Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza kwa kuchangia kuhusu bajeti. Bajeti kwa kweli ni ndogo na inashangaza kabisa. Tunasema kuwa maji ni uhai na kila mmoja anajua kuwa maji ni uhai. Maji ni uhai kwa binadamu, maji ni uhai kwa kila kiumbe na maji ni uhai kwa viwanda ambavyo tunasema tunaenda kwenye Tanzania ya Viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, bila ya kuwa na maji ya kutosha hatuwezi kuendeleza haya mambo mazuri ambayo tunayopanga. Bajeti ya mwaka huu ni ndogo ukilinganisha na ya mwaka wa jana, nawaomba Waheshimiwa Wabunge kila mmoja atakayesimama aiongelee hii bajeti kusudi tuweze kuiongeza na kufikia angalau ya mwaka wa jana ili tuweze kufikia malengo mazuri ya mwaka 2021 ya kuwa na maji ya kutosha na kuweza kumtua mwanamke ndoo kichwani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo naomba kuongelea ni tozo. Mwaka wa jana tuliongelea kwamba tozo kwa ajili ya Mfuko wa Maji iwe sh. 100, lakini haikupitishwa. Sasa hivi nazidi kuongelea zaidi na zaidi na naungana pamoja na Kamati ya Kilimo na Maji kusudi iweze kufikia lita moja ya diesel na lita moja ya mafuta ya petrol kuwa sh. 100. Kwa namna hiyo tutakuwa tumekuza Mfuko wa Maji. Vijijini akinamama wanapata shida sana na hata watoto wa kike ambao ndio wanatumika kuchota maji hawaendi mashuleni kwa sababu ya kutafuta maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 70 ya fedha ambazo zitakuwa zimekusanywa tuzipeleke huko vijijini na asilimia 30 ziweze kupelekwa mijini. Kwa nini nasema hivi, ni kwa sababu mijini kuna miradi mingi ya maji na wafadhili ni wengi ambao wanafadhili mijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukipata maji safi na salama tutaweza kupunguza magonjwa nyemelezi hasa ya tumbo, kwa mfano kipindupindu ambacho kimekithiri kwenye miji yetu pamoja na kuhara kwa tumbo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuongelea juu ya Halmashauri zetu. Kwenye Halmashauri zetu ilikuwepo sheria ndogo ya uvunaji maji, naomba sheria hii irudishwe kwenye hizi Halmashauri zetu. Kama haipo kwenye Halmashauri nyingine itungwe na kama kwenye Halmashauri nyingine ipo isimamiwe vizuri sana kusudi wananchi waweze kuvuna maji kwenye nyumba wanazojenga na pia kwenye mabwawa ambayo watakuwa wameyatengeneza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukipata maji safi na salama tutakuwa tumepunguza mambo mengi. Tutakuwa tumeimarisha afya yetu na familia na wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu fedha za maendeleo. Tunapanga fedha za maendeleo na zinapitishwa vizuri sana, lakini ukiangalia haziji kama tunavyopanga. Kwa mfano mwaka jana fedha za maendeleo ambazo zimetolewa ni aslilimia 19.8 tu kwa upande wa maji na upande wa kilimo cha umwagiliaji ni asilimia 8.4 tu ambazo zimetoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, bila ya kuwa na fedha za maendeleo miradi yetu yote ambayo tutakuwa tunapanga haiwezi kukamilika, ndiyo sababu unakuta tuna miradi mingi viporo. Kwa mfano miradi mingi ya Benki ya Dunia bado haijakamilika kwa sababu fedha tunazotenga hazitoshi na hazitoki.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha zote za ndani hasa ndizo zinazopaswa kutoka kwa sababu fedha za ndani tunakuwa na uhakika nazo. Kwa mfano, mwaka huu, Serikali imetenga asilimia 66 ya fedha za maendeleo za ndani. Kwa hiyo naiomba Serikali, kuwa hizi fedha ambazo zimetengwa tuzisimamie na kwa sababu ni za ndani tunaamini kuwa zitatoka; fedha hizi ziweze kutoka ili zikamilishe miradi yetu ambayo tutakuwa tumetenga.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kilimo cha Umwagiliaji. Hatuwezi kusema kuwa tutaweza kufanikiwa katika kilimo kwa kutegemea mvua na kwa kutegemea jembe la mkono. Kwa hiyo naomba Serikali yetu, kwamba miradi mizuri iliyopangwa ikiwemo ya Mkoa wangu wa Morogoro, kama ile ya Mikula pamoja na miradi mingine, itekelezwe kusudi tuweze kutoka kwenye hekta 468.338 mpaka kwenye hekta milioni moja mwaka 2021. Ukame ulitunyemelea kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi, nyote mnajua. Nchi zote zilizoendelea zinatumia kilimo cha umwagiliaji pamoja na kulima kwa matrekta.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mfumo wa Umwagiliaji. Nashauri; kwa sababu hela tunazotenga hazitoshi na hazitoki kutoka Hazina; kwamba uanzishwe Mfuko wa Umwagiliaji. Tukiwa na Mfuko huu tutakuwa na uhakika kuwa hela tunazotoa kwenye mfuko huo tunaweza kulima na kupata chakula cha kutosha na hivyo tutapata chakula cha uhakika kwa mwaka mzima na tutainua lishe yetu, hasa Mkoa wetu wa Morogoro pamoja na Tanzania kwa ujumla, ambapo sasa hivi tuna utapiamlo unaokaribia asilimia 34 ambayo si nzuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili tufanikiwe kwenye kilimo cha umwagiliaji lazima tuwe na watalaam. Hata hivyo, mpaka sasa hivi tuna watalaam wachache; engineers, surveyors ni wachache sana kwa upande wa kilimo cha umwagiliaji. Kwa hiyo, naomba kuiuliza Serikali, je, ina mkakati gani? Kwa sababu tuna vyuo vichache vinavyotoa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia naomba mradi wangu wa Chalinze namba..
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda wako umemalizika
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante