Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi nami niwe wa kwanza kuchangia katika hotuba hii ya Viwanda na Biashara. Kwanza nianze kwa kuishukuru Serikali ya CCM inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri wote na watendaji wa Wizara mbalimbali kwa kazi nzuri wanazozifanya katika kutekeleza Ilani ya CCM. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia hapa hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, ukurasa wa 24. Hivi Mkuu wa Nchi ndiye baba, Rais, amepita mahali wananchi wamelalamika akatoa jibu kwamba atawasaidia, sasa hapa wanasema kwa nini alitoa majibu ya papo kwa papo kule wapi na nini, walitaka afanye nini? Watu wamemlalamikia Mheshimiwa Rais, si lazima ndio awape majibu wanasubiri na kwenye Ilani ya CCM tulisema tutatekeleza tutatoa majibu ya kuwasaidia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo vile vile Bunge lako hili tumesema kwamba kuna baadhi ya mikataba hasa ya madini sio mizuri tulisema hapa, sasa imetekelezwa tena tunalalamika tunasema kwa nini michanga na kadhalika, aaa. Serikali imeunda Kamati ya kushughulikia, tuiache Serikali ifanye kazi yake. Kwa hiyo naipongeza sana Serikali kwa kazi nzuri inayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie juu ya Wizara hii, juu ya fidia iliyoko katika Soko Kuu la Kimataifa katika Mji wetu wa Makambako. Kitabu cha bajeti, kilichopita cha 2016/2017, Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi wa Makambako na Mheshimiwa Rais alipopita pale aliwaambia fidia hii mtalipwa; na alipokuja Waziri Mkuu alisema majibu nitarudi nayo mimi ya kuwalipa fidia wananchi wa Makambako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kabisa Serikali ione maana kwenye kitabu hiki cha bajeti ambacho kiko hapa, cha 2017/2018 haipo tena, hazijawekwa. Kwa hiyo niiombe Serikali itekeleze na mwisho ni mwezi huu Juni, niiombe sana Serikali ihakikishe inalipa fidia za wananchi wa Makambako, vinginevyo mimi kama Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa leo nitashika shilingi kama nitakuwa sijapata majibu maana kwenye bajeti ya 2017/2018 hakuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Serikali ihakikishe inalipa fidia ya wananchi katika maeneo ya Makambako. Wananchi hao wamekaa kwa muda mrefu, hawawezi kufanya kitu chochote wala kuendeleza wala kufanya kitu chochote katika maeneo yale na Serikali ilisema italipa fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri uko hapa na nilikutana na Waziri wa fedha akanihakikishia tutalipa fidia, nikuombe Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya viwanda uko hapa nimwombe ahakikishe wanasimamia kulipa fidia katika eneo hili la Makambako. Vile vile katika fidia, wako hawa watu wa ujenzi, kuna mradi unaojengwa pale, one stop center ambao unajengwa katika eneo letu la Makambako, vile vile nao wanahitaji kulipwa fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kupitia hili nimwombe sana wahakikishe wanawasiliana pia katika Wizara hii nyingine ambayo kuna fidia mbili hapo, kuhakikisha tunalipa fidia ya Mji wetu wa Makambako ili wananchi wa mji ule waendelee sasa kuwekeza viwanda na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, limezungumzwa kwa uchungu sana suala Liganga na Mchuchuma. Suala hili limezungumzwa kwa miaka mingi, mpaka tunajiuliza kuna tatizo gani sisi watu wa Kusini kule? Kuna tatizo gani na ni uchumi mkubwa katika Mkoa wa Njombe na Kitaifa kwa ujumla, lakini mpaka sasa hatujaona hapa nini ambacho kinaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, alipokuja Waziri Mkuu tumekwenda pale Liganga mwaka huu, wale wawekezaji wametenga hela za kulipa fidia, wale wawekezaji wako tayari na Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema Kamati maalum itaundwa ya kuona je, zile fedha zilizotengwa, bilioni kumi na tatu, zinaendana na fidia ile?

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimuulize Mheshimiwa Waziri, mpaka sasa wamefikia wapi juu ya kulipa fidia ya Liganga na Mchuchuma ili mwekezaji yule aweze kuendelea na shughuli ile kwa sababu fedha zipo? Ni uchumi mkubwa sisi tunaoutegemea sana katika Liganga na Mchuchuma na mwekezaji yule tunamkatisha tamaa maana sasa hatuelewi nini kinachoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana Serikali ihakikishe kwamba inalipa fidia kwa sababu fedha zipo mwekezaji anazo yeye mwenyewe na kuhakikisha wawekezaji wale wanaanza na walikuwa tayari kuanza. Bajeti iliyopita mlituambia mwaka huu wa 2016/2017 mwekezaji ilitakiwa aanze, nini kimechelewesha? Tupate majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, leo katika Wizara hii kwa kweli inafanya kazi nzuri ya kuhakikisha viwanda vinajengwa katika nchi yetu na ndio uchumi. Tukiwekeza kwenye viwanda tutapata ajira na kadhalika. Nakubaliana kabisa Mheshimiwa Mwijage anafanya kazi nzuri pamoja na watendaji wake na Naibu Waziri, lakini nirudie tena, nasema kwa uchungu kabisa, wale watu wa Makambako hivi sasa wako njiani wanakuja, kwa hiyo jioni Mheshimiwa Mwijage anao na Mheshimiwa Waziri Mkuu jioni atatakiwa akutane nao, kwa sababu Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema majibu nitarudi nayo mimi, sasa wanakuja. Nimwombe jioni ahakikishe anakutana na hao watu wa kutoka Makambako.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili linanipa tabu, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu nitakaposhika shilingi juu ya kulipa fidia ya watu hawa mniunge mkono, kabisa, yaani Mbunge mwenzenu napata tabu juu ya watu hawa kulipwa fidia. Kwa sababu kwenye bajeti humu ya mwaka huu hazimo sasa maana yake mpaka mwezi Juni hii zilitakiwa ziwe zimeshalipwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana ndugu yangu Mheshimiwa Mwijage sijui nisemeje, wale watu wananipa tabu kwa kweli. Yaani nakosa raha juu ya kulipa fidia hizi, niiombe sana Serikali yangu. Mheshimiwa Rais alishasema fidia ilipwe sasa nini? Yamechukuliwa makaratasi yote yanayotakiwa ya wale watu, wako 274 yako kwenu Hazina na Mheshimiwa Mwijage anayo.

T A A R I F A . . .

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, unajua tungekuwa tunaelewa kwamba Waheshimiwa Wabunge wote humu ndani tunatekeleza Ilani ya CCM tusingesema hivyo. Wote hapa tunatekeleza Ilani ya CCM ndiyo tuliyopata ridhaa, ndiyo maana naiambia Serikali yangu ya CCM itekeleze Ilani ambayo tulishaiambia. Kwa hiyo wote humu tunatekeleza Ilani ya CCM.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana, nadhani ameelewa humu ndani wote tunatekeleza Ilani ya CCM, ndiyo inayosimamiwa na ndiyo maana tunaiambia Serikali sasa yale mambo ambayo iliahidi iweze kutekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimalizie tu kwa kusema Mheshimiwa Mwijage na watendaji wake, wamenielewa nilichokisema, niombe sana kuhakikisha mpaka Juni, angalau wale watu tuwalipe fidia zao kama ambavyo tulikuwa tumeahidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo haya nikushukuru sana, niishukuru Serikali, nimshukuru Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya. Naunga mkono hoja. Ahsante sana.