Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia kuwa na afya njema na kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Maji. Vile vile nami niungane na Wabunge wenzangu na Watanzania kwa ujumla kutoa pole kwa wazazi, ndugu, jamaa na marafiki ambao watoto wao wamefariki katika ajali kule Mkoani Arusha.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo pia natoa nyingine kule kule Arusha, kama tulivyoona katika vyombo vya habari kuwa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha mti umeanguka na msiba mwingine umetokea wakiwemo watoto wamefariki. Pia nitumie fursa hii kutoa pole za dhati kabisa kwa wananchi wangu wa Jimbo la Tanga kwa mafuriko makubwa yaliyotokea ambapo yamesababisha uharibufu wa mali, maisha na vile vile pia madaraja yamekatika na kukata mawasiliano kati ya mji wa Tanga na Pangani na vilevile Lushoto na Tanga Mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nianze kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kitabu cha Mwenyenzi Mungu cha Qurani kwenye Surat Anbiyaa aya ya thelathini Mwenyezi Mungu anasema wajaalna minal-mai kul shaiyn hai; kwamba ametujalia sisi binadamu kwamba maji ni uhaki kwa kila kitu. Utaoa ni namna gani Mwenyezi Mungu mwenyewe ametoa umuhimu kwa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, maji hayana mbadala, umeme ukikatikaunaweza ukaweka kibatari, lakini maji yakikatika hakuna mbadala. Kwa hiyo, naitaka Serikali ijue kwanza umuhimu wa maji kwa maisha ya binadamu. Vile vile mahitaji ya si kwa binadamu tu, wanyama, wadudu, ndege na kadhalika na kadhalika wote wanahitaji maji; mpaka vyombo vya moto tunavyovitumia pia vinahitaji maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa inashangaza Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya maji na mifugo kupunguza bajeti ya maji kutoka Shilingi za Kitanzania bilioni mia tisa thelathini na tisa na kurudi chini hadi bilioni 623, hilo jambo haliingii akilini hata kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nami niungane na Mheshimiwa Zitto Kabwe na Waheshimiwa Wabunge wengine waliosema kwamba bajeti hii irudi ili ikarekebishwe iongezwe; kwamba kutoka shilingi milioni mia sita za mwaka 2017/2018 ipande. Haiingii akilini kwamba ikiwa maji yanamhusu kila mtu lakini bajeti tunaipunguza wakati ndiyo sehemu muhimu katika maisha ya binadamu. Kwa hiyo naungana na wale wote waliosema kwamba bajeti hii irudi na ikongezwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, siishii hapo. Jambo lingine kwenye suala zima la maji, sasa hivi maji katika baadhi ya mikoa kwa mfano katika jimbo langu bei ya maji sasa hivi imekuwa ghali kuliko umeme; na wananchi wanahitaji maji kwa shughuli za kimaendeleo lakini maji yamekuwa hayapatikani kama yanavyokusudiwa. Pia katika jimbo langu siku za karibuni maji yamekuwa ni machafu kuliko maelezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namtaka Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa; nilitoa mwongozo siku moja akasema alikuwa hana habari; sasa nataka pia anijibu kupitia majibu yake kwamba amegundua nini mpaka Tanga iliyokuwa na historia ya maji safi kabisa leo yanatoka machafu kama chai ya maziwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ninalotaka kulizungumzia ni miradi ya maji vijijini. Miradi ya maji vijijini Serikali imepata ufadhili wa Benki ya Dunia, sasa kinachotushangaza Benki ya Dunia wametoa fedha kwa nini miradi ile haikamiliki? Kwa mfano mimi nina miradi ya vijiji kumi, kuna mradi unaoelekea kaskazini na kuna mradi unaelekea kusini.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mradi wa Kaskazini maji yameishia sehemu moja inaitwa Mabokweni ambayo ndiyo jina la kata vile vile; lakini mradi unatakiwa ufike mpaka Kata ya Chongoleani kwenye Vijiji na Vitongoji vya Mpirani, Kibafuta, Mchanga Mweupe, Mchana Mwekundu, Putini, Helani hadi Chongoleani kwenyewe na kufikia Bagamoyo; lakini mradi kule Mkandarasi ameondoa mpaka vifaa anasema anaidai Serikali na hajalipwa fedha zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa napata kigugumizi hapa kujiuliza, fedha tunaambiwa zimeletwa na benki ya dunia kwa nini mradi haukamiliki na wananchi wanapata shida? Wameeleza wengi hapa; akinamama kule Tanga wamekuwa na vipara kama wanaume kwa kubeba ndoo za maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa Mawaziri nao ni watoto waliozaliwa na mama, binadamu wote wamezaliwa na mama, kwa nini basi hata kama wao hawana huruma, wangewaonea huruma hawa akinamama ambao ndio waliotuleta sisi hapa duniani. Maji ni bidhaa muhimu katika maisha ya kila siku ya binadamu. Kwa hiyo, namtaka Mheshimiwa Waziri, hili la kwamba bajeti irudi ili iongezwe alizingatie.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine linahusu miradi ya maji vijijini; baadhi ya contractors wa miradi ile ya maji wamefikishwa mahakamani kwa sababu na wao wamekopa materials ili wakaendeleze ile miradi, hawajalipwa na Serikalini kwa kwa muda mrefu kumekuwa kuna ubabaishaji hapa. Naomba hilo pia Mheshimiwa Waziri atueleze kwa nini wakandarasi wale wa maji hawalipwi na ikiwa fedha za World Bank zimetoka na wao kwa kuisaidia Serikali yao lakini wanapelekwa mahakamani kwa kuwasaidia wananchi wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfumo wa Maji Taka. Wamesema wazungumzaji wengi hapa kwamba hata mifumo ya maji taka katika mikoa yetu, majiji yetu na manispaa zake si mizuri na lazima tujue tukiwa na mfumo mbaya wa maji taka ndicho kinakuwa chanzo kikubwa cha malaria. Kwa sababu kama utakuwa na mfumo nzuri wa maji taka maji yatakakuwa hayasimami, hayatuami, yatakuwa yanakwenda ambapo mbu hawatoweza kuzaliana.

Mheshimiwa Naibu Spika, maji taka yanayotuama na kumwagika hovyo kwanza yanaharibu mandhari ya miji yetu lakini pia harufu na pia kusababisha magonjwa ya milipuko kama kuhara na kutapika. Kwa hiyo, lazima wizara inayohusika ihakikishe inatilia nguvu ama kwa kutafuta wafadhili au kupeleka fedha pia katika miradi ya maji taka.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo wananchi wanahitaji kuwekewa mfumo wa majitaka kwa mfano katika jiji letu la Tanga lakini Mamlaka ya Majisafi na Majitaka hawana uwezo, wanasema tu tuna uwezo wa kukarabati si kuanzisha miradi mipya ya mifumo ya majitaka. Naitaka Wizara pia ipeleke fedha katika Mamlaka ya Majisafi na Majitaka kwa Jiji la Tanga ili iweze kuweka mfumo wa maji taka na hivyo tuondokane na maradhi ya milipuko pia na masalia ya mbu yanayosabisha malaria.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninalotaka kuzungumzia katika suala la maji ni kwamba maji katika Halmashauri ya Tanga ilikuwa ni historia. Halmashauri nyingi na Waheshimiwa Wabunge watakuwa ni mashahidi hapa walikuja kujifunza ku-treat maji kutoka Mamlaka ya Majisafi na Majitaka ya Tanga. Leo wananchi wanapata tabu mpaka maji yanatoka machafu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile pia nimuulize Mheshimiwa Waziri kupunguza bajeti haoni kwamba hili ni tatizo? Leo tuna miaka 56 ya uhuru maji wanayokunywa wanyama wa porini ndiyo hayo hayo maji wanayokunywa binadamu. Yapo baadhi ya maeneo unakuta watu wanachota maji kwenye madimbwi ya barabarani au kwenye mifereji pembeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii hali ni mbaya, haiingi akilini nchi kama Tanzania iliyojaliwa raslimali lukuki lakini tunashindwa kusimamia hata maji; mimi nasema hili jambo ni la aibu sana. Lazima Mheshimiwa Waziri aliyepewa dhamana utuletee mfumo mpya; pamoja na kurudi na bajeti lakini ukija uje na mikakati mipya ya kuwasaidia wananchi wetu wa vijijini. Sote hapa tunatokea vijijini lakini kama vijijini kutakuwa hakuna maji safi na salama ina maana watu wote watazidi kuathirika na maradhi yataongezeka.