Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuzungumza bajeti hii muhimu sana ya maji, kwa sababu maji ni uhai, bila maji hatuwezi kuishi, kila binadamu lazima atumie maji ili aweze kuishi. Bajeti hii tunaiomba Serikali kwa ajili ni jambo muhimu sana kwa binadamu tunaomba iongezwe kama ilivyokuwa 2016/2017 kwa sababu maji ni uhai. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya, tunaona jinsi gani wanavyoipigania Wizara yao kwa ajili ya kufungua miradi mbalimbali. Hata hivyo, bado kaka zangu wana kazi kubwa sana kwa sababu Wizara waliyokuwa nayo ni ngumu sana inawagusa wananchi moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeomba bajeti iongezwe kwa sababu kama nilivyosema maji ni muhimu sana kwa binadamu. Vilevile ukiangalia kuna mifuko mbalimbali ambayo tunaiona imefanya kazi vizuri. Tukizingatia REA imefanya kazi vizuri sana kwa upande wa umeme. Tulikuwa tunaiomba Serikali kwenye tozo ya Mfuko wa Barabara tutoe at least shilingi hamsini, Mfuko wa Umeme tutoe shilingi hamsini ili iwe shilingi mia iende kwenye Mfuko wa Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona ni jinsi gani REA ilivyofanya kazi vizuri ndani ya vijiji vyetu; leo hii wananchi wanafurahi wanapata huduma safi ya mwanga. Sasa maji ni uhai, kila mtu anahitaji maji na tukiangalia maeneo yetu ya vijijini hakuna maji kabisa, akina mama wanahangaika. Tukienda kwenye ziara zetu, ndiyo maana unakuta Waheshimiwa Wabunge wengi wanapiga kelele kwa sababu ya maji kwa kuwa tunapokwenda kwenye ziara zetu huko tunaona hali halisia ya jinsi gani maji hakuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, akinamama wanatoka saa tisa za usiku, vijiji vingine saa nane za usiku wanakwenda kutafuta maji na akienda kutafuta maji hapati yale maji safi na salama anapata maji machafu. Matokeo yake sasa unakuta asilimia kubwa ya maji yale ya vijijini ambayo ni ya vijito kuna maradhi mengi yanapatikanika huko, watu wanaumwa vichocho na kuharisha. Halafu sasa hivi mpaka mijini kwa sababu hatutumii maji safi na salama, mjini sehemu nyingi maji hayatibiwi matokeo yake watu asilimia 90 tunapata magonjwa ya UTI.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaomba Serikali kwa hili sasa hivi lazima tujipange vizuri, bajeti ongezeke ili nchi yetu ya Tanzania tuweze kujivunia kwa hilo. Tunaomba asilimia 70 iende vijijini na asilimia 30 ibaki mjini kwa sababu mijini kuna miradi mbalimbali mikubwa ambayo inatekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende sasa kwangu Mpanda. Naomba niishukuru Serikali kwa sababu Mpanda tuna miradi mikubwa kama vile mradi wa Ikolongo ambao umefanyika na sasa asilimia 60 ya wananchi wa Mpanda wanapata maji, lakini asilimia 40 pale Manispaa hawapati maji. Hapa ndani ya ukurasa wa 66 Mpanda kuna huu mradi wa mwaka 2016/2017 tulipangiwa bilioni mbili. Huwezi ukaamini kuna watu wanatafuta maslahi yao wenyewe badala ya kutafuta maslahi ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pesa hizi zilivyofika Mpanda Tender Board imerudiwa mara tatu, mpaka leo ninavyokwambia mradi huu unakutana na pesa za bajeti hii ya 2017/2018. Mradi haujatekelezeka kwa sababu ya ubinafsi; watu wanataka maslahi yao wenyewe binafsi badala ya maslahi ya wananchi. Wananchi wa Mpanda wanahangaika maji wenyewe wanataka waweze kupata mradi wajinufaishe wao. Inasikitisha sana kwa Mpanda! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali Mheshimiwa Waziri, najua sasa hivi Tender Board ime-tender mara tatu kiasi ambacho wamekwenda kushtakiana kwa ajili ya ubinafsi. Naomba Mheshimiwa Waziri alifuatilie hili jambo ili wananchi wa Mpanda Mjini waweze kupata maji, mradi huu uweze kufanyika na hizi bilioni mbili ziweze kufanya kazi kutoka Kanoge mpaka Mpanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii Hospitali ya Mpanda Mjini ambayo wananchi tunaitegemea haina maji, na huu mradi wa bilioni mbili ulitegemewa ukifika pale maji yafike kwenye Hospitali yetu ya Mpanda Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hizi bilioni mbili ambazo zilikuwa za bajeti iliyopita ziweze kufanya kazi na kama safari hii wametupangia bajeti vilevile iweze kufanya kazi kwa sababu wananchi wa Mpanda Mjini wanapata tabu kwa sababu ya watu wachache ambao wanataka maslahi yao binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii sisi Mkoa wa Katavi tuna Ziwa Tanganyika; sisi tunafurahi wenzetu hapa wana Ziwa Victoria leo ziwa lile limewapa manufaa. Hata hivyo, sisi Wanakatavi tuna Ziwa Tanganyika ambalo lina kina kirefu, kina chake kirefu kushinda Ziwa Victoria. Kwa nini sasa Serikali na Ziwa Tanganyika… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana.