Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kuchangia naomba tu niwaulize hawa Mawaziri wa Maji, hivi ni kwa nini ninyi hampewi hela? Kuna tatizo gani? Labda wakitueleza tutatoka hapo tukajua tuwasaidie vipi, kwa sababu tunajua sekta ya maji ni sekta muhimu, lakini ukienda kwenye pesa walizopewa za maendeleo ni asilimia 19.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunakaa hapa tunajadili, tunafanya nini, lakini mwisho wa siku utekelezaji finyu, kwa hiyo, wakati wanakuja kujibu watueleze kwa nini Wizara ya Maji haipewi pesa za kutosha?

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo ni lazima nichangie tu. Kuhusu Mfuko wa Maji, naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba, pesa ziongezwe kwa ile tozo kutoka shilingi 50/= kwa lita mpaka shilingi 100/=, lakini katika kuongeza huko naomba ile pesa ikiongezwa ikafanye jambo lililokusudiwa. Sisi lengo letu watu wa vijijini wapate maji, angalau ile pesa asilimia 70 ikatumike vijijini ili kuwawezesha akinamama wa vijijini wapate maji; isiwe kwamba ile pesa ichukuliwe ikafanye mambo mengine kama administration na vitu kama hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Mto Ruvuma. Mimi Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa kuhitimisha hii hoja naomba aje na majibu. Kila siku wanatwambia mkandarasi yuko site anafanya hivi, anafanya hivi. Tunataka tupate jibu la uhakika, pesa ya kufanya huu mradi ipo ama haipo? Swali la kwanza. Hata hivyo, pale unapopita mradi wamewaambia watu wasiendeleze, lakini mpaka leo hakuna fidia yoyote waliyolipwa? Watu wale mnawaachaachaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii Serikali ya China na Serikali ya Tanzania kwenye mradi huu tunaomba sisi watu wa Mtwara tupate maelezo ya kina kwa sababu mradi huu ukikamilika, kama kweli tunasema tunaitaka Mtwara ya Viwanda maji haya yatatusaidia kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye Manispaa ya Mtwara Mikindani; pale maji yapo ya kutosha, tatizo miundombinu. Miundombinu ya tangu mwaka 47 wakati watu wanavaa kaptula badala ya suruali ndiyo hiyo hiyo iko mpaka sasa hivi, haitoshelezi. Huwezi kuamini watu wa Mtwara Mjini kuna watu wengine ukienda mitaa ya Komoro wanachota maji, kule kwetu tunaita ya kuokota; unasubiri mvua inyeshe unachimba kisima unachota, hiyo ndiyo Manispaa ya Mtwara Mjini. Sasa nafikiri kuna haja ya makusudi kabisa Mheshimiwa Waziri wa Maji atueleze mikakati thabiti ya kuitekeleza ili kusudi tuepukane na matatizo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia Mkoa wa Mtwara kwa matokeo ya elimu kila siku ni karibu unashika nafasi za chini; kwa mfano mwaka jana shule tisa katika 10 za mwisho zimetoka Mkoa wa Mtwara kwenye mtihani wa form two; na waathirika wakubwa ni watoto wa kike. Wanaathirika kwa sababu, pamoja na mambo mengine maji hakuna, wanatumia muda mwingi kwenda kutafuta maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa cha kusikitisha Mheshimiwa Rais ametoa amri ya Kata Umeme. Kweli umeme umekatwa, umekatwa mpaka kwenye vyanzo vya maji, ukienda kwenye Mradi wa Makonde umeme umekatwa, wananchi wamehangaika maji hakuna.

Sasa najiuliza mwananchi wa kawaida akipelekewa maji nyumbani kwake bili analipa, wale wanaenda kukata umeme kwenye chanzo ambacho maji yale wanaowadai si wananchi wa kawaida; wanadai Jeshi, wanadai Polisi, wanadai Hospitali, lakini wanaenda kukata maji ambayo wananchi wote hawapati; wanaenda kukata umeme kwenye ule mtambo ambapo unasababisha wananchi wengine huku wote wasipate maji, hata wale ambao wanalipa bili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hilo hilo la kukata maji; kwa mfano ukienda katika Manispaa ya Mtwara Mikindani watu wa maji wanadai sana madeni. Ukiangalia wanadai Jeshi, wanadai Polisi, wanadai Hospitali, lakini na wao kwa sababu hawalipwi, wanadaiwa umeme! Ikafikia stage wakakata maji Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Ligula siku nne. Niambie yule mama yule tunayemtaka akajifungue, yule mtoto anayeumwa anatibiwa katika mazingira gani? Mpaka maabara ilifungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya mambo mimi nayaongea kwa uchungu sana kwa sababu wale watu wanateseka tatizo sio la kwao, tatizo la Serikali hii hampeleki hela za kulipia hizi huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Umwagiliaji. Naomba nipate maelezo ya kina, inavyoonekana issue ya umwagiliaji kwetu si kipaumbele. Sasa kama si kipaumbele watu wakilalamika njaa msiwazuie waacheni waseme, kwa sababu nina mfano. Kuna Skimu ya Umwagiliaji Mtwara Vijijini katika Bonde la Mto Kitere, ile skimu ilifunguliwa na mbio za mwenge mwaka 2014, lakini cha ajabu sijui walifungua kitu gani. Ndiyo maana sometimes tunasema mwenge tuuweke makumbusho! Walienda pale wametumia hela chungu nzima, wamefungua, lakini hakuna kinachofanyika. Sasa walifungua ili iweje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bonde lile likitumiwa vizuri sisi watu wa Mikoa ya Kusini naamini hatutahangaika kwenda kufuata mchele Ifakara, hatutahangaika kwenda kufuata mchele Mbeya. Mheshimiwa Waziri anakiri kabisa kwamba miradi mingi ya umwagiliaji ilifanyika kifisadi.

Sasa tunamwomba afanye jitihada za makusudi kuhakikisha miradi ile inafanya kazi na wale watu ambao walihusika katika kuhujumu miradi ile wachukuliwe hatua za kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, magonjwa mengi, karibu asilimia tisa ya wagonjwa wanaolazwa hospitali matatizo yao yanatokana na kutumia maji ambayo si safi na salama. Serikali inatumia pesa nyingi kutibu watu wetu. Kwa hiyo, ushauri wangu tuwekeze kwenye maji kwa sababu tutapunguza kutibu watu na kuwafanya watu wakose vizazi, kwa sababu haya magonjwa ya UTI na nini yanaenda kusababisha watu wengine wakose vizazi kwa sababu, vinakuwa vinapata matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia suala la uvunaji wa maji ya mvua, nafikiri wenzangu wengi wameliongea, tuweke msisitizo kabisa, tuweke mkakati maalum kama tunavyofanya mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.