Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunipa afya ambayo ndiyo nyenzo muhimu katika ufanyaji kazi wa kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa imani yake aliyoonesha kwangu kwa kuniteua kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye Ulemavu. Nasema ni heshima kubwa sababu nafahamu changamoto iliyoko miongoni mwa jamii ya watu wenye ulemavu. Namwahidi sitomwangusha, nitafanya kazi kwa uadilifu mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake thabiti. Namshukuru pia kwa miongozo yake ya kila siku, ambayo siyo tu kwamba imetupa ari lakini imetujenga katika uongozi na naamini ni Waziri Mkuu imara na Wanaruangwa wamepata mwakilishi mzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri wa Nchi, Mheshimiwa Jenista Mhagama na Naibu Waziri mwenzangu, Mheshimiwa Antony Mavunde. Kutoka kwa hawa wawili nimejifunza kwamba umoja ni nyenzo muhimu katika kutatua changamoto mbalimbali na nafahamu kwamba Wanaperamiho na Wanadodoma Mjini wamepata Wawakilishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakupongeza wewe na kukushukuru pia kwa ushirikiano wako uliotupa siku zote tulizokuwa hapa Bungeni. Nawapongeza Mawaziri na Waheshimiwa Wabunge wote. Sasa kwa mujibu wa kanuni 99(2) ya Kanuni za Bunge, Toleo la mwaka 2016 nijibu baadhi ya mambo mbalimbali yaliyoongelewa kuhusu watu wenye ulemavu. Nitayajibu kwa ujumla wao kwa sababu baadhi ya mambo yamerudiwa rudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zimetolewa hoja kuhusu elimu katika mambo mbalimbali. Niseme tu, tayari Serikali inatambua umuhimu wa elimu kwa watu wenye ulemavu, jitihada zimekuwa zikifanywa. Binafsi nimefanya ziara katika maeneo mbalimbali, nimeona kuna dalili njema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi yangu itazidi kuwasiliana na Wizara ya elimu ili kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu wanapata elimu sawa na watu wengine, katika suala hilo hilo la elimu limezungumziwa jambo linalohusu Vyuo vya Elimu ya Ufundi kwa Watu Wenye Ulemavu. Ni dhima ya Serikali kuboresha elimu katika Vyuo hivi hasa kupitia Program ya Kukuza Ujuzi inayosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu. Niseme tu, haya hayataishia hapa. Vyuo vingine vyovyote vinavyotoa Elimu ya Ufundi, vina jukumu pia la kuhakikisha elimu yao ni shirikishi na tutaendelea kushirikiana na Wizara ya Elimu ili Vyuo vya VETA pia viweze kutoa elimu shirikishi kwa watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, limeongelewa pia suala la ajira. Niseme tu Sheria Na. 9 ya mwaka 2010, lakini pia na Sheria ya Ajira ya Employment and Labour Relations Act vinazungumzia kuhusu ajira kwa watu wenye ulemavu. Niseme tu na nikumbushe kwamba ni marufuku kwa mujibu wa sheria zote hizi mbili, mtu kuachishwa tu kazi eti kwa sababu ya ulemavu. Ukweli ni kwamba waajri wana jukumu la kuweka miundombinu na kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyakazi wenye ulemavu, yaani kwa Kiingereza ni reasonable accommodation. Kwa hiyo, natoe tu wito kwa watu wenye ulemavu kulizingatia hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, limeongelewa pia suala kuhusu majengo ya umma (accessibility). Ofisi yangu imeshaanza kuwasiliana na itaendelea kuwasiliana hasa na TAMISEMI lakini pamoja na Idara na Taasisi nyingine za Serikali ili kuhakikisha kwamba majengo ya umma yanafikika kirahisi kwa watu wenye ulemavu. Hili ni suala la kisera lakini pia ni suala la kisheria lipo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo inatekelezwa na Serikali iliyoko madarakani kwa sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yamezungumziwa pia masuala yanayohusu mauaji wa watu wenye Ualbino, niseme tu hili ni suala ambalo lilianza toka miaka ya 2006. Nashukuru Mungu kwa sasa limepungua, lakini nafahamu suluhisho thabiti la mauaji haya ni watu kuondokana na imani potofu. Watu mara nyingi wanaangalia hili suala kwa uchache wanafikiri ni ushirikina, lakini tunakwenda mbali zaidi, tatizo kubwa ni binadamu kufikiria kwamba mtu mwenye Ualbino ni mtu tofauti. Once imani hiyo inapotoka, basi usalama sahihi ndiyo utapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inashirikiana na wadau mbalimbali na itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuwa na mpango madhubuti wa kuondoa unyanyapaa na tayari tuko katika stage za awali za kuandaa mpango huo ambao once