Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kujadili bajeti hii ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Nami nianze kwa kuwapa pole wale wote ambao wamepata majanga mbalimbali yakiwemo haya ya ajali ambazo zimewakumba watoto wetu kule Arusha, lakini na zingine mbalimbali ambazo zimetokea.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nitumie fursa hii kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Baraza lake lote la Mawaziri kwa jinsi wanavyotutendea haki kwa jinsi sisi wawakilishi. Kipekee niipongeze Wizara hii na hasa Waziri wake Engineer Lwenge pamoja na Naibu, Katibu Mkuu wake kwa kutukumbuka sisi wana Tabora.
Sisi Tabora kwa muda mrefu tumekuwa na matatizo ya maji na tatizo hili tumekuwa tukiliimba hapa kila mara na hata waliotangulia ni tatizo lililokuwa sugu. Sisi wana Tabora tunaendelea kusema tunaomba mtufikishie salamu za shukrani kwa Mheshimiwa Rais kwa kutimiza Ilani na Sera za Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo pale Tabora kwenye upande wa maji juzi juzi tu tumetoka kushuhudia mkataba wa mradi wa Ziwa Victoria wa bilioni 600 ambazo zimesemewa semewa hapa; nazidi kuishukuru Serikali. Pia siku chache zilizopita Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan alikuwepo pale kwa ajili ya kuzindua mradi wa maji kule Mabama Mkoani Tabora. Tunasema ahsante Serikali kwa kuijali Tabora.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna matatizo ya maji ambayo kwa kutumia lile ziwa moja la Igombe maji yetu yamekuwa hayana uhakika na hasa yamekuwa ni maji machafu ambayo hata rangi yake mara nyingi utaona ni ya kijani. Sasa tumepata fursa hii tunasema ahsante. Hata hivyo, nitakuwa sijaitendea haki nafsi yangu na hata wananchi wa Tabora kama sitazungumzia hili lililojitokeza leo kwa baadhi ya Wabunge wenzetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Mbunge mwenzetu tena naomba ku-declare interest kwamba nipo naye kwenye Kamati ya Miundombinu, bahati mbaya hayupo hapa, Mheshimiwa Kitwanga, alizungumzia suala la kwa nini ule mradi wa Tabora umepewa hela nyingi kiasi hicho, amesahau kwamba Tabora ilikuwa imesahaulika miaka mingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, napata mashaka Mheshimiwa ambaye ameshakuwa hata Waziri, kauli alizozitumia hapa hazipaswi kabisa kutumiwa na mtu yoyote ambaye ni kiongozi wa Serikali, ambaye amewahi kuwa kiongozi wa Serikali na pia ni Mbunge. Unapo sema kwamba mradi ule umepita kwao, kule Kolomije na kwamba mradi ule kwa kuwa unakuja Tabora, yeye yuko tayari kuhujumu mradi ule kuzima mitambo. Kwanza huu ni uasi, lakini si tu uasi ni kuchochea mambo ambayo katika nchi yetu hatujayazoea kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyofahamu kuna miradi mingi imepita nchi hii ambayo haijawanufaisha watu ambao wanaokaa maeneo yale, kwa mfano mradi wa REA, hata nguzo za umeme zinapita mahali pengine ambapo watu hawapati mradi huo, lakini sijawahi kusikia wakisema watang’oa nguzo za umeme. Sasa yeye akisema yuko tayari ule mradi aweze kuzima zile mashine huu ni uchochezi ambao haukubaliki kabisa. Pia unaposema kwamba mimi nikiwa Waziri kule ndani nilikuwa sisemi nitasema nje anataka kutupa message gani? Kwamba wakiwa kule ndani wanakuwa waoga? Sidhani kwamba lile suala linapaswa kuzungumza namna hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kutokana na mradi huu, kuna Mheshimiwa Mbunge mwingine ameongelea mpaka mchakato wake wa mradi wa maji wa Tabora kwamba mchakato wake ana taarifa kwamba haukwenda vizuri na kwamba kulikuwa na waombaji watano na kwamba wengine hawakutendewa haki. Nashangaa pilipili usiokula inakuwashia nini?
Sisi ambao ndio wenye mradi ule tunaona kila kitu kimekwenda vizuri na ule mradi tayari na ule mradi tayari umesainiwa na watu sasa hivi karibu wanaanza kazi. Atuachie sisi wana Tabora tuamue kwamba wale waliopewa ule mradi hawapaswi kuwa na ule mradi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Tabora tuna tatizo moja wakati tuanasubiri huo mradi wa Ziwa Victoria. Tabora ile mamlaka yetu ya maji TUWASA imekuwa na madeni makubwa wanaidai Serikali zaidi ya shilingi bilioni 3.3 ambazo ni malimbikizo ya madeni ya muda mrefu. Sasa naiomba Serikali, ili kuwe na ufanisi na ile Mamlaka ya Maji Tabora, basi deni hili lilipwe ili angalau tuweze kuwa na huduma ya maji ya uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, wanasema asiyeshukuru kwa dogo hata kwa kubwa hawezi kushukuru. Mimi kwa upande kwa Mkoa wa Tabora kwa hapa ambapo Wizara na Serikali yetu imetufikisha kwenye suala la maji, niendelee kuipongeza Wizara pamoja na Chama chetu cha Mapinduzi kwa sababu tunatekeleza sera yake na Ilani pamoja na ahadi mbalimbali zilizoahidiwa kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante.