Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. SEIF K.S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia leo katika Wizara hii ya Maji na Umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipotoa shukrani zetu hasa kwa watu wa Manonga, Wilaya ya Igunga ama Mkoa wa Tabora kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, lakini pia kwa Wizara ya Maji na Umwagiliaji hasa baada ya kusaini ule mkataba wa maji ya Ziwa Victoria Mkoani Tabora hivi karibuni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini mradi huu wa maji ya Ziwa Victoria unaenda kupunguza uhaba ama tatizo la maji hasa kwa wananchi wetu ambao ni wa hali ya chini sana. Mradi huu katika kupita utapita katika maeneo ya vijijini, kwa hiyo vijiji ambavyo vitapitiwa na mradi ule vitapata maji. Hii yote ni shukrani kwa Mheshimiwa Rais kwa kuamua kujitoa kwa hali na mali kuhakikisha kwamba analitatua tatizo hili la maji katika maeneo ambayo yalikuwa yana shida ya maji kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme, mradi huu wakati unakwenda pale Igunga maeneo kama Ziba, Ibologelo, Nyandekwa, Ndembezi pamoja na Kata zilizopo jirani pale maana ni kilometa kumi na mbili yatapata maji ya Ziwa Victoria. Vile vile naamini mpaka Nkinga pale kwenye Hospitali yetu ya Rufaa maji yatafika kwa sababu ni Hospitali ya Rufaa ambayo inatoa huduma maeneo mbalimbali, maji na wao watapata.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo maji ni uhai na kama alivyosema Mheshimiwa aliyetoka hapa bila maji huwezi kufanya mambo yoyote, lakini kwa programu hii namshukuru sana Mheshimiwa Rais na Wizara. Niombe tu hii progamu iende kama ilivyopangwa na naamini kufikia 2018 maji yatakuwa yanatiririka katika maeneo yetu. Nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie mambo machache ambayo napenda leo nichangie, ni kuhusu masuala ya uchimbaji wa mabwawa. Tumeona kila Mbunge anazungumzia maji hapa na tumeona kuna baadhi ya maeneo mvua zinanyesha kwa kasi sana kiasi kwamba inapeleka mpaka mafuriko.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe Wizara hii iangalie katika masuala kama haya maji mengi yanapotea; tungechimba mabwawa makubwa ambayo yangesaidia kuhifadhi haya maji kwa sababu maji mengi yanapotea. Sehemu nyingine Mwenyezi Mungu amejalia tuna mvua za kutosha lakini baada ya mvua kukatika na maji yanapotea na shida ya maji inaendelea kuwepo katika yale yale maeneo ambayo mvua nyingi zilinyesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Wizara iliangalie jambo hili kwa macho mawili. Hata nikitolea tu mfano pale kwetu Choma Chankola kulikuwa na survey ilifanyika ilitolewa milioni thelathini na tano ya kuchimba bwawa na usanifu ukafanyika, lakini ule uchimbaji wa bwawa sijui umepotelea wapi, imekuwa kimya. Kila mwaka tunaulizia. Mwaka jana nilizungumza hili suala na mwaka huu tena nagusia Mheshimiwa Waziri amesahau ama ile fedha iliyotolewa milioni thelathini na tano walitoa sadaka? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini wanavyotoa fedha baadaye inafuata mipango ya utekelezaji. Sasa tumetoa milioni thelathini na tano, isipotee, naomba mabwawa haya yachimbwe katika maeneo ambayo maporomoko ya maji yapo mengi hasa Choma, Ziba pale kuna maji mengi sana na kilimo cha mpunga, lakini pia mabwawa maeneo ya Simbo nashukuru sasa hivi kuna NGO ya World Vision wana programu ya uchimbaji wa bwawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sasa Serikali mshirikiane na hii NGO ili tuweze kuhakikisha kwamba hii programu yao ya uchimbaji wa bwawa kubwa pale Simbo iweze kukamilika na kufikia mwisho ili kuhakikisha kwamba maeneo jirani yanapata haya maji ambayo yatawasaidia kwenye kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na kuchangia kwenye ishu ya mabwawa Mheshimiwa Waziri mimi nigusie; tuna miradi inayofadhiliwa ama tunaopata miradi katika maeneo yetu ya maji vijijini. Tunatumia fedha nyingi sana kutengeneza miradi ya maji katika vijiji vyetu, lakini tuna shida ya kukosa wataalam wa kusimamia ile miradi na inapelekea miradi ile baada ya muda mfupi inakufa. Kwa mfano kuna mradi wa usambazaji wa maji katika Kijiji cha Choma namba sita pale Matinje, ukienda Ziba mradi wa maji upo, ukienda Ndembezi, Nkinga na Simbo kote kuna miradi wa maji. Tatizo wanakosa wataalam wanaachiwa Serikali za Vijiji wale Wenyeviti wa Vitongoji na Wajumbe mwisho wa siku wanakusanya fedha na baada ya kupata mapato wanazila zile hela.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sisi Wizara, katika maeneo ambayo kuna miradi, tuajiri au tupeleke mtaalam pale aweze kusimamia na kuwaongoza hawa viongozi na watu ambao wanasimamia huu mradi wa maji. Niiombe Wizara iliangalie hili suala ili ihakikishe kwamba inaokoa fedha ambazo zimekwishatumika katika uchimbaji ama uwepo wa miradi ile ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niiombe Wizara katika ile miradi yao wanayopata ya ufadhili wa World Bank ya uchimbaji wa visima virefu, niombe watuangalie na sisi pale Igunga hasa Manonga kwa sababu yako maeneo yana shida sana ya maji. Tuna shida kweli ya maji hasa ukiangalia kuna baadhi ya vijiji; naweza nikamtajia ama nitamletea Mheshimiwa Waziri kwenye taarifa yake atusaidie. Kuna maeneo kama Kata za Mwamala, Uswaya, Igoweko, Kitangili, Nyandekwa na Mwansugho Ngulu, maeneo yote hayo hayana maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuiombe Wizara katika ule ufadhili wanaoupata kutoka World Bank na maeneo mengine waiangalie Wilaya yetu wahakikishe kwamba tunapata visima hivyo virefu angalau; maana bajeti imekwisha sijaona kisima hata kimoja ndani ya Wilaya yangu ya Igunga. Sasa niiombe Wizara iangalie hili suala na iweze kupitia ili waweze kutusaidia kutatua hii changamoto ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine nipende kushauri tu kwa Mheshimiwa Waziri, waliangalie kwenye Wizara. Nilihudhuria kwenye bajeti moja ya Kamati ya Fedha Wilayani pale Igunga. Tumekaa zimekuja fedha za maji milioni ishirini nafikiri, kuna mradi fulani wa maji vijijini; lakini wanasema katika hii milioni ishirini mwongozo kutoka Wizarani asilimia 30 ya fedha ni kwa ajili ya usimamizi wa miradi hii. Milioni ishirini, usimamizi ni milioni sita maana yake ni kwamba kwenye milioni ishirini unatoa sita inabaki milioni
14. Sasa kwa vijiji sijui 14 vile vitagawana shilingi ngapi ngapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu tuangalie kama ni mwongozo kweli wa asilimia 30 kama ni kweli, maana wameniambia wataalam wilayani, huu ni mwongozo wa Wizara, tunakata asilimia 30 kwa ajili ya usimamizi; nikauliza usimamizi gani? Wanasema kwamba sijui kuna mafuta na posho, ukipiga mahesabu hazifiki milioni sita au saba. Sasa leo tuna programu ya bilioniā€¦

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gulamali muda wako umemalizika.

MHE. SEIF K.S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja, niiombe Wizara ifuatilie hizi fedha ambazo zinakuja kwenye Halmashauri. Ahsante sana.