Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia hoja iliyowekwa mezani na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango na kabla sijaanza kuchangia naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha sote kufika hii siku ya leo na kunijalia mimi mwenyewe uzima na nafasi katika kulitumikia Taifa langu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu naomba pia niwashukuru wazazi wangu, baba na mama yangu, mimi kama kitinda mimba wao nawashukuru sana kwa kuendelea kuniombea, kuniamini na kunipa radhi yao ili niweze kulitumikia taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia nimshukuru sana rafiki yangu wa kudumu na mume wangu mpenzi Dkt. Muhajir Kachwamba ambaye yupo ndani ya Bunge hili, nikushukuru sana kwa kuendelea kuwa rafiki yangu kwa kila hali na katika kila gumu na jema ninalolipitia, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana naomba pia nimshukuru mtoto wangu mwingine ambaye yupo shuleni yuko kidato cha nne, Samira Muhajir; nimuombee kwa Mwenyezi Mungu aweze kufanya vizuri katika maandalizi yake na mtihani wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda nitoe pongezi; pongezi zangu ziende kwa Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli kwa uthubutu, ujasiri na ujemedari wake wa kurejesha hadhi ya taifa letu ndani ya Bara letu la Afrika. Tanzania imekuwa mfano na namshukuru sana Mheshimiwa Rais, naendelea kumpongeza na niseme kama Mbunge wa Kondoa, kama alivyosema alipokuwa akiomba kura alipofika Kondoa na sasa anayatekeleza kwa vitendo yale yote aliyowaahidi wapiga kura wetu wa Jimbo la Kondoa. Nimwambie wapiga kura wetu wa Jimbo la Kondoa wapo na yeye asilimia mia moja wanamuunga mkono, aendelee kuchapa kazi kwa niaba yao na kwa niaba ya Watanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimshukuru na nimpe pongezi sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango. Amekuwa ni kiongozi makini, mwenye dira na asiyetetereka; namshukuru Mwenyezi Mungu kunipa nafasi ya kufanya kazi na Mheshimiwa Dkt. Mpango. Imedhihirika kwenye bajeti hii ya mwaka huu imemuonesha Mpango ni nani katika tasnia ya uchumi, huyu ndiye Dkt. Mpango, katika tasnia ya uchumi wanakufahamu Dkt. Mpango, chapa kazi sisi watumishi tulio wako chini yako tuko na wewe, tutapokea maelekezo yako na tutaendelea kuyatekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia niwape pongezi watumishi wote wa Wizara ya Fedha na Mipango; naomba niwakumbushe wakati tunaanza vikao vya Kamati ya Bajeti pale mwezi wa pili niliwaambia kama ni siku basi sasa hivi ndiyo alfajiri, ndio saa kumi na moja, mpaka tutakapoelekea. Naomba niwape pongezi sana, wamefanya kazi usiku na mchana bila kupumzika wakipokea maelekezo na wakiyafanyia kazi mpaka saa kumi usiku, hongereni sana chini ya Katibu wetu Mkuu Bwana Doto James. Mmeonesha kwamba Wizara ya Fedha tunaweza na tumeweza kurejesha hadhi na tunaendelea kukimbia, hongereni sana na tupo pamoja na nanyi viongozi wenu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa nichangie baadhi ya hoja ambazo zimetolewa humu ndani, niweze kuzitolea ufafanuzi. Niwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kuleta hoja mbalimbali ambazo ni za kuimarisha na pale penye kukosoa mmeweza kukosoa, nawashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, hoja ya kwanza ambayo ningependa kuitolea ufafanuzi ipo katika kitabu cha hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, Msemaji katika Wizara ya Fedha na Mipango, nayo alisemea kuhusu hali ya uchumi wa Taifa na akaendelea kusema ametoa katika taarifa ya Benki ya Dunia. Naomba ninukuu maneno machache yaliyoandikwa kwenye kitabu kile, aliandika yafuatayo:-

“Kukua kwa uchumi kumepungua kutokana na upatikanaji wa fedha kuwa hafifu na kutotabirika/ kutokueleweka kwa Rais Magufuli.”

Mheshimiwa Spika, hoja yake ya pili, aliandika, baadhi ya wawekezaji wa kigeni wameamua au; naomba tuangalie sana hapa ninaposema au kwa sababu anaandika neno halafu analitafutia neno la pili; au wanataka kupunguza shughuli zao na akasema sababu zake ni hizi zifuatazo; alisema moja, ni masharti mapya, magumu na kutozwa kodi kubwa na sababu ya pili katika hilo akatoa reference kutoka PricewaterhouseCoopers Comparative World Studies of Tax Regimes of 2014.

Mheshimiwa Spika, naomba sana Waheshimiwa Wabunge na hasa ndugu zangu wa Kambi Rasmi ya Upinzani tunapojenga hoja zetu tuzijenge tukiwa na uhakika nazo. Umesema mwanzo kabisa kwamba kutotabirika au kutokueleweka kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Magufuli halafu reference ya 2014, hivi reference ya 2014 Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli alikuwa Rais kweli? Kwa hiyo, tuwe na uhakika na nini tunakipeleka.

Mheshimiwa Spika, unasema masharti magumu na kutozwa kodi kubwa; Mheshimiwa Spika wewe ni shahidi na Bunge lako tukufu, ni kodi zipi mpya ambazo zimeongezwa baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani? Anaongelea hizo kodi mpya na kubwa anatoa reference ya mwaka 2014. Hii ni ngumu sana, lazima tuwe na uhakika ni nini tunakifanya na tunalitendea haki Taifa letu kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa naomba nimwambie na niwaambie Watanzania kwa ujumla, kwanza waendelee kuamini taarifa iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango kuhusu hali ya uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nina kitabu nimekiacha hapa, nitakukabidhi wewe ili ndugu zetu wakifanyie reference. Hiki ni kitabu kilichoandikwa na World Bank alikosema yeye amepata data hizi. Katika kitabu hiki cha taarifa iliyoandikwa na World Bank ni cha tarehe 23 Februari, 2017; chenye kichwa cha habari kinasema United Republic of Tanzania Systematic Country Diagnostic.

Mheshimiwa Spika, katika kitabu hiki ambacho ni very current, cha mwezi wa pili, ndani yake wamesema nini; wamesema, naomba ni-quote maneno yao kwa Kiingereza, wanasema:-

“For the past 10 years the country’s macroeconomic performance has been robust, with GDP growing annually at an average of 6.5 percent-higher than the Sub-Saharan African average and that of many regional peers.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tafsiri isiyo rasmi katika hili ni kwamba kwa miaka kumi sasa uchumi wa Taifa letu umekuwa mzuri na umekuwa ukikua kwa zaidi ya wastani wa asilimia 6.5, juu zaidi ya wastani wa ukuaji wa uchumi wa nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara na wenzetu waliotuzunguka katika Ukanda wetu wa Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hizi ndizo taarifa tunazotakiwa kuwapa wananchi wetu, kwa lengo lolote lile ambalo unalo ni vizuri kuzisema kwa umakini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika taarifa hiyo ya Benki ya Dunia ya mwezi wa pili inasema kumekuwa pia na kupungua kwa umaskini kunakoambatana na kupungua kwa utofauti wa kipato kati ya makundi mbalimbali ndani ya jamii. Huu ndio uchumi wa Tanzania na niwaombe Watanzania waendelee kuamini. Kitabu hiki kimetaja sababu ambazo tumekuwa tukizisema hapa kwa nini wamesema hiki wanachokiona na kwa nini taarifa zao zimeonesha hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wamesema taarifa ya kwanza ni kuimarika kwa miundombinu ya barabara na masoko ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, nani si shahidi wa kwamba Nchi yetu imeweza kuunganishwa sasa mkoa kwa mkoa nchi nzima kasoro Mkoa mmoja wa Rukwa. Tuitendee haki nchi yetu, tuwatendee haki viongozi wetu, tumtendee haki Mheshimiwa Rais wetu ambaye kabla ya kuwa Rais alikuwa Waziri wa Miundombinu na Uchukuzi, lazima tumtendee sana haki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sababu au kiashiria cha pili kilichosababisha conclusion ya taarifa yao na utafiti wao, walisema ni kumiliki kwa vyombo mbalimbali vya mawasiliano na usafiri kwa Watanzania wote. Sisi sote ni mashahidi, kijiji gani utaenda ndani ya nchi hii ukose usafiri dunia ya leo? Hilo ni jambo la msingi sana, utafika popote hata kama kijiji kipo interior kiasi gani utapata usafiri na utafika, naomba ndugu zetu waweze kututendea haki.

Mheshimiwa Spika, naamini sisi sote humu kama Waheshimiwa Wabunge tunawahudumia wapigakura wetu kwa e-payments; hivi kweli sisi ndio wa kusema kwamba uchumi wa nchi yetu haukui? Nani ambaye hatumi M-Pesa, Tigo-Pesa, Airtel-Money kwa wapigakura wake kijiji chochote ndani ya Tanzania? Lazima tujitendee haki na tuwatendee haki Watanzania. Hivi ni baadhi tu ya viasharia vilivyowekwa na taarifa hii, vipo vingi, kama nilivyosema nitakabidhi taarifa hii kwako ili ambaye anataka kufanya reference aje afanye reference ili tuwe na uelewa wa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie na nukuu chache kuhusu hali ya uchumi wa Taifa letu kutoka kwa wageni mbalimbali waliolitembelea Taifa letu miezi michache iliyopita. Mmoja wao alikuwa Naibu Mkurugenzi wa Benki ya Dunia, Bwana Tao Zhang; akiwa Tanzania, wala hakuwa Washington, alikuwa Tanzania; alisema hivi, nanukuu maneno yake:-

“Uchumi wa Tanzania umebaki kuwa imara kutokana na maboresho ya kisera yanayotekelezwa chini ya uongozi thabiti wa Rais John Pombe Joseph Magufuli.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, akasema hasa katika suala la ukusanyaji wa mapato na vita dhidi ya rushwa na ugaidi. Hao ndio wachumi wa dunia na wanafanya analysis kwa kutumia data ambazo ni credible, naomba tuendelee kuwaamini.

Mheshimiwa Spika, sishangazwi sana na maneno haya yaliyopo kwenye Hotuba hii ya Kambi Rasmi ya Upinzani. Naomba ninukuu pia maneno ya mwekezaji mmoja kutoka China ambaye alikuwa anatafuta taarifa za kwenda kuwekeza katika viwanda vya ngozi na viatu nchini Ethiopia. Mwekezaji huyu kabla hajaenda alikuwa akitafuta taarifa, na haya maneno yake alisema, akasema:-

“Ukiwa nje ya Afrika unapewa picha na baadhi ya watu wakiwemo Waafrika wenyewe kwamba Afrika ni sehemu ya vita, Afrika ni sehemu iliyojaa njaa, Afrika ni sehemu ya magonjwa na kusahau kuwa Afrika ina mchango mkubwa na fursa nyingi katika mchango wa dunia.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nanukuu maneno haya ili tu Watanzania watuelewe, kwamba tunachokifanya chini ya uongozi wa jemedari, Dkt. John Pombe Magufuli ni kuimarisha uchumi wa kila Mtanzania (inclusive growth for everyone in Tanzania) hiki ndicho tunachokifanya. Niwaombe Watanzania wapuuze taarifa zilizowasilishwa, niwaombe sana ndugu zangu, Mheshimiwa Bunge lako hili ni Tukufu, litendewe haki kwa kuletewa taarifa ambazo ni haki, taarifa ambazo ni halali, taarifa zenye vyanzo vyenye uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hili, naomba sasa niendelee na baadhi ya hoja nyingine. Hoja ya pili ambayo ninapenda kuielezea ilisemwa na niliitolea maelezo, yawezekana sikuelewa vizuri; ilikuwa ni kuhusu Serikali kutoa maelezo kuhusu utekelezaji wa ahadi ya shilingi milioni hamsini.

Mheshimiwa Spika, wewe umeshuhudia Waheshimiwa Wabunge wakiongea kwa uchungu, wengine kwa kejeli ambazo sio nzuri na hili pia limeandikwa kwa kejeli kubwa sana katika Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani katika Wizara ya Fedha na Mipango.

Naomba nikumbushe, wakati tuna-conclude Bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango nilisema fedha kwa mwaka wa fedha 2016/2017 zilitengwa shilingi bilioni 59.5, na mwaka huu tumetenga shilingi bilioni 60 chini ya Fungu 21 - Wizara ya Fedha na Mipango. Fedha zimetengwa na hazina wasiwasi kwamba hazipo, zipo fedha hizi. Nikasema kwamba tunachokifanya sasa ni kuhakikisha tunasoma mfumo mzima, tunajifunza kutokana na makosa yaliyotendeka huko nyuma ili tuhakikishe fedha hizi za walipa kodi wa Tanzania zinakuwa na matokeo chanya katika Taifa letu na zinaweza kutekeleza kile ambacho kimesababisha Mheshimiwa Rais aweze kuahidi ahadi hii ya shilingi milioni hamsini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yapo maswali ambayo tunajaribu kujiuliza kama wataalam wa uchumi, kwamba hivi governance ya hii shilingi milioni hamsini ikoje katika kila kijiji? Hivi tunaposema tunapeleka, tunapeleka shilingi milioni hamsini hizi katika mfumo upi? Tunajiuliza ni njia gani bora tunaweza kumpatia pesa Mtanzania huyu aliyeko kijijini kwangu kule Kalamba. Tunajiuliza, je, baada ya kutambua kijiji kinahitaji kiasi hiki tunawezaje sasa kujua nani anapata nini na kwa kiasi gani na anakwenda kutekeleza mradi gani? Tunaweza kujiuliza na kujibu maswali, je, ni mfumo gani tunataka kuutumia sasa ili kurejesha fedha hizi? Tukumbuke nilisema hapa kwamba fedha hizi si zawadi, fedha hizi ni mkopo. Fedha hizi zinatakiwa zipelekwe zikaimarishe uchumi na hatimaye tuhakikishe zinazunguka kwa Watanzania wote na kila Mtanzania anafaidika na pesa hii na mwisho wa siku pesa hizi zinarudi ndani ya Serikali yetu tukiwa tumeimarisha uchumi wa watu wetu.

Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwamba mpaka tulipofika tupo hatua nzuri sana, na pesa kama nilivyosema shilingi bilioni 59.5 zipo, shilingi bilioni 60 tumetenga kwenye bajeti yetu ya mwaka huu, zote tutazipeleka kama ambavyo tuliahidi. Sasa hivi tumefika hatua nzuri, tayari Waraka wa Baraza la Mawaziri umeandaliwa kuhusu utaratibu na maeneo pamoja na mfumo utakaotumika katika kutekeleza programu hii ya uwezeshaji wananchi wetu kiuchumi. Niwaambie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais na tumeona kwa pamoja, hakuna ahadi anayoahidi akashindwa kuitekeleza, anatekeleza ahadi zake zote na hili atalitekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niende kwenye hoja nyingine ambayo imesemwa sana kwamba Serikali inaona kuwa na utaratibu wa kukopa zaidi katika soko la ndani, hali hii kiuchumi si nzuri kwa kuwa taasisi za fedha zinakimbilia kuikopesha Serikali zaidi kuliko sekta binafsi. Katika hili tunafahamu zipo instruments mbalimbali zinatumika kuhakikisha Serikali inakopa na inakopa kwa vigezo, inakopa ikiwa na ukomo kwamba inakopa kiasi gani ili isiathiri utendaji wa sekta binafsi ndani ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama Wizara ya Fedha na Mipango tunafahamu sekta binafsi ndiyo engine ya uchumi, hatuwezi Serikali kufanya kitu chochote kinyume na sekta binafsi. Tunachukua tahadhari ya kutosha katika kulifanya hili na Serikali, kama nilivyosema, imeweka ukomo wa kukopa ndani usiozidi asilimia 1.5 ya Pato la Taifa kwa mwaka ili kuzipa nafasi benki za biashara kuendelea kukopa mikopo kwenye sekta binafsi ambayo ndiyo engine ya uchumi wetu kama nilivyosema. Kwa mwaka huu tumeona kwamba tupunguze kiwango cha kukopa kutoka ndani na mwaka huu tunakopa asilimia moja tu ya Pato la Taifa ili kuipa nafasi sekta binafsi kuchukua mikopo ndani ya benki zetu. (Makofi)

Jambo lingine ambalo limesemewa sana; nililijibu lakini naona nalo halikukaa vizuri au Waheshimiwa Wabunge hawakunielewa ilikuwa ni mikopo kutoka mifuko ya hifadhi ya jamii, kwamba Serikali imekuwa na tabia ya kukopa fedha kutoka Mifuko ya Jamii bila kuzirudisha kwa wakati, nini mpango wa Serikali wa kulipa madeni hayo?

Mheshimiwa Spika, naomba niseme kama nilivyosema kwenye jibu la hoja iliyopita, kukopa ndani ya nchi na hasa kwa mifuko yetu tunaipa nafasi pia mifuko yetu kupata fedha ambazo ni za uhakika. Hata hivyo, katika kulipa madeni haya naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba katika uchumi malipo ni jambo la muhimu lakini kuhakikisha unalipa nini ni jambo la muhimu zaidi, na hicho ndicho ambacho kimechelewesha malipo haya kwa Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii. Tumefanya uhakiki; na ninaomba nitoe taarifa chache tu ya kuona ni kwa nini Serikali iliona ni muhimu kufanya uhakiki wa madeni haya, tuchukue mfano mmoja… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, muda umekuwa ni mchache sana lakini naomba niseme kwamba hoja hizi tutaziwasilisha kwa maandishi, na ninaomba niseme kwamba nia na lengo la Serikali yetu ni jema sana la kuhakikisha tunalipa mikopo yote, si ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii tu bali ya wakandarasi, wazabuni pamoja na watumishi. Tunafanya hivyo kuhakikisha Watanzania wanaweza kuimarisha uchumi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na ninaomba niseme naunga mkono hoja hii ya Serikali iliyowekwa Mezani na Waziri wa Fedha na Mipango ambayo imetuhakikishia Serikali yetu ina nia ya dhati ya kuhakikisha uchumi wa viwanda na uchumi wa kati unafika Tanzania kabla ya mwaka 2025.