Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Mbeya Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nichangie katika Wizara hii muhimu sana ya Viwanda na Biashara. Mimi kama mama na mzazi naomba nichukue fursa hii kuwapa pole familia zote za wale vijana wetu waliofariki pale Karatu, zaidi ya 33 na Mwenyezi Mungu aziweke roho zao mahali pema, peponi.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, Komandoo, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa Kauli Mbiu yake mahiri kabisa ya kwamba ‘Tanzania ya Viwanda Inawezekana’. Amekuja na good spirit ya uchumi wa viwanda na nina hakika kabisa tukimuunga mkono kwa vitendo inawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natoka katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na naelewa kabisa kwamba Serikali haijengi viwanda, Serikali ina-facilitate viwanda. Hata hivyo, pamoja na hayo nataka kujua, Serikali inapoingia katika miradi ya kimkakati kama vile Liganga na Mchuchuma, nime- declare interest mimi natoka mikoa ya huko, lakini Serikali hii haitoi GN (Government Notice).
Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo yake ni kwamba, miradi mingi inasimama. Haijulikani miradi hii itaanza lini? Miundombinu haieleweki, Power Purchase Agreement zake hazieleweki. Namwomba kaka yangu Mheshimiwa Mwijage pamoja na kujieleza vizuri sana, lakini atuletee majibu yenye tija atakapokuja ku-wind up hapa juu ya suala zima la Mradi ule wa Liganga na Mchuchuma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala zima la kodi. Kodi za VAT kwa wawekezaji wenye viwanda nchini ni tatizo kubwa sana. Wawekezaji hawa wanachajiwa VAT kwenye utengenezaji wa bidhaa za ndani, lakini cha ajabu na cha kusikitisha sana ambacho ambacho nashindwa kuelewa mpaka kesho, bidhaa hizi zinazokuwa imported kutoka nje hazina VAT. Sasa nashindwa kuelewa kabisa hapa, hivi tunauwa hili soko la ndani ama tunajenga? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri ni kwenye hizi textile factories, hata hapa Dodoma kwenyewe kuna kiwanda cha gypsum mpaka kimefungwa kwa sababu hozohizo ambazo mimi ninazitoa. Naamini inawezekana kabisa buy Tanzania use Tanzania, tujivunie products zetu za hapa nchini jamani, inawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la hii NEDF (National Enterprenuers Development Fund). Hii pesa Serikali inahitaji iipe Wizara kwa nguvu sana kwa sababu, inasaidia sana kuinua wafanyabiashara wadogo wadogo. Hivyo tunaomba Serikali itilie mkazo suala zima hili la NEDF na hii itasaidia kuleta kile kitu tunaita One District One Product, kwa sababu yote haya yanawezekana tukiwa na mikakati thabiti na yenye tija kwa vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na haya yote mwenzangu pale Mbunge wa Muheza, Mheshimiwa Balozi Adadi amezungumza. Tunazungumzia ukuaji wa viwanda, mimi natoka Mbeya, kule kwetu Mbeya kuna viwanda vingi sana vimekufa yamebaki ni magofu tu. Tunaelewa kabisa ufufuaji wa viwanda uko chini ya TR, lakini pamoja na hayo tunataka Serikali itupe mkakati wa ufufuaji wa viwanda hivi umefikia wapi kwa sababu kule kwetu Mbeya majengo yale yamebaki ni magofu, rasilimali zinapotea bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa haya yote ni suala ambalo halieleweki, tunahitaji Mheshimiwa Waziri hata kama iko chini ya TR tuletee mkakati mzima wa Serikali juu ya ufufuaji wa viwanda ili twende na dhana nzima ile inayosema ukuaji wa viwanda, ufufuaji wa viwanda na ujengaji wa viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mengine ninayozungumza kule kwetu Mbeya Textile ni magofu, Tanganyika Packers magofu, Sijui kutengeneza sabuni vyote hivyo ni magofu, ni magofu, ni magofu! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwenyewe unaelewa, hii ni hasara; hata zana za kilimo; ni hasara kubwa. Rasilimali zetu zinapopotea bure ina maana Serikali yetu hii yenye nia njema ya Awamu ya Tano tunakuwa hatufikii zile ndoto zetu tunazosema ukuaji wa viwanda. Kama ikishindikana worse to worse pia tupate PPP, provided tunaweza kupata ile win win Situation. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, nisigongewe kengele, naunga mkono hoja hii ya Biashara na Viwanda, lakini kaka yangu Mheshimiwa Mwijage akija hapa atuletee majibu ambayo yana tija kwa vitendo. Ahsante sana.