Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE.VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii ili niweze kuchangia machache kwenye hii Wizara yetu ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, ni kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayofanya. Natambua wako baadhi ya watu wanabeza yale mafanikio yanayopatikana, lakini hii ni kwa sababu tu kwamba kila mmoja ana uhuru wa kutoa mawazo yake, ndiyo maana anaweza kuzungumza hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kazi kubwa anayofanya Mheshimiwa Rais, kwanza ya kukusanya mapato, lakini na kusimamia mapato hayo, hiyo tu inaonesha kwamba Rais wetu amedhamiria kuhakikisha kwamba nchi yetu inapiga hatua nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile niendelee kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya. Hata nilikuwa napitia hiki kitabu chake, Mheshimiwa Waziri, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mchango wangu; moja, nataka tu kumkumbusha Mheshimiwa Waziri kuhusiana na Kiwanda cha MUTEX cha Musoma. Kama unakumbuka, kiwanda hiki tumekizungumza kwa muda mrefu, toka mwaka 2005 nazungumzia hatima ya wafanyakazi waliokuwa wa Kiwanda cha MUTEX. Wale wafanyakazi baada ya kile kiwanda kubinafsishwa, hadi leo hawajalipwa haki zao. Kwa hiyo, wengine wako pale, hawana namna ya kuishi. Sasa Mheshimiwa Waziri, kwa sababu hili tumeshalizungumza wote, kesho namsubiri tu kwenye shilingi, kama hajatoa majibu sahihi, basi sina namna ya kuweza kuiachia shilingi yake. Hilo ni la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ni hii Idara au Shirika letu la Viwango (TBS). Sasa hivi huko mjini kuna msako mkubwa unaoendelea na wanafanya kazi ya kuharibu zile bidhaa zote ambazo hazikukidhi viwango.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme jambo moja; zile bidhaa zote ni bidhaa ambazo zinapita katika njia halali, lakini hawa watu wetu wa TBS wanao wawakilishi kule kutoka kwenye nchi husika ambao wana-certify kwamba zile bidhaa zina haki ya kuingia nchini. Sasa zikishafika humu, mtu kalipa na ushuru lakini kinachofuatia, tunasema hizo bidhaa zote zinateketezwa, yakiwemo mfano, mabati na bidhaa nyingine kama hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wakati mwingine unajiuliza, hivi kweli hilo bati hata kama basi makosa yameshafanyika, hilo bati ni gauge labda tuseme 34 badala ya 32, hivi ukililinganisha na nyasi, ni lipi bora? Kwa hiyo, nilidhani unahitaji utueleze una mikakati gani kuhakikisha kwamba zile bidhaa tunazizuia kule kule, kuliko vile ambavyo Watanzania tunaziingiza ndani, halafu zinakuja kutupatia hasara? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, naomba nizungumzie suala la viwanda. Ni kweli kwamba hii nchi uchumi wake unaweza ukajengwa na viwanda. Kwa bahati nzuri, Mheshimiwa Waziri mwenyewe amesema tunavyo viwanda vya aina tatu; viwanda vidogo, viwanda vya kati na viwanda vikubwa.

Waheshimiwa Wabunge wenzangu, mimi binafsi, nisingependa sana tuka-support hivi viwanda vikubwa na ninazo sababu za kimsingi ambazo nasema ni vizuri nguvu zetu tukazielekeza kwenye viwanda vidogo. Kwa bahati nzuri, Mheshimiwa Waziri kwenye page ya tisa, yeye mwenyewe ametoa ushahidi hapa akasema, katika Tanzania asilimia 99.5 ya viwanda vyote nchini ni viwanda vidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeangalia hata katika nchi nyingine, mfano Kenya ni asilimia 98, Malaysia asilimia 97, Ujerumani asilimia 99 pamoja na nchi nyinginezo. Kwa hiyo, huo tu ni ushahidi tosha ambao unadhihirisha kwamba kumbe tunahitaji nguvu kubwa zaidi tuelekeze katika vile viwanda vidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi kuzungumzia viwanda vidogo bila kuzungumza habari ya SIDO. Kwenye page ya 68 Mheshimiwa Waziri amesema hivi; “Shirika la SIDO ndiyo Taasisi ya Serikali yenye thamani ya kuendeleza viwanda vidogo nchini.” Sasa kama hivyo ndivyo, Mheshimiwa Waziri ameizungumzia SIDO nusu page, lakini tunakubaliana kwamba asilimia 99 ya viwanda vya hapa nchini vinapaswa kujengwa au kusaidiwa na SIDO. Kwa hiyo, ombi langu la kwanza ni kwamba hebu tuisaidie SIDO, tuipe uwezo ili iweze kusaidia hivi viwanda vidogo vidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ngoja niwaambie tu jambo moja, kwamba asilimia kubwa ya kazi inayopaswa kufanyika katika viwanda, ni suala la packaging. Labda nitoe mfano mdogo; ukienda hapo sokoni, kuna ile asali imeandikwa “Asali ya Pinda,” tunamshukuru sana Waziri Mkuu Mstaafu kwa kazi nzuri aliyofanya. Robo ya bei ya ile asali ni sawasawa na lita moja ya asali inayotoka Tabora. Hiyo yote ni kwa sababu gani? Ni kwa sababu ya packaging. Kwa hiyo, kumbe tukiendelea kuwasaidia hawa SIDO, maana yake ni kwamba watasaidia watu wetu wengi; kwanza, katika kupata mafunzo ya packaging na zile bidhaa karibu nusu tutaendelea kuzitumia hapa kwetu nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naendelea kushauri zaidi kwamba Mheshimiwa Waziri tuangalie uwezekano wa kuendelea kuisaidia SIDO na kuijengena uwezo. Tena kwa yale mafunzo ambayo wanayapata, yataleta tija zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, juzi tuliona Rais wa Afrika Kusini alipokuja hapa, alikuja na wafanyabiashara wasiopungua 80, lakini kwetu sisi jambo hilo hatulifanyi. Ni ukweli usiopingika kwamba zaidi ya asilimia 80 ya wafanyabiashara ambao tunawafahamu elimu yao kama wameenda sana, ni elimu ya sekondari. Kwa hiyo, ni kwamba viko baadhi ya viwanda vingi wangeweza kuvileta, lakini kwa sababu ya ile exposure ambayo wangesaidiwa, wangeweza kufanya vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, moja kubwa, leo Tanzania hakuna incentives kwa ajili ya viwanda vidogo, isipokuwa ipo kwa ajili ya viwanda vikubwa. Kwa hiyo, nadhani hilo nalo Serikali ilipaswa iliangalie, ione namna ya kuwasaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nawashukuru sana na naunga mkono hoja.