ukifanikiwa baada ya miaka mitano tuna uhakika hali itakuwa nzuri ili wale wanaoishi katika vituo maalum, sasa waweze pia kujumuika na wenzao kwa sababu tunafahamu ni kinyume cha sheria, ni kinyume cha haki za binadamu kwa watu kuwekwa kwenye makambi pasipo sababu maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia limezungumziwa suala la kodi na incentives mbalimbali kwa watu wenye ulemavu. Hili ni wazo zuri na teknolojia inapoendelea, inarahisha mambo mengi. Haijaandikwa popote kwamba chombo cha usafiri cha mtu mwenye ulemavu kiwe ni bajaji peke yake. Kwa hiyo, pale ambapo ataweza kuendesha gari, basi Ofisi ya Waziri Mkuu itawasiliana na Wizara ya Fedha ili kutengeneza utaratibu maalum kwamba yale magari ambayo yatakuwa ni nyenzo nzuri ya kujongea kwa watu wenye ulemavu, basi incentives zipatikane. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia utaratibu kwa sababu nafahamu experience ya nchi nyingine, utaratibu huu ulikuwa abused kwa mara ya kwanza, lakini walijitahidi wakaweka sawa. Kwa hiyo, ni wazo zuri na tutaendelea kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine hapa ambalo kidogo itabidi nilielezee kwa kirefu ni kuhusu makazi ya Watu Wenye Ulemavu. Hoja zilizotolewa, yaliitwa makambi, sidhani kama ni lugha nzuri sana, ni Makazi ya Watu Wenye Ulemavu. Haya yana historia ndefu; yalikuwa ni makazi ya wazee na wasiojiweza na watu wenye ulemavu na ukiangalia historia yake hasa, yalianza kuwatunza waathirika wa ugonjwa wa ukoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba dhamira ya Serikali hasa ukizingatia sheria na mikataba mbalimbali ya haki za binadanu na hasa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu wa mwaka 2006 ni kuhakikisha kwamba mtu mwenye ulemavu anashiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii na siyo kuwekwa kwenye makambi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu pia kutokana na changamoto mbalimbali, wapo watu wachache kwa namna moja au nyingine watahitaji msaada fulani. Kwa hiyo, niseme tu kwa wale wanaoishi katika makambi haya kwa sasa Serikali itajitahidi kuyaboresha makambi haya, tayari tulishaanza mawasiliano na Wizara ya Ardhi ili kuzuia uvamizi katika baadhi ya haya maeneo na huduma nyingine zimendeelea kuboreshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, dhima kuu ni kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu wanaishi katika jamii shirikishi. Kwa hiyo, nikumbushe tena, Halmashauri zina wajibu wa kuwasaidia watu wenye ulemavu ambao hawana msaada lakini jamii pamoja na familia kisheria vyote hivi vina jukumu la kuwasaidia na kuwatunza watu wenye ulemavu ambao watahitaji msaada. Ila kwa hali halisi ni kwamba suala la ulemavu ni suala mtambuka na watu wenye ulemavu wana haki ya kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia limeongelewa suala la kuwezesha watu wenye ulemavu kiuchumi. Niseme tu kwamba kuna baadhi ya mambo kwa kweli yanahitaji tu kubadilisha namna ya kufikiri.
Kwa mfano, tunapozungumzia asilimia kumi ya bajeti ya maendeleo ambayo inakwenda kwa vijana na akinamama katika Halmashauri mbalimbali, hakuna kikwazo chochote cha sheria kwa Mtendaji wa Serikali kutoa kipaumbele maalum kwa watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niweke msisitizo tu na niseme kwamba kwa sababu watu wenye ulemavu ni watu ambao waliachwa nyuma kwa muda mrefu na kwa sababu affirmative action (kipaumbele maalum) kimekuwa ni jambo la kawaida cha kuwakwamua watu walioachwa nyuma kwa muda mrefu, imefanywa hapa katika jinsia lakini hata katika zile nchi ambazo zili-suffer ubaguzi wa rangi, yalifanywa hivyo kwa makundi maalum yaliyobaguliwa kutokana na hali zao. Hivyo basi, kutokana na Sheria ya Watu Wenye Ulemavu na Katiba ya Nchi na Mikataba mbalimbali na sera nitoe maagizo tu kwa Watendaji wote wa Serikali, sasa kutoa kipaumbele kwa watu wenye ulemavu siyo option kwa sababu ni suala la lazima ili kuhakikisha kwamba usawa halisi kwa watu wenye ulemavu unapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niseme tu kwamba, naunga mkono hoja na niwatakie heri Mawaziri wote na Viongozi wote wa Serikali katika kuchapa kazi, waendelee kufanya kazi vizuri. Nitoe ushauri tu kwa wenzangu wa upande wa pili, wapo watu wanaosema kwamba utakuwa una busara sana if you try to hide a bit of your stupidity. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja.