamba, twende mbele